Symbion isijiingize kwenye tope la Dowans


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 25 May 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

PAMOJA na kwamba hatuna mashaka na uwezo wa kampuni ya Symbion Power LLC inayodai kuwa imenunua mitambo ya kampuni ya Dowans kuweza kuzalisha umeme, lakini ukweli ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kampuni hiyo kutumbikia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na hata kisheria.

Symbion tayari imeshapewa mikataba kadhaa nchini inayohusiana na suala la nishati ya umeme kwa kupitia Akaunti ya Changamoto ya Milenia inayofadhiriwa na Marekani na ile ya Kifaransa ya Pike ambapo wanafanya matengenezokwenye vituo vya kuzalisha umeme na kutandaza nyaya mpya za umeme chini ya bahari kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar. Mkataba huo, unakadiriwa kuwa na thamani ya Sh. 68 bilioni. Fedha hizi ni sehemu ya zaidi ya Sh. 700 bilioni zinazotolewa na serikali ya Marekani kupitia mpango huo.

Hata hivyo, kuna kesi kadhaa zilizofunguliwa mahakamani kupinga tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kibiashara (ICC) na hivyo inaweza kuzorotesha kufungwa kwa mkataba kati ya kampuni hiyo na TANESCO.

Kwa mfano, tayari jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam, Emilia Mushi ametoa amri inayopiga marufuku majadiliano yoyote yanayohusu mitambo ya Dowans kufanyika bila kibali cha mahakama yake.

Haya yalitokea baada ya kampuni ya Dowans na TANESCO kujaribu kufanya mazungumzo ya kutaka kuwasha mitambo hiyo kwa mkataba mfupi, huku kukiwa na taarifa kwamba tayari mitambo hiyo imeuzwa kwa mtu mwingine.

Hadi sasa, haijafahamika kama makubaliano kati ya Symbion  na Dowans ama hata serikali kama yamezingatia amri hiyo ya mahakama.

Kutokana na hilo hapo juu bado suala la tuzo ambayo Dowans walitakiwa kulipwa na TANESCO baada ya kushinda kesi yao kule ICA linapaswa kuelezwa linakoelekea. Kwa vile kwa kadiri tunavyojua fedha hizo hazijalipwa na kesi bado ipo mahakamani katika mabadilishano haya ya umiliki wa Dowans katika deni hili unatakiwa ufahamike.

Je, limerithiwa na kuwa ni sehemu ya madeni na mali za Symbion, ama linaendelea kuwa mali ya Dowans? Katika mazingira ya kawaida ya mikataba chombo kinachorithi mkataba kinaridhi vile vile madeni yake.

Uzuri wa hili ni kuwa kama tumekataa kuwalipa Dowans, na Symbion wanajua kuwa tumekataa kulipa kampuni hiyo na wao wameamua kuchukua mkataba wa Dowans, wajue mapema kuwa itabidi wafikirie jinsi deni hili litakavyoweza kuingizwa katika mikataba yao  kwani kama hatukuwa na fedha wala sababu ya kuwalipa Dowans, ndiyo hivyo hivyo tusivyoweza kulipa deni hilo kwa Symbion.

Lakini kuna hili pia. Kama ni kweli serikali ya Marekani kama inavyojitapa kuwa inatupenda, kwa nini isisaidie serikali kununua majenereta kutoka nchini humo kupitia mpango huo wa MMC au ACM?

Najiuliza Marekani kama nchi rafiki kwa nini wasingesaidia serikali kuagiza kwa haraka mitambo kama hiyo tena kwa bei ya chini kutoka nchini humo na ikafungwa na kuwa mali ya serikali badala ya kukodisha hii ya Dowans?

Symbion kama walivyosema wanaweza kupeleka mitambo hii sehemu yoyote duniani; kama hili ni kweli, kwanini wakishainunua kutoka Dowans wasiondoe na kuachilia eneo hilo ili serikali ilete majenereta yake yenyewe?

Ninafahamu jibu la haraka ambalo watawala wetu watalitoa katika kuhalalisha mradi wao, ni kuwa tayari kuna shida ya umeme. Kwa nini yaondolewe na kusubiri majenereta mengine ambayo hatujui yatakuja lini?

Lakini kipi kitakuwa na gharama nafuu kwa muda mrefu ujao? Kuendelea kukodisha majenereta haya na kulipia gharama nyingi za uzalishaji ikiwamo gharama za kuweka mitambo au kununua majenereta ya kwetu wenyewe ambayo hayatafungwa na kuondoa hizi gharama zisizokuwa na tija?

Kwa mfano, Symbion wangepewa mkataba wa kufunga hayo majenereta yetu mapya – kama sisi wenyewe hatuna utaalamu – kitu ambacho siamini ni kweli, mabilioni ya shilingi yangeweza kuokolewa na kutumika kwa kazi nyingine.

Kuna vitu vingi ambavyo vinahitaji majibu kabla ya serikali kujiingiza katika mradi wake huu. Kwa mfano, mwisho wa mkataba majenereta haya yatakuwa mali ya nani?

Ni wazi kuwa kabla ya mkataba kufungwa wananchi wanatakiwa kuelezwa masharti ya umiliki wa mitambo hiyo toka Symbion mwishoni mwa mkataba kati ya TANESCO na kampuni hiyo.

Lazima ifahamike kama Symbion wanachukua mkataba toka kwa Dowans na wao ndio wanakuwa wamiliki halafu wanaingia mkataba wa kuzalisha umeme na TANESCO, je mkataba ukiisha TANESCO watalazimika kununua “tena” majenereta hayo?

Au mkataba utaweka wazi na pasipo utata kuwa mwisho wa mkataba mitambo hii itakuwa ni mali ya TANESCO.

Jingine ambalo wananchi wanataka kufahamu kabla ya TANESCO kujifunga katika mkataba na Symbion, ni iwapo kama sheria za manunuzi ya umma (PPRA) ya mwaka 2004 kama itafuatwa.

Kuna kila dalili kuwa tunaweza kujikuta kwenye tatizo lilelile ambapo TANESCO inaonekana imeshaandaliwa kuingia mkataba na Symbion nje ya sheria ya manunuzi ya umma. Hili ni muhimu likazingatiwa ili yasije kujirudia yale yaliyotokea katika sakata la Richmond na baadaye Dowans.

Hadi hivi sasa, kwa vyovyote vile, sheria hii ni kikwazo kwa Symbion. Sheria hii hairuhusu kampuni hiyo kupewa mkataba bila kuwapo kwa ushindani. Na endapo upindaji wa sheria utafanyika kama ilivyotokea kwenye suala la Richmond na Dowans, basi pamoja na hicho kinachoitwa “nia nzuri ya Wamarekani” watajikuta wanarudi kwenye tatizo lile lile.

Hata hivyo, ni matarajio ya wengi kwamba kwa kuwa Wamarekani wanajua uzito wa kufuata sheria, ni matumaini yangu kuwa hawatavunja sheria ili kampuni yao ipewe mkataba.

Njia pekee inayoweza kutumika ili kuharakisha mkataba huu kwa kufuata sheria, ni kwa  Rais Jakaya Kikwete kutumia madaraka yake chini ya sheria ya dharura ya umeme (Emergency Powers) ya mwaka 1986 ambayo inampa mamlaka ya kutangaza hali ya udharura wa umeme nchini.

Chini ya sheria hiyo anaweza – baada ya kutangaza kwenye gazeti la serikali – kusitisha  baadhi ya vifungu vya sheria ya manunuzi ya umma na kutumia madaraka hayo kuingia mkataba ambao utazingatia mahitaji ya nchi.

Hii ina maana badala ya kuachilia wizara na TANESCO kwenye suala hili jambo ambalo limeachwa kufanyika kwa muda mrefu, suala hili lisimamiwe na ikulu wenyewe. Je, Kikwete baada ya daflauru alilopigwa swahiba wake – Edward Lowassa - yuko tayari kwa hilo?

Hivyo, basi wakati wananchi wanasubiri kuona suala la Symbion na Dowans linakoelekea na hasa jinsi gani lina maana kwa watumiaji wa umeme nchini na dhana nzima ya utawala bora, ni wazi kuwa maswali ya mengi ya msingi yamebakia yakisubiri kujibiwa.

Ili makosa yaliyotokea huko nyuma yasitokee tena, suala la uwazi ni la msingi sana. Kwa vile kampuni hii ya Marekani haitaki na haistahili kuonekana kuhusika au kuhusishwa na usiri unaotokana na ufisadi ni matumaini yangu kuwa endapo mkataba kati yake na TANESCO utafungwa, wananchi wataelezwa na mkataba huo utafungwa hadharani.

Hii itaweza kuisaidia serikali yenyewe kuaminika mbele ya wananchi wake na mbele ya nchi wahisani. Itasaidia pia kuwafanya watendaji serikali kuingia mkataba wenye tija badala ya kila kukicha kuingiza nchi katika mikataba ya kikandamizaji na unaobebesha mzigo Watanzania.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: