Symbion: Mwanzo au mwisho wa kashfa?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 June 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

SERIKALI ya Rais Jakaya Kikwete iliridhia mapendekezo ya Bunge ya kuvunja mkataba wa kufua umeme kati yake na kampuni ya Dowans Holdings SA.

Sababu zilikuwa kuthibitika kuwa kampuni hiyo ilirithi mkataba wa Richmond Development Company (LLC) uliopatikana kinyume cha taratibu.

Ni serikali iliyozuia Tanesco kuingia mkataba na aliyejiita mmiliki wa makampuni ya Dowans Tanzania Limited (DTL) na Dowans Holdings SA ya Costa Rica, Brigedia Suleiman Mohammed Al Adawi.

Umeme ulihitajika sana na mashine zilikuwepo. Lakini kwa jina la utawala bora, serikali ililazimishwa, hata kama siyo waziwazi, kujiepusha na mitambo iliyotumika kuleta kashfa iliyong’oa waziri mkuu na kuvunjwa kwa serikali ya kwanza ya Kikwete.

Sasa tunaambiwa kampuni ya Marekani iitwayo Symbion, imenunua mitambo ya Dowans. Hivi mitambo hiyo imenunuliwa kutoka kwa nani?

Kutoka kwa Rostam Aziz ambaye, tarehe 28 Novemba 2005 alipewa nguvu ya kisheria (Power of Attorney) kushitaki, kusimamia, kununua au kuuza hisa za kampuni ya Dowans pale atakapoona inafaa?

Kama Rostam siye aliyeuza mitambo hii, Symbion wameuziwa na Bregedia Alawi, au Bernal Zamora Arce anayejiita rais wa kampuni hiyo, au Noemy del Carmen Cespedes Palma ambaye ni mwanasheria wa kampuni?

Nani hasa aliyeuza mitambo hii? Serikali imtaje ili kuepuka kuingia katika migogoro mingine mikubwa ya kisheria. Hii ni muhimu kwa sababu, nyaraka zinaonyesha kampuni ya Dowans Holdings SA (Costa Rica) inamilikiwa na Bernal Zamora Arce.

Lakini Bregidia Al Adawi amekana Bernal Zamora Arce kumiliki kampuni hiyo, ingawa anatambua ndiye alimpa nguvu za kisheria Rostam.

Hapa kuna kitu. Kwa hali ya kawaida, haiwezekani Brigedia Al Adawi kumkana Zamora lakini papo hapo akatambua nguvu za kisheria zilizotolewa na Zamora kwa Rostam.

Haiwezekani pia kwa Brigedia Al Adawi kumkana Bernal Zamora, wakati ambapo nyaraka zote za Dowans Holdings SA ya Costa Rica zinamuonyesha kuwa huyu ndiye mwenye kampuni.

Kabla ya mitambo ya Dowans/Symbion kuleta kasheshe, serikali itafute majibu ya maswali hayo. Ieleze vipi Dowans Tanzania Limited imeweza kuingia katika mkataba kati ya serikali na kampuni ya Dowans Holdings SA wakati katika kipindi chote cha mgogoro kati ya Richmond na Dowans, taifa hili halikuwahi kusikia kinachoitwa, “Dowans Tanzania Limited.”

Hata uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya Biashara (ICC) wa 15 Novemba 2010, unaagiza Tanesco kulipa Sh.185 bilioni kwa makampuni ya Dowans Holdings SA (Costa Rica) na Dowans Tanzania Limited (DTL).

Kampuni ya Dowans Holdings SA (Costa Rica), iliwahi kutajwa na msajili wa makampuni nchini Costa Rica kuwa haijawahi kusajiliwa nchini humo.

Mkataba wa Symboni na Tanesco, ni zao la mkataba tata kati ya serikali na Richmond kwa upande mmoja; na makampuni ya Dowans na serikali kwa upande wa pili.

Kutokana na hali hiyo, hatua ya serikali kuruhusu Symbion kuuza umeme wa mitambo yenye kashfa, kunachochea mifarakano zaidi.

Kwa macho yanayoweza kuangalia kila jambo kwa mapana yake, hakika utabaini kuwa kinachofanyika katika mikataba hii, ni mabadiliko ya kanzu tu; lakini shekhe bado ni yuleyule.

Mkataba kati ya serikali na Dowans hauwezi kuwa halali bila kuihusisha Richmond kwa kuwa kampuni hiyo ndiyo iliyoingiza katika gridi ya taifa megawati 20 za awali za umeme.

Vilevile, ndani ya mkataba huu ndimo Richmond ilikopata haki ya kusikilizwa katika shauri ililofungua huko Houston, Texas, Marekani ambapo wanasheria wa kampuni hiyo wameomba mahakama iiruhusu Richmond kunufaika na fedha zitakazolipwa Dowans na Tanesco.

Jambo jingine ambalo serikali inapaswa kuliweka wazi ni juu ya madai yake kuwa imeagiza Tanesco kuzima mitambo yake ya Ubungo Gas Plant ambayo inamilikiwa na Tanesco ili kuipisha Symbion izalishe umeme kwa kutumia mitambo ya Dowans.

Mitambo inayodaiwa kuzimwa kupisha Symbion ili iweze kuzalisha umeme, ni mali ya Tanesco. Mitambo hiyo haihitaji kulipiwa gharama za kuihifadhi pale ilipo – capacity charge.

Bali mitambo ya Symbion ni ya kukodi. Mbali na kulipia gharama za kuiweka pale, Tanesco wanalipia umeme unaozalishwa.

Kuzimwa kwa mitambo ya gesi kunatokana na madai kuwa gesi inayozalishwa katika kisiwa cha Songo Songo, kilichopo wilayani Kilwa mkoani Lindi, haitoshi kuendeshea mitambo hiyo kwa sasa.

Lakini wakati Symbion haiwezi kuingiza kwenye gridi ya taifa megawati 120 za umeme kwa wakati mmoja, serikali inalazimika kulipa kampuni hii gharama za kuhifadhi mitambo Ubungo.

Hadi sasa, hakuna anayefahamu kiasi cha fedha kinacholipwa kwa ajili ya kazi hiyo. Si Tanesco wala Symbion waliokubali kutaja kiasi cha fedha kinacholipwa.

Kinachofahamika kwa wengi ni kwamba, kampuni ya Richmond ambayo ndiyo ilikuwa na mkataba na Tanesco, ilikuwa inalipwa kiasi cha Sh. 155 milioni kwa siku.

Mpaka juzi Jumatatu, kuna taarifa kwamba visima vitano kati ya 10 vinavyozalisha gesi kisiwani Songo Songo, viko katika hali mbaya ya kulipuka kutokana na kushindwa kuhimili mkandamizo wa gesi. Mabomba yanayosafirisha gesi hiyo kutoka ardhini yamedaiwa kuchakaa na hayafanyi kazi kama inavyotakiwa.

Visima vilivyoathirika kwa kutu hiyo na ambavyo inadaiwa viko hatarini kulipuka, ni kisima “SS 3” na “SS 4.” Kisima “SS 5” tayari kimeharibika kabisa.

Sasa lipi lilitakiwa kuanza: Serikali kufanyia matengenezo mabomba hayo au kuingiza nchi katika mkataba mwingine wa kuzalisha umeme ambao hautakuwa na tija? Mitambo ya Symbion inatumia gesi na serikali haina uhakika wa kupatikana kwa gesi hiyo.

Pamoja na kwamba gesi inayozalishwa ni mali ya serikali na ilivumbuliwa na Shirika la Maendeleo ya Mafuta la Taifa (TPDC), lakini katika uendelezaji unaohusisha uchimbaji na usafirishaji – serikali imeweka mwekezaji – kampuni ya Song Gas kutoka Canada. Huyu ndiye anayegawana faida na serikali.

Lakini Song Gas wamekabidhi jukumu hilo kwa mkandarasi mwingine – kampuni ya Pan African Energy Tanzania. Hapo ndipo tatizo la msingi linapoanzia.

Song Gas inadaiwa kuweka maslahi ya pesa mbele. Imeamua kuuza gesi katika viwanda na makampuni kadhaa ya jijini Dar es Salaam badala ya kukarabati visima hivyo.

Gesi ya Songo Songo hutumika kuzalisha umeme katika mitambo mbalimbali ikiwamo Song Gas uliopo Ubungo (Megawati 80), Tegeta (Megawati 45) na mitambo mingine inayozalisha karibu megawati 250 ambazo ni zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa na Tanesco kwa sasa kupitia maporomoko ya maji.

Tutegemee nini kutoka Symbion? Migogoro ileile au kashfa zilezile? Je, huu ndio mwisho au mwanzo wa kashfa mpya? Mara hii, nani ataanguka na Symbion/Dowans?

0
Your rating: None Average: 4.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: