Synovate wametumwa na nani?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WAKATI mwingine ni vigumu kuamini namna nchi yetu inavyoruhusu mambo yaende kienyeji bila ya kuangalia maslahi ya taifa baadaye.

Tuchukulie mfano wa taasisi ya Synovate ambayo imekuwa ikijishughulisha na mambo ya utafiti na masoko katika nchi mbalimbali duniani.

Katika siku za karibuni, taasisi hii imekuwa maarufu kwa utoaji wake wa utafiti wa hali ya kisiasa nchini. Katika eneo la utafiti mimi sina shida kabisa na hilo; shida yangu ipo kwenye aina ya utafiti unaofanyika.

Tatizo langu na taasisi kama hii linakuja pale inapoingia kwenye utafiti wa hali ya kisiasa nchini. Hivi, tunaruhusu vipi kampuni ya kimataifa ije kufanya utafiti wa hali ya kisiasa nchini?

Naweza kuwa sikubaliani na utafiti unaofanywa na taasisi ya REDET ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini angalau hii ni taasisi ya ndani ya nchi yetu ambayo inaweza kuwa inaangalia maslahi ya taifa kwa namna moja au nyingine.

Lakini taasisi kama Synovate, ni nani ambaye anajua sababu ya wao kufanya utafiti wa jambo nyeti kama hili ndani ya nchi yetu? Nani amewatuma Synovate kufanya utafiti wao hapa kwetu?

Kuna mfano rahisi sana ninaoweza kuusema kuwahusu. Hebu fikiria, kama watasema ni asilimia nne tu ya Watanzania wana imani na rais wao, na wakarudiarudia maneno hayo walau mara 10, unafikiri nini kitatokea kwa nchi yetu?

Taasisi ya kigeni inawezaje, kwa mfano, kufanya utafiti kuhusu imani ya wananchi wa Tanzania kwa serikali yao au kiongozi wao mkuu? Je, tunafahamu sababu ya wao kutaka kujua hilo?

Labda nirudi kwenye swali langu la msingi; Nani amewatuma Synovate?

Synovate ni tawi la kampuni ya kimataifa ya Aegis Group lililosajiliwa katika Soko la Hisa la London likiwa na ofisi karibu katika mabara yote duniani. Aegis ina matawi mawili, Synovate na Aegis Media.

Aegis huwa inajihusisha na masuala ya utafiti na mawasiliano. Kazi yake kubwa ni kusaidia wateja wake kupata taarifa mbalimbali kuhusu hali ya soko ilivyo pamoja na tabia za watumiaji wa bidhaa.

Wateja wa Aegis ni watu binafsi, makampuni, taasisi na wafanyabiashara ambao wanataka bidhaa au mambo yao yaende vizuri mbele ya watu.

Kwa mfano, kama wewe unamiliki kiwanda cha CocaCola, unaweza kuwafuata Aegis na kuomba wakupe taarifa kuhusu nini ambacho wateja wanataka, kama wanapenda soda yako au hawapendi.

Hata sisi MwanaHALISI tunaweza kuwasiliana nao na kutaka watuambie ni kwa vipi gazeti hili litaendelea kuwa kinara katika mauzo ya gazeti.

Kwa hiyo Aegis, kwa kuitumia Synovate, watafanya utafiti na watatuletea matokeo. Wanaweza wakataka tupunguze au tuongeze bei, wanaweza wakatuelekeza kuhusu maeneo mapya ya kuuzia magazeti na vitu vingine.

Na haya si maneno yangu. Ukienda kwenye tovuti ya Aegis, www.aegisplc.com, utaona maandishi yanayosomeka ifuatavyo;

“They do this in many ways: by helping clients understand what consumers are thinking and how they are spending their time, and by enabling them to communicate with consumers at the right moments and in the best way.”

Kwa tafsiri yangu na si ya neno kwa neno, Synovate huwasaidia wateja wake kufahamu ni nini wateja wanachofikiri, wanavyotumia muda wao na namna bora ya kuwasiliana na watumiaji wa bidhaa zao katika wakati muafaka na kwa namna mwafaka.

Kwa hiyo, katika hali ya kawaida, Synovate inatakiwa kufanya kazi yake kwa mujibu wa aliyewatuma kufanya kazi. Na wameshafanya kazi nyingi za namna hii, chini ya mwavuli wa Aegis, ikiwamo hata kwenye kuandaa orodha ya watu matajiri zaidi duniani inayoandaliwa na jarida la Forbes la Marekani.

Ndiyo maana, yalikuwapo maswali mengi wakati Aegis ilipoamua kuinunua iliyokuwa Steadman Group mnamo mwaka juzi. Steadman, pamoja na kuwa na ofisi katika nchi kadhaa za Afrika, ilikuwa ikifahamika kama kampuni ya Kenya.

Ilipata umaarufu mkubwa katika chaguzi mbalimbali za Kenya miaka michache iliyopita kutokana na tabia yake ya kutoa matokeo ya utafiti wa nani atashinda uchaguzi wa nchi hiyo.

Aegis ilifahamika kwamba haikuwa ikifanya aina hii ya utafiti wa kura za maoni. Kwa hiyo, uamuzi wa kampuni hii kuinunua Steadman ulizusha maswali mengi lakini kubwa zaidi likiwa; itakuaje kuhusu mambo ya kura ya maoni?

Ndiyo maana, Mkurugenzi wa Synovate kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Jon Stalters, aliwahi kunukuliwa na mtandao wa AllAfrica.com mwaka juzi akisisitiza kwamba pamoja na ununuzi huo wa kampuni hiyo ya Kenya (bei ya uuzwaji wa kampuni hiyo haifahamiki hadi leo), utaratibu wa kura za maoni utaendelea.

Bila shaka, inawezekana Steadman walilazimisha kwamba hata kama mambo ya utafiti wa kura za maoni hayapo kwenye taratibu za Aegis, ni lazima yaendelee kuwapo chini ya Synovate.

Swali linakuja, ni kwa nini ni muhimu kwa Synovate kuendelea na utaratibu huo hata kama kimataifa Aegis hawana utaratibu huo? Kuna kampuni gani inanufaika na kujua iwapo CCM au CUF inapendwa sana?

Ni nani ananufaika kibiashara kama Kikwete anapendwa au kuchukiwa na asilimia 65 ya Watanzania? Ni nani anafaidika kwa kuambiwa kwamba wananchi wa Tanzania wanafurahishwa na utendaji kazi wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuliko Rais Jakaya Kikwete?

Ninafikiri kwamba Aegis hawawezi kukubali Synovate ifanye utafiti wa namna hii pasipo kuwa na sababu au faida ya kufanya utafiti. Ama kuna mtu amelipia utafiti huo (na matokeo ni lazima yamfurahishe) au wenye kampuni wana maslahi binafsi na utafiti huo.

Hebu tujiulize, Synovate wanapofanya utafiti kuhusu wabunge waliofanya vizuri zaidi bungeni na kumchanganya Pinda, Spika wa Bunge, Samweli Sitta na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wana maana gani.

Pinda ameuliza maswali mangapi bungeni? Sitta ameuliza maswali mangapi bungeni. Hivi kwa nini utafiti usimhukumu Sitta kama Spika wa Bunge na Pinda kama Waziri Mkuu badala ya kuwaona kama wabunge?

Haya ni maswali ambayo taifa linapaswa kujiuliza. Kama tutasubiri makampuni ya nje ya nchi yaje kutuambia hatumtaki rais wetu ndipo tushtuke, basi tujiandae kulia siku moja.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: