Syria imejitumbukiza katika vita


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version

MWAKA mmoja tangu Syria iingie katika machafuko ya kisiasa yanayolenga kumwondoa madarakani rais wa nchi hiyo, Bashar Assad, Shirika la Msalaba Mwekundu limekiri kuwa nchi hiyo sasa imeingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Maelezo hayo ya shirika hilo yalitolewa  Jumapili wakati wachunguzi wa Umoja wa Mataifa (UN) wakikusanya taarifa mpya zinazoonyesha kuwepo na idadi kubwa ya watu waliouawa katika kijiji cha Tremseh.

Taarifa zinasema kuwa baada ya kutembelea kwa mara ya pili sehemu hiyo ya Tremseh Jumapili, timu hiyo ilisema kwamba wanajeshi wa Syria walienda moja kwa moja katika kijiji hicho cha wafugaji, wakakagua vitambulisho vya wanavijiji na kuwaua huku wakiondoka na watu wengine.

Kwa mujibu wa taarifa ya UN, shambulio hilo liliwalenga wapinzani na wanaharakati.

"Mito ya damu na ubongo uliosambaa viligunduliwa katika nyumba nyingi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, serikali ya Syria imepinga taarifa hiyo kwamba serikali ilitumia silaha kubwa katika shambulio hilo lililotokea Alhamisi iliyopita.

Msemaji wa Mambo ya Nje wa Syria, Jihad Makdissi alisema kwamba vurugu hizo hazikulenga kusababisha mauaji – tofauti na jinsi wanavyodai wanaharakati na viongozi wengi wa nchi za nje – lakini operesheni hiyo ya kijeshi, ilililenga katika kupambana na wapiganaji waliokichukua kijiji.

"Kilichotokea halikuwa shambulio kwa raia," Makdissi aliviambia vyombo vya habari katika mji wa Damascus. Alisema kuwa wapiganaji 37 waliokuwa na silaha waliuawa pamoja na raia wawili.

Alisema zaidi kuwa “kilichosemwa kuhusu kutumika kwa silaha kubwa hakina misingi.” Hata hivyo, timu ya UN inasema kuwa zaidi ya watu 100 waliuawa na kwamba lawama zote zinaelekezwa kwa rais Assad. Hayo yalisemwa na kiongozi wa uchunguzi wa UN.

Taarifa zaidi zinasema kuwa machafuko hayo ni moja kati ya mapambano yaliyotokea hivi karibuni ya kumpinga Assad, ambayo wanaharakati wanasema mpaka sasa yamesababisha vifo vya watu 17,000.

Umwagaji wa damu nchini humo unaonekana kuongezeka kwa kasi. Jumapili, Tume ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ilisema sasa inayachukulia machafuko hayo kuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe na wakataka zitumike sheria za kimataifa za haki za binadamu nchini humo.

"Kwa sasa tunazungumzia uwepo wa majeshi ya kimataifa usio na machafuko ndani ya nchi," alisema msemaji wa ICRC, Hicham Hassan.

Taarifa zaidi zinasema kuwa katika siku za nyuma, shirika hilo lilikuwa likitoa taarifa za machafuko katika mitandao ya Idlib, Homs na Hama. Lakini Hassan alisema kuwa shirika hilo lilihitimisha kwa kusema kuwa vurugu zilikuwa zikisambaa katika maeneo mbalimbali.

"Uadui umeenea katika sehemu nyingine za nchi, sheria za kimataifa za haki za binadamu zinatumika katika maeneo yote ambapo uadui unatokea," alisema Hassan.

Ingawa machafuko nchini humo yamedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja, tume imekuwa ikisita kuviita vita hivyo kuwa ni vya wenyewe kwa wenyewe japokuwa wengine, wakiwemo maofisa wa UN wameviita hivyo.

Pale ambapo shirika la Msalaba Mwekundu linaposema kitu “kinakuwa ni cha kuvutia na uhakika," alisema Louise Doswald-Beck, ambaye ni profesa wa sheria za kimataifa katika taasisi ya Geneva Graduate.

Hata hivyo, Stephen M. Saideman, ambaye ni profesa katika shule ya masuala ya kimataifa ya Norman Paterson, Ontario-Canada, alihoji endapo mapendekezo ya shirika hilo yatabadilisha kitu kwa upande mwingine.

“Assad na wafuasi wake hawataacha kupambana au kubadilisha msimamo wao kwasababu watapoteza mengi” alisema Saideman.

Jumamosi iliyopita, wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliingia katika kijiji cha Tremseh ambacho kina idadi ya watu 6,000 mpaka 10,000 katika maeneo ya kilimo karibu na mto Orontes, Kaskazini Magharibi mwa mji wa Hama.

Hapo ndipo walipogundua damu nyingi katika nyumba za watu hao, huku wakiokota maganda ya risasi zilizotumika pamoja na silaha nyingine. Ushahidi huo unatosha kuthibitisha kile ambacho wanaharakati wanakiita “tukio lenye idadi kubwa ya mauaji tangu kuanza kwa machafuko.”

0
No votes yet