Tabasamu usoni mwa yatima


Leah Mwanyakule's picture

Na Leah Mwanyakule - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version

KATIKA eneo lenye upepo mkali, Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, baridi inaongezeka wakati msimu wa baridi unavyokaribia. 

Watoto wanacheza pekupeku lakini hawaonekani kujali hali ya hewa, huku majani ya miti yakipeperushwa kulia na kushoto kufuata mwelekeo wa upepo.

Kadri unavyokaribia miti mingi, ndivyo baridi nayo inavyozidi katika mitaa iliyonyooka kuelekea sehemu moja tu – Shule ya Sekondari ya Wasichana, Ifunda.

Beatrice Mbilinyi ni mwanafunzi katika shule hiyo, na dhamira yake ni kusoma na kuwa mhandisi.

Anaonekana mwenye afya njema na anatabasamu la bashasha usoni mwake.
Lakini nyuma ya tabasamu hilo kuna hadithi ya kutia simanzi ya namna binti huyo alivyolelewa, kukua na kisha kuwekwa kwenye kundi la watoto walio katika mazingira hatarishi.

“Wala sijui baba yangu alipo. Kwanza hata simfahamu.  Ninachokifahamu ni kwamba ubini wake ni Mbilinyi na hata hilo nililijua baada ya mama yangu kufariki mwaka 2000. Kabla ya hapo ubini wangu ulikuwa kutoka kwa mama yangu, akina Kyaruzi,” anasimulia.

Na kila alipojaribu kumuulizia baba yake, hakupata jibu.

Beatrice alizaliwa na kukulia wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya ambako mama yake aliishi. Alikuwa na wadogo zake wawili.

Baba wa watoto hao akatoweka, na wakaanza kuishi katika mazingira ya umasikini mkubwa na walihitaji msaada, hasa baada ya mama yao kufariki dunia.

Mama mdogo wa Beatrice akaamua kumchukua ili kumlea, lakini hata yeye mwenyewe alikuwa na familia ya kuhudumia, na hivyo suala la elimu kwa Beatrice likawa tatizo.

“Ndio nilienda shule kwa kuwa ilikuwa ni shule ya msingi, lakini hali ilikuwa ngumu sana. Chakula hakikutosha na hata kupata sare ya shule ilikuwa shughuli,” anakumbuka.

Lakini hilo halikumzuia Beatrice kufanya vema katika masomo na kuchaguliwa kujiunga shule ya sekondari ya Vwawa.  Aliamua kujikita katika masomo na shirika lisilo la kiserikali Action for Development Programme (ADP) lililopo wilayani Mbozi likaamua kumsaidia ili aweze kumaliza masomo yake bila matatizo.

Wakati maisha ya Beatrice yakianza kuwa mepesi, akili yake nayo ikazidi kukua.  Alimaliza kidato cha nne mwaka jana na kufaulu kwa kupata daraja la pili. 

Baada ya kumaliza alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana, Ifunda na sasa amebobea katika masomo ya Fizikia, Kemia na Hesabu.

Emmanuel Kayombo alikuwa mwalimu wa hesabu wa Beatrice katika Shule ya Sekondari, Vwawa na anakumbuka jinsi binti huyo alivyokuwa “kipanga” darasani, hasa katika somo lake.

“Kwa kweli alikuwa anajitahidi sana.  Kulikuwa na idadi kubwa tu ya watoto walio katika mazingira hatarishi katika darasa lao; lakini ulikuwa ukiona dhahiri kwamba wengine wala hata hawajishughulishi kujisomea hata katika makundi,” anaeleza. 

Lakini ilipokuja kwa Beatrice, alikuwa akichukua hatua za hadi kuwasumbua walimu kumpatia mitihani iliyopita na hata msaada mwingine pale anapotindikiwa kimasomo.

“Wote tulijua kwamba atafaulu mitihani yake, na ndio maana hata majibu yalipokuja wala hatukushangaa kuona amefanya vizuri,” anasema mwalimu Kayombo kwa kujigamba.

Burhani Ngatumbula alikuwa mwalimu wa Beatrice katika somo la Kemia, naye pia anakiri kwamba binti huyo alikuwa mwanafunzi bora.

Anasema, “Alikuwa makini katika kila kitu; iwe ni katika masomo, heshima na hata ushirikiano na wenzake.”

Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Vwawa, Laurian G. Changalima anasema shule yake ina watoto walio katika mazingira hatarishi wapatao 76 na si wote wanaofaya vizuri darasani kama Beatrice.

“Hii ni kwa sababu maisha wanayoishi watoto hawa ni magumu sana, na ni vugumu kwao kufanya vizuri katika masomo; wanachokihitaji watoto hao ni ushauri wa kisaikolojia.”

Anasema, “Mtoto aliye katika mazingira hatarishi anaweza kupewa sare ya shule na kulipiwa ada na kuondolewa michango mingine; lakini endapo anarudi katika nyumba isiyo na kitanda, au nyumba wanayopata mlo mmoja kwa siku, kujishughulisha na masomo linakuwa tatizo.”

Anaomba wafadhili wasisaidie tu ada na vifaa vya shule, bali wasaidie pia kujenga hosteli ambazo watoto hao watalala, ili waondokane na mazingira ya kufikiria sehemu ngumu wanazoishi, na badala yake wajikite katika masomo.

“Hosteli inaweza kusaidia idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.  Watoto kama Beatrice wanakuja na kuondoka pindi wanapomaliza shule, lakini wengine wengi watafaidika na hosteli ambayo itaendelea kuwepo na kusaidia vizazi vijavyo,” anasema Mwalimu Changalima.

Kwa upande wa Beatrice, safari yake ya mafanikio ndio kwanza imeanza.  Japokuwa hana hakika kama anataka kuwa mtaalam wa kompyuta au mhandisi wa maji, jambo moja analolijua ni kwamba hataki kuwa mjenzi wa barabara.

“Mm, hapana,” anasema huku akicheka wakati akijubu swali endapo angependa kuwa mjenzi.  “Najua kwamba sitakuwa huko, lakini kadri siku zinavyoendelea ndivyo nitakavyofahamu ni nini ninachokitaka; lakini bado itakuwa inahusiana na mambo ya uhandisi,” anasema.

Na bado hajakata tamaa kuhusiana na baba yake.

“Nilikuwa nikimuulizia mara nyingi, lakini wakati huo nilikuwa mdogo.  Kwa sasa nimekua na dhamira yangu ni kujaribu kumtafuta mwenyewe.  Natamani kama ningefahamu japo hata rafiki zake, na huenda ningeanza kwa kuwahoji hao,” anaeleza.

Licha ya kila kitu ambacho yeye na wadogo zake wamekipitia, Beatrice anasema kwamba bado angependa kumwona baba yake.

“Nitafurahi kumwona. Lakini baada ya vicheko vyote na kuungana, bado atatakiwa anijibu maswali yangu ya kwa nini alitutelekeza miaka yote hiyo. Mwisho wa yote, bado ni baba yangu,” anasema kwa tabasamu.

ADP, ni shirika linalojishughulisha na kuleta maendeleo katika jamii za nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

Shirika hilo linashirikiana na Pact Tanzania, shirika la kimataifa linaloratibu mradi wa kusaidia watoto walio katika mazingira hatarishi ujulikanao kama Jali Watoto. 

Mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupunguza Makali ya Ukimwi (PEPFAR) kwa kupitia Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Mradi wa Jali Watoto na kampeni ya kupinga unyanyapaa, umeanza Januari mwaka 2006 na umefanikiwa kuimarisha maisha ya watoto pamoja na familia zao kwa kusaidiana pia na Idara ya Ustawi wa Jamii.

Beatrice ni mmoja wa mamia ya watoto kutoka Mbozi ambao wamepokea msaada kupitia mradi wa Jali Watoto. 

Hata hivyo, maisha ya watoto walio katika mazingira hatarishi huko Mbozi bado si mazuri, na watoto hao wanazidi kuongezeka kutokana na kuenea kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi. Watoto wengi wanaachwa yatima, katika mazingira magumu.

0
No votes yet