Taifa la JK linajiendea lenyewe


Eligius Mulokozi's picture

Na Eligius Mulokozi - Imechapwa 11 June 2008

Printer-friendly version

Lazima tukubaliane kwamba taifa hili kwa sasa halina viongozi wa kutoa mwelekeo, lawama zote zikiendee Chama Cha Mapinduzi (CCM) Chama tawala. Inasikitisha sana kwa taifa aliloliasisi hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JK) limepatwa na ukoma wa uongozi. Pengo la uongozi kwa sasa liko dhahiri, matumaini ya wananchi yameteketea.Watu tuliowatuma watuletee maisha bora hawaeleweki vipaumbele vyao. Kila kukicha maisha ya mtanzania yanazidi kuwa magumu huku watawala wakijilimbizia 'Vijisenti'. Sauti ya umma unaoteseka kwa ufukara haisikilizwi tena na watawala, watawala hawajui hisia za Watanzania. Imefika wakati baadhi ya wananchi wanajuta kuwa Watanzania, hakika uzalendo umeanza kuwaishia. Haya yote yamesababishwa na watawala wetu wasio sikiliza maoni ya watu waliowatuma kuwafanyia kazi.

Ni vigumu kujua watawala wetu viburi walivyonavyo wanavitoa wapi. Maana mamlaka ya mwisho ni umma. Kuna mambo mengi ambayo yamepigiwa kelele na umma lakini watawala wanayabeza, imefika wakati sasa umma wenyewe uamue hatma ya taifa lao. Hoja hii ni kwa sababu watawala wetu sio wawakilishi tena wa wanyonge. Kwa hali ilivyo itafika wakati Umma utataka Rais Kikwete ajiuzulu kwa makosa ya wasaidizi wake, naomba tusifikie huko lakini umma ukiamua ni nani atabisha!

Katika haya yote Chama cha Mapinduzi(CCM) kinatia aibu, hakuna aliyetarajia kama watawala waliojiuzulu kwa kashfa za ufisadi kama wangeendelea kuwa wanachama wake, hii ni aibu!! Haiwezekani chama kiendelee kukumbatia watu wenye dosari alafu chenyewe kisiwe na kasoro. Tumefika wakati mtu anayejiuzulu kwa tuhuma za ufisadi serikalini anaandaliwa na Chama mapokezi ya kishujaa jimboni kwake. CCM kwa sasa kimekuwa chama kinachowalea dhahiri watu wenye dosari tofauti na enzi za JK. Kuwa na kashfa za aina yoyote kulitosha kuwa kigezo cha kuvuliwa uanachama.

Kuonesha jinsi CCM inaugua kansa ya uongozi ni hoja za viongozi wake kwamba 'Ufisadi ni wa wanachama wake na wala usihusishwe na chama chenyewe' hapa tunaweza kukubaliana kwamba watawala wetu na watawala wa chama tawala hawajui wanachokifanya, hivi ni kweli unaweza kutenganisha chama na wanachama wake? Chama kama chama ni nadharia kiukweli chama ni ujumla wa wanachama wake. Ukiondoa mwanachama mmoja mmoja mpaka mwisho hatuwezi kuwa na chama, ndio maana inaleta maana ya kipuuzi kusema ufisadi unaofanywa na Wanachama wa CCM usihusishwe na chama. Sijui kwa watu wa aina hii kwao chama ni nini nje na wanachama. Niseme kwamba kama chama kinawanyamazia watu wenye madoa hakika chama hakiwezi kukwepa kuwa na madoa, kama chama kinafuga mafisadi chama hakiwezi kukwepa kuitwa Chama Cha Mafisadi (CCM). Hoja yangu imetokana na ukweli kwamba tabia ya mtu mmoja mmoja (Individuals behavior) inapelekea tabia ya Oganaizesheni (Organization behavior) hivyo tabia za mwanachama huwezi kuzitenganisha na chama. Kwa mantiki huwezi kukuta chama kiadilifu kama hakina wanachama waadilifu. Huwezi kuwa na taifa lenye dira kama linaongozwa na chama tawala kisichokuwa na Dira. Mzee Joseph Butiku alishatahadharisha kuhusu Chama cha Mapinduzi (CCM) kukosa Dira,leo hii taifa chini ya chama hicho kama chama tawala halina dira, taifa linajiendea lenyewe bila uelekeo wowote.

Tulitarajia chama tawala kitoe mwelekeo wa taifa hili lakini kimeshindwa na kuliacha taifa hili libaki njia panda, hakika taifa letu liko katika mtanzuko mkubwa. Matatizo yanayotokea serikalini huwezi kuyatenganisha na chama cha Mapinduzi, sijui kama wenye fikra mgando na wahafidhina na hapo watatuambia kwamba mafanikio au matatizo ya serikali ya awamu ya Nne yasihusishwe na Chama cha Mapinduzi (chama tawala)? Wenye tuhuma mbalimbali wanaendelea kutamba utafikiri taifa halina uongozi. Hata wakijiuzulu bado wanaendelea kuenziwa na watawala kama mashujaa walioshinda vita. Mpaka leowatanzania hawaamini kama ni Rais Kikwete aliyesema kwamba ?Kujiuzulu kwa Edward Lowassa ilikuwa ni ajali ya kisiasa', Watanzania hawakutarajia kama Rais wa wananchi angetoa kauli ile. Hii ilikuwa na maana gani? Kwamba anayetuhumiwa kwa ufisadi asijiuzulu, kwamba Lowassa alifanya makosa kujiuzulu japo alituhumiwa? Tuliandika makala nyingi kuonesha madoa ya Andrew Chenge lakini Rais akaendelea kumteua kushika wadhifa serikalini mpaka ilipokuja kutoka ripoti ya uchunguzi ya vyombo vya magharibi na kuandikwa na gazeti la kimagharibi (The Guardian la Uingereza) kuhusu 'Vijisenti vya Chenge' hali hii ni kwamba Rais naye hasikilizi maoni na mapendekezo ya wananchi waliomuweka madarakani. Watanzania kupitia magazeti ya hapa nyumbani na vyombo vingine vya habari vilishasema sana kuhusu suala hilo lakini walibezwa na kupuuzwa. Tukubaliane kimsingi kwamba Rais ni mtumishi wa umma, anatakiwa kuwa mnyenyekevu na msikivu kwa umma. Umma umemwajiri Rais kwa kura zao hivyo lazima asikilize matakwa yao.

Mpaka sasa huwezi kujua ni waziri gani anamudu wizara ipi?, mabadiliko ya mara kwa mara hayawezi kuleta ufanisi. Ndani ya miaka miwili na nusu waziri mmoja anahama zaidi ya wizara tatu mpaka nne, hakika hatuwezi kufikia malengo. Baraza la mawaziri la Rais Kikwete halina tofauti na timu ya Taifa chini ya Kocha Marcio Maximo, huwezi kutarajia mafanikio kwa kubadili timu mara kwa mara. Watu wengine wanaweza kusema kwamba pengine ni mbinu ya kuja kujitetea kwamba wachezaji (Watendaji) walikuwa hawajazoeana hivyo tusingeweza kushinda. Mazoezi(Semina elekezi) ya timu hizi (Mawaziri na Taifa stars) huko Ngurdoto na Brazili hayana matunda yoyote maana tumeishia kuzibadilisha timu mpaka na kupoteza rasilimali ambazo zingesadia kutatua kero nyingine. Mbona Rais ameacha kuzunguka mawizarani kusikia mikakati ya mawiziri? Tangu wakati ule alipozungukia mawizarani nadhani ni mawaziri wachache mno waliobaki wizara zilezile, wengi wao wameshazunguka mpaka wameshajichanganya. Rais hawezi kuzizungukia wizara tena maana ameelemewa na kazi ya Kuapisha mawaziri na viongozi wengine kila mara, Ziara za Ng'ambo na mikutano mingimingi imeshamchosha Rais wetu.

Watendaji wa Chama tawala wamebaki kupiga propaganda badala ya kuhimiza serikali kutekeleza ilani ya uchaguzi. Wakati huu ndio ulikuwa muda muafaka wa Rais kuzunguka nchi nzima na Mawaziri wake kuhimiza Kilimo ili kuepukana na baa la njaa linaloinyemelea Dunia. Huu ndio ulikuwa wakati muafaka wa kutoa Fedha kila mkoa ili kununua mbegu na pembejeo za kilimo na sio kusubiri hatari ya njaa iwe kubwa ndio tuanze kuzunguka Dunia nzima ili kuombaomba chakula, ni aibu kwa taifa kama Tanzania kusubiri kulishwa na wahisani kama Makinda ya ndege. Ni aibu kwa Rais wa taifa hili kuombaomba chakula. JK Nyerere alishawahi kusemea juu ya aibu ya kuombaomba chakula.Kwa bahati mbaya hatuweki mikakati ya kuachana na utegemezi hata wa chakula.

Tatizo linaloonekana kwa sasa ni kila suala kufanywa kishabiki bila kuzingatia madhara yake kwa taifa, wasaidizi wa Rais hawamsaidii lolote zaidi ya kuukwaza umma. Mfano aina ya mawaziri kama Waziri wa Elimu na Mafunzo Stadi Profesa Jumanne Maghembe inastua sana hii ni kutokana na aina ya utendaji na maamuzi anayochukua. Katika Mkutano wa 11 wa Bunge aliibua utata mara baada ya kutangaza kuwafutia udahili wanafunzi zaidi ya Mia tatu wa Chuo kikuu cha Dar-Es-salaam, waziri huyu alidiriki kusema kwamba wasidahiliwe katika chuo chochote hapa nchini na Bodi ya mikopo iwafutie mikopo. Nilisikitika sana na maamuzi ya Profesa wetu, maana alishindwa kujua kwamba Migogoro katika vyuo vya Elimu ya Juu kikiwemo chuo kikuu cha Dar-es-salaam inatokana na nini. Waziri hakujua kwamba wakuu wa vyuo na menajimenti za vyuo ndio shida, waziri kama msomi na mtu mwenye dhamana kubwa hakufanya utafiti kujua vyanzo vya migogoro. Waziri hakupima athari ya maamuzi aliyoyafikia ya kukatisha masomo kwa watoto wa watanzania duni waliokomboka kifikra, tumshukuru Dr.Slaa kwa kuwatetea wana wa wanyonge. Kwa bahati nzuri watawala walijigundua madhaifu yao na kuwarudisha wanafunzi hao kimya kimya. Huyu ndiye yuleyule aliyetangaza kwamba Stashahada ya Juu (Advanced diploma) inatambulika, lakini akasema isiendelee kutolewa tena na vyuo.

Kwa kifupi hii ni aina ya watawala tulionao kwa sasa, watawala wanaoweza kuamka asubuhi na kutoa maamuzi mazito kwa taifa bila kujali athari kwa umma. Lakini Chama cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuandaa watawala wasiokua na dira, kupitia umoja wake wa vijana (UVCCM) rejea tamko la Katibu mkuu wa umoja huo Francis Isaac Mtinga akijibu hoja za viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu hali ya mazungumzo ya muafaka eti "Profesa Ibrahim Lipumba ni Prefesa wa Mitishamba na Maalim Seif Shariff Hamad, ana akili ya kuku,kwa maana kwamba anasahau mapema". Kwa hoja mataputapu na matusi ya aina hii kweli chama cha Mapinduzi bado kina viongozi wa baadaye?

Taifa hili kwa sasa linaendeshwa kama vile halina wenyewe,mali za umma zimegawiwa kwa wageni, wazalendo waliolalia ngozi za wanyama kipindi cha kupigania uhuru bado wanaendelea kulalia ngozi hizohizo tena zilizochakaa zaidi ya kipindi kile. Huku mafisadi wakichota 'Vijisenti' na watawala wakiendelea kutuambia 'tuleteeni ushahidi tuwashughulikie' wananchi waliopiga vigelegele na kuvaa fulana, khanga, kofia za rangi za Kijani na manjano wakati wa uchaguzi wanaendelea kunywa maji machafu, kukosa madawa hospitalini, kujifungulia njiani huku watoto wao wakikalia mawe wengine wakikosa hata uwezo wa kusoma shule.

Baba wa Taifa hili JK alitutoka sasa leo hii tumebaki bila usimamizi wa kutosha, hakika hajapata wa kumrithi. Taifa aliloliasisi JK wananchi wake wanakulana wenyewe kwa wenyewe. Mafisadi wanakingiwa vifua, watawala wanataka ushahidi kwenye tuhuma za ufisadi kana kwamba wao ni mahakama. Hakika taifa lako Julius Kambarage (JK) linajiendea lenyewe.

Popote ulipo Mwasisi wa taifa letu la Tanzania (JK) tulioko huku hatuna amani tena Mabwanyenye wametukalia kooni, tumebomolewa nyumba zetu hapa Tabata Dampo mpaka sasa tunalala kwenye mahema kama wakimbizi ndani ya nchi yetu, utu wetu hauthaminiwi na watawala. Sisi Maalbino ndio kabisa tumejifungia ndani hatuwezi hata kutoka nje maana tukionekana sehemu yoyote tunauliwa na kukatwa viungo vya miili yetu, watawala uliotuachia hawatilii mkazo utatuliwaji wa tatizo hili. Kwakweli baba wa taifa ungekuwepo huku ungeona jinsi watawala tunavyojichotea 'Vijisenti', ungeona jinsi tunavyonunua magari ya kifahari. Hakika baba ungenipongeza kwa kuwa 'Mjasiriamali' nikiwa Ikulu. Hivi sasa Chama chetu hakihitaji mkulima wala mfanyakazi, wa nini? Sasa hivi ni zama za wafanyabiashara. Hatutaki usumbufu ndio maana kupitia serikali yetu tunaendelea kukata rufaa kupinga maamuzi ya mahakama kuu na ya rufaa ya kuruhusu mgombea huru asiye na chama. Tumeshafanya mengi, tukiruhusu vyama vingine au wagombea binafsi wachukue dola watatutia ndani!!

Taifa linajiendea lenyewe kwani ni nani mwenye uchungu nalo?.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: