Taifa lilihitaji spika, likapata Makinda


Jestina Katunda's picture

Na Jestina Katunda - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Spika Anna Makinda

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimelazimika kubadili mbinu za mapambano ili kumpata spika. Safari hii, imeonekana wazi kuwa CCM haikuangalia inamchagua nani, bali inamwondoa nani katika nafasi yake.

Baada ya kukamilisha azima hiyo ya kuondoa, badala ya kuchagua, ndipo ikaja na maelezo ya kuhalalisha uamuzi wake.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili, mwanamke akachaguliwa kurithi mikoba iliyokuwa ikishikiliwa na wanaume tangu tupate uhuru.

Bila kuonekana ninaongozwa na fikra za “mfumo dume,” – wakati mimi ni mwanamke, waliompitisha mwanamke wametumia njia hiyo kuendeleza ajenda maalum ya watuhumiwa wa ufisadi nchini.

Inawezekana mwenyewe hajui hilo, lakini hataamini kitakachotokea mbele ya macho yake.

Katiba ya nchi haijabadilika katika kueleza namna ya kuwapata viongozi wa mihimili mitatu ya dola – rais, jaji mkuu na spika.

Pamoja na mabadiliko makubwa ya kuboresha demokrasia ndani ya Bunge, uteuzi wowote unategemewa uzingatie uwezo, badala ya mambo kama jinsia, dini, eneo, itikadi, na hata umri.

Pamoja na kwamba vitu hivyo vinaweza kuwa vizuri, lakini vikitumiwa vibaya vinaweza kustawisha ubaguzi na pengine hata kunyima wenye sifa nafasi ya kuongoza.

Kibaya zaidi, wenye uwezo na ushawishi wa kifedha na nafasi katika jamii, wanaweza kuvitumia kutuchagulia watu, ambao mwisho wa siku, watatumika kwa manufaa ya wenye fedha badala ya kuwatumikia wananchi wote.

Hakuna anayesema Anna Makinda atashindwa kuongoza bunge, bali nafasi hizi za mihimili ya dola hazipaswi kupatikana kwa kutumia dhana ya “viti maalum” badala ya umahiri, weledi, uadilifu na uzalendo.

Kwa kuzingatia kuwa Watanzania wanaishi katika sura ya jinsia, dini, maeneo, itikadi na mambo mengine, basi katika uchaguzi wa wasaidizi wa mihimili hiyo mitatu, ndipo masuala haya yanaweza kuangaliwa ili kuleta uwiano.

Mathalani, ukiwa na rais mwanamme, si vibaya kuwa na makamu au waziri mkuu mwanamke. Ukiwa na spika mwanamme au mwanamke, basi naibu spika awe wa jinsia tofauti.

Jaji Mkuu akiwa mwanamme au mwanamke, jaji kiongozi apatikane wa jinsia nyingine ili mradi weledi na vigezo vingine vya taaluma hiyo vizingatiwe.

Lengo ni kutochanganya mambo katika kuchagua viongozi wa mihimili ya dola kama ilivyofanyika hivi karibuni huko Dodoma.

Baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika kwa madai ya mizengwe ya uchakachuaji, wananchi walitazamia kupata spika bila maelezo ya ziada ya kujazia upungufu unaoweza kuwa unaonekana katika haiba ya mtu aliyechaguliwa.

Kujaribu kutoa maelezo ya ziada ili aliyechaguliwa akubalike, ni kulazimisha kuficha udhaifu au hata hujuma inayoweza kuwa imetumika katika kumpata mteule huyo.

Nafasi ya spika ilipokuwa wazi, watu walikuwa huru kuigombea na vigezo vilikuwa vinafahamika kwa kila mmoja.

Hapakuwa na taarifa kutoka ofisi ya bunge iliyoeleza kuwa safari hii, wagombea wenye jinsia fulani watakuwa na sifa ya ziada.

Hata ndani ya vyama vya siasa, hakukuwapo taarifa kuwa nafasi ya spika itazingatia kigezo kipya cha jinsia. Wanachama wa jinsia zote walihamasishwa kuchukua fomu.

Kwa CCM, ambacho ni chama chenye uwezo wa kumpitisha mgombea yeyote kutokana na wingi wa wabunge wake, hatukusikia pia msisitizo au dokezo la sifa ya ziada kwa wagombea wa jinsia fulani.

Naamini kwa dhati pia, kuwa vyama vyote vilikuwa na lengo la kuhakikisha anapatikana spika mwenye uwezo, mwanamke au mwanamme – lakini spika asiyehitaji maelezo ya ziada ili kukamilisha sifa zake.

Kwa hali hiyo, kitendo cha CCM kuibuka na sifa ya ziada ndani ya Kamati Kuu (CC), kiliibua hisia za ziada na zinahitaji maelezo ya ziada kuzikubali.

Hata kama CCM iliamua kuwa sifa ya jinsia itumike, bado kingeweza kuleta majina ya wanawake na wanaume na bado kikaweza kupata mwanamke, hata kama mwanamke huyo angepata kura chache ndani ya kamati ya wabunge wake.

Si mara ya kwanza kufanya hivyo. Wamefanya hivyo hata katika michakato mingine, kwamba wamekuwa wakichukuliwa wagombea wenye kura ndogo na bado wakashinda katika chaguzi zinazoshirikisha vyama vingine.

Katika hili, wangeweza kufanya hivyo ili kuepusha fikra zinazozagaa sasa kuwa lengo la CCM katika nafasi hii, lilikuwa ni kumuondoa Sitta, na si kuchagua spika mwenye uwezo, hadhi na sifa ya kuongoza bunge.

Kama lengo lilikuwa ni kuchagua mtu, bado spika aliyeondolewa angeambiwa asichukue fomu au aondoe jina lake kama ilivyofanyika kwa nafasi ya naibu spika.

Lakini kwa kuwa hapakuwa na nia njema, makosa makubwa yalifanyika na kuacha majeraha yanayoweza kukigharimu chama siku za usoni.

Kwa nini basi inaonekana umakini ulipungua sana katika mchakato wa kumpata spika? Wapo wanaodai mtendaji mkuu wa chama, Yusuf Makamba ni chanzo cha kukosa umakini.

Amekuwa anapokea maelekezo kutoka kwa wakubwa wawili na kushindwa kuyaunganisha kwa umakini unaotakiwa.

Mmoja ni mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete; mwingine ni Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu.

Ingawa maelekezo yao yana lengo linalofanana, lakini inabidi yatekelezwe kwa njia tofauti.

Wakati Kikwete angependa ajenda ya kumtosa Sitta ifanyike kwa umakini usioacha ushahidi wa mchezo mchafu, Lowassa anadaiwa kutaka Sitta aondoke “kwa vyovyote vile.”

Mkakati wa kumtupa Sitta kwa kumchagua Makinda, hauna maana ya kuwainua akina mama, kwa sababu kimsingi akinamama hawahitaji hisani ya aina hiyo.

Wanahitaji kuongoza bila kupokea maelezo yenye harufu ya kifisadi na yenye lengo la kuzima ajenda ya msingi ambayo inatumika kuwakandamiza. Humo ndimo kuna heshima yao.

Sasa dalili za awali zimeanza kuonekana kuwa akina mama watatumika kuzima ajenda za ufisadi kwa sababu tayari spika mpya amesema hajui “ufisadi” unaokamua raslimali za nchi ni kitu gani.

Huyo ni Anna Makinda tofauti na yule tuliyemzoea akiwa naibu spika wa Samweli Sitta.

Jambo moja ni muhimu. Kwamba Makinda anatakiwa kufahamu kuwa wakandamizaji wake wa juzi hawawezi kuwa wakombozi wake wa leo. Afahamu kuwa wananchi walihitaji spika, hawakuhitaji mwanamke.

Kwani bungeni, wawakilishi hawaendi kuoa au kuolewa. Wanakwenda kufanya uwakilishi, kutunga sheria na kushauri na kusimamia serikali. Haya hayaendi kwa misingi ya upendeleo kijinsia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: