Taifa linayumba


editor's picture

Na editor - Imechapwa 08 July 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

RAIS Jakaya Kikwete ni kiongozi wa taifa na amiri jeshi mkuu mwenye jukumu la kuwa msimamizi wa ulinzi wa jamhuri na amani ya wananchi katika jamhuri nzima.

Kama kiongozi wa Taifa, rais anatarajiwa kuwa makini kwa asilimia zote 100 na hata kuzidi. Anapaswa kuonyesha njia pale walio chini yake wanapopotea.

Kama kiongozi wa Taifa, rais anatakiwa, tena ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri aliyoapa kuitekeleza, kuilinda na kuitetea, adhibiti dalili za kupeleka taifa mrama.

Rais pia anatakiwa kuhakikisha serikali yake inaendeshwa kwa misingi ya utawala bora; utawala unaozingatia taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba.

Tunaamini haya yote si mageni kwa Rais Kikwete; anayatambua na kuyafahamu vilivyo. Kinachoonekana kama ni tatizo kwa sasa, ni kuwepo udhaifu katika kutekeleza jukumu hili.

Tunaona kasoro katika kurekebisha makosa yaliyotendwa na wateule wake kwenye wizara, idara na taasisi za serikali anayoiongoza kwa niaba ya wananchi.

Taifa linayumba kwa sababu kiongozi mkuu ni mzito wa kufanya maamuzi thabiti na kwa wakati unaofaa. Ile kaulimbiu ya 'ari, nguvu na kasi mpya' aliyoiakisi alipoomba ridhaa na hata baada ya kuchaguliwa, haionekani katika kufanya maamuzi panapotokea matatizo mazito.

Uongozi wa Tanzania umeguswa mno katika siku za hivi karibuni na hii ni indiketa ya wazi kwamba kuna mahali wajibu hautekelezwi sawasawa. Hii haionyeshi kudra njema.

Taifa linakabiliwa na kashfa za kifisadi zilizochangia kuhujumu uchumi na raslimali za nchi. Wapo viongozi wa kisiasa na wataalamu serikalini (kwa maana ya wizara, idara na taasisi za kiserikali) wanatuhumiwa kwa ufisadi na uzembe lakini wanalindwa.

Baadhi yao wanahusika na kashfa ya EPA, wengine ya mkataba wa kifisadi wa Richmond, kwa kutaja machache tu; wapo walaji rushwa wakubwa kwenye Mahakama wanalindwa; wapo mafundi wa ufisadi na uhalifu katika Jeshi la Polisi wanalindwa.

Lipo tatizo la kukwama kwa ahadi yake ya kutafutia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar. Vyama vimeshindwa na kilichobaki tunaona ni yeye kama kiongozi wa Taifa kuchukua nafasi yake kumaliza mkwamo. Anapiga siasa tu na ahadi zisizo matokeo zaidi ya kupoteza muda.

Tunaotazama maslahi ya Taifa badala ya itikadi za vyama, tunaona ukimya wa kupindukia alionao Rais Kikwete, unazidisha hatari ya alichokiita 'mpasuko' kukua na kusambaratisha taifa.

Haya ni mambo mazito yaliyohitaji maamuzi makini. Kudhibiti ufisadi na kukomesha uzembe na rushwa serikalini si mambo yanayofanikiwa kwa kutoa ahadi tu, bali vitendo vinavyoonekana matunda yake.

Tunahofu kwamba pana ukosefu wa uongozi wa kutenda katika namna ambayo matokeo ya kutenda huko, ni kujenga imani wananchi juu ya serikali yao na kiongozi wao.

Rais Kikwete hajachelewa sana iwapo tu ataona umuhimu wa kuchukua jukumu lake la kikatiba la kushughulikia masuala haya yanayohitaji mkono na kauli yake. Panahitajika matendo bayana.

Tunatoa indhari kwamba lazima tufike mahali, Rais achangamke kwa kauli na matendo yanayoelekeza dola kurudi katika mstari. Vinginevyo, tunaonya, madhara ya ukimya na uzito wa kimaamuzi, yanaweza kuwa makubwa si muda mrefu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: