Taifa Stars bado ina safari ndefu


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 13 June 2012

Printer-friendly version

TANZANIA imeanza kuona mwanga katika mbio za kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil, baada ya Jumapili iliyopita kuifunga Gambia 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa timu hiyo maarufu kama Taifa Stars, chini ya Kim Poulsen.

Katika mchezo wa kwanza wa Kundi C, Taifa Stars ilifungwa mabao 2-0 na Ivory Coast, huku Gambia ikitoka sare ya bao 1-1 na Morocco. Pia juzi, Morocco ilitoka sare ya 2-2 na Ivory Coast.

Kwa matokeo ya mechi hizi mbili, Taifa Stars inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu na mabao mawili nyuma ya vinara Ivory Coast wenye pointi nne na mabao manne huku Moroco yenye pointi mbili na mabao matatu inashika nafasi ya tatu na Gambia ya nne ikiwa na pointi moja.

Poulsen raia wa Denmark ameingia na falsafa ya kujaza wachezaji vijana kikosini ili wapate uzoefu kutoka kwa wakongwe na kulisaidia taifa baadaye.

Wachezaji chipukizi kama Shomari Kapombe, Frank Domayo, Salum Aboubakar ‘Sure Boy’, Mbwana Samatta, Gerald Jonas hata Mwinyi Kazimoto waliopo katika kikosi hicho kuna hakika wataonyesha tofauti kubwa.

Katika mechi mbili za Taifa Stars hapa nchini ikiwemo ya kirafiki dhidi ya Malawi chini ya Poulsen, tumeona kikosi kikicheza kwa uelewano huku njia za kutafuta mabao zikionekana muda mwingi, tofauti na awali timu ilitegemea mashambulizi ya kushtukiza.

Katika sehemu ya kiungo, Domayo na Sure Boy ndio wanatumiwa na Poulsen kila mara na hakika wanaonekana kuelewana na hata katika mchezo dhidi ya Gambia, ndio waliobeba timu. Hakuna ubishi.

Viungo hao waliweza kutibua mipira ya adui huku wakitoa pasi zenye macho kwa washambuliaji, na hata wanapoharibu mipira hujipanga haraka na kuzuia hatari langoni kwao.

Awali, walionekana kukosa uzoefu wa mechi za kimataifa lakini baada ya mechi mbili dhidi ya Malawi na Ivory Coast, na ukichanganya mechi walizokuwa wakicheza katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 (U-20), kiasi chake wamepiga hatua.

Chipukizi hao walionekana kutulia katika sehemu kubwa ya mchezo huo, kiasi cha kutishia nafasi ya wakongwe kama Shaaban Nditi na Nurdin Bakar katika nafasi hizo. Hata hivyo, nguvu na pumzi bado ni tatizo kwa chipukizi hawa.

Katika mchezo dhidi ya Gambia ambayo inashika nafasi ya 108 kwa ubora wa soka duniani ikilinganishwa na Tanzania nafasi ya 139, Taifa Stars ilionekana kuwa na tatizo lile lile la kuruhusu kufungwa bao la haraka ndani ya dakika 10 za kwanza.

Kwa miaka minne hadi mitano sasa, Taifa Stars imekuwa na tabia ya kutojipanga vizuri katika safu yake ya ulinzi kiasi cha kuruhusu kufungwa dakika za mwanzo, mabeki wake wanashindwa kushusha presha ya timu pinzani na kujichanganya katika kuokoa.

Bao walilopata Gambia dakika ya saba lilikuwa zuri, kwani mshambuliaji Momodou Ceesay alitumia vyema kosa la beki wa kati Kapombe, ambaye aliduwaa kuokoa mpira wa juu uliopigwa kutoka pembeni. Kwa kutumia urefu wake, Momodou alifunga kirahisi.

Mara nyingi Poulsen anakataza wachezaji wake kuchezea mpira muda mwingi bila ya malengo; mshambuliaji Mbwana Samatta naye ameingia katika mkumbo huo ambao awali ulizoeleka kufanywa na Mrisho Ngassa.

Kuna wakati Samatta alijisahau na kumiliki mpira kwa muda mrefu huku akipiga chenga kuelekea pembeni ya uwanja hadi alipofanyiwa madhambi na wachezaji wa Gambia.

Poulsen na kocha mwingine yeyote anayehitaji ushindi, hawezi kuruhusu uchezaji huo kwani unaweza kuchelewesha au kuhatarisha ushindi wa timu na hata afya ya mchezaji.

Endapo kikosi cha Taifa Stars kilichoivaa Gambia kitaweza kubaki katika kiwango chake, kinaweza kufika mbali japokuwa wachezaji wake wengi hawana msingi wa soka.

Mchezaji kama Samatta bado anahitaji kucheza kwa uzalendo zaidi na hana haja ya kujithibitisha kwa mashabiki kwa kucheza huku akisubiri kelele za kumshangilia. Anaigharimu timu kwa vitu visivyo na msingi wakati mwingine.

Beki wa kushoto Amir Maftah anahitaji kupewa darasa la ‘marking’ kwani mara nyingi upande wake huwa ‘njia kuu’ ya kuanzisha na kuratibu mashambulizi yote yanayoelekea lango la Taifa Stars. Hata bao la Gambia lilipitia upande wake.

Maftah ana tatizo la kutocheza mpira asipokuwa nao, hilo ni tatizo anapaswa kubadilika haraka. Tabia hii ya Maftah anayo hata akicheza katika kikosi cha Simba, na hata huko mashambulizi kupitia upande wake huwa mengi.

Hata hivyo, Maftah ana uwezo mkubwa wa kupandisha timu wakati inashambulia, pia ni mpigaji mzuri wa krosi zenye matumaini.

Marekebisho yanaweza kufanyika katika kikosi cha Taifa Stars lakini kwa kuzingatia matatizo yaliyopo ili kuweza kutoa changamoto kwa timu nyingine za Kundi C na kuwa katika nafasi nzuri ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2014.

Huu ni mwanzo mzuri wa udhamini wa miaka mitano wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wenye thamani ya Sh. 23 bilioni kwa Stars.

0
No votes yet