Taifa Stars tafuna sasa Les Fauves


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version

KATIKA miezi ya kuelekea kumenyana na timu ya soka ya Jamhuri ya Afrika Kati maarufu kama Les Fauves yaani wanyama wakali, Taifa Stars ilicheza mechi kadhaa za kirafiki za kimataifa na kupata matokeo mchanganyiko.

Desemba 12, 2010, Kilimanjaro Stars inayoundwa na wachezaji wa bara pekee ilitwaa ubingwa wa michuano ya Afrika Mashariki na Kati kwa kuilaza Cote d’Ivoire bao 1-0 katika fainali.

Ushindi huo ulisababisha Taifa Stars kulalia mlango wazi bahati ya Kili Stars ikakubali haraka mwaliko wa kushiriki mashindano mapya ya Kombe la Mto Nile yaliyoandaliwa na Misri.

Taifa Stars iligalagazwa kwa mabao 5-1 na Misri katika mchezo wa kwanza uliofanyika Januari 5, 2011 halafu ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Burundi, na ikapata sare ya 1-1 na Uganda kabla ya kupigwa mabao 2-0 na Sudan.

Matokeo hayo si ya kujivunia inapoelekea kukutana na timu isiyotabirika ya Les Fauves mwishoni mwa wiki hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mathalani wakati Stars ilianza kwa sare ya bao 1-1 na Algeria katika mechi ya kwanza kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa mwaka 2012, Les Fauves ilianza kwa suluhu na Morocco.

Les Fauves ilizinduka mechi ya pili na kuilaza Algeria mabao 2-0 jijini Bangui, Taifa Stars ilikula kichapo cha bao 1-0 kutoka Morocco kwenye Uwanja wa Taifa.

Ushindi dhidi ya Algeria, ambao ni wa kwanza mkubwa katika miaka ya hivi karibuni, ni kielelezo kwamba Les Fauves imebadilika sasa ina uwezo wa kuvishinda hata vigogo vya soka barani Afrika.

Hata hivyo, rekodi zilizopo zinaonyesha Les Fauves haina rekodi ya kushiriki kwa mafanikio michuano mikubwa; ama imekuwa ikijitoa au kutojisajili. Mwaka 1978 ilijitoa kushiriki michuano ya Kombe la Dunia, mwaka 1982 ilifukuzwa, wakati mwaka 2002 haikufuzu; miaka mingine yote haikushiriki.

Katika Kombe la Mataifa ya Afrika ilijitoa fainali za 2006, haikujisajili fainali ya 2008 na ilijiondoa fainali za 2010.

Hata mechi za kirafiki ilizoshiriki haijawa na matokeo mazuri. Machi 12, 2007 ilichapwa mabao 4-1 na Congo; siku nne baadaye ilifungwa bao 1-0 na Chad halafu Novemba 21, 2007 ililazimisha sare ya 1-1 na Guinea ya Ikweta.

Lakini timu ambayo imekuwa na matokeo mabovu kama hayo, ilishangaza ilipozivimbia timu kubwa na hata kuichapa Algeria na kushika nafasi ya kwanza katika msimamo ikiwa na pointi 4 sawa na Morocco iliyoko nafasi ya pili huku Stars na Algeria zikipigana vikumbo nafasi ya tatu na nne.

Wakati Algeria itakuwa nyumbani kuisubiri Morocco katika mechi ya tatu, Stars inapaswa kupania ushindi ili kufufua matumaini ya kucheza fainali hizo zilizopangwa kufanyika Ikweta ya Guinea na Gabon mwakani. Stars ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1980.

Kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan Borge Poulsen kutoka Denmark amekaririwa na vyombo vya habari akisema hataki kuingiliwa kupanga kikosi. Mwishoni mwa wiki amesikika akisema kwamba kazi yake si kufundisha wachezaji kutoa pasi, kumiliki mpira, kufunga, kukaba na kufungua nafasi.

Kazi yake, amesema ni kuunganisha idara zote kucheza katika mfumo utakaowezesha kupata ushindi. Sawa.

Kwa kuwa amegundua kwamba wachezaji wanakosa mafunzo muhimu ya awali ya namna ya kucheza soka bora, kwa kuwa anajua mapungufu yaliyopo, na kwa kuwa kasoro hazijaanza leo, wadau wa soka wanasubiri mageuzi.

Makocha wenyeji watakaa kusubiri msaada anaohitaji, na TFF (shirikisho la soka Tanzania) watampa kila aina ya ushirikiano huku mashabiki wakitoa mchango wao katika kushangilia.

Jambo moja kubwa ambalo Poulsen anapaswa kulijua ni kwamba Watanzania wanataka ushindi akianza na Les Fauves ambao kama silka ya wanyama hawakawii kuishiwa pumzi.

Wadau wa soka wana kiu ya ushindi katika mechi za kufuzu siyo za kirafiki kama ilivyokuwa dhidi ya Palestina.

Msafara wa Les Fauves una:

Makipa Prince Samola, Geoffrey Lembet na Emmanuel Yezzouat.

Mabeki ni Salif Keita, Manasse Enza, Fernander Kassai, Audin Boutou, Delphin Gbazinon, Franklin Anzite.

Viungo ni Mamadi Saoudi, Euloges Enza, David Manga, Eudes Dagoulou, Amores Dertin, Freddy Lignanzi, Vianney Mabide, Onassis Kemo.

Washambuliaji ni Habib Habibou, Hilaire Momi, Josue Balamandji, Foxi Kette-Vouama, Charlie Dopekoulouyen, na Kocha mkuu ni Jules Accorsi.

Msafara uliokuja ni wa wachezaji na viongozi 32 ukiongozwa na Waziri wa Michezo, Aurelien Zingas.

Ubora: CAR iko nafasi ya 114 wakati Stars ni ya 121.

Vipigo: CAR ilipigwa 7-1 na Cameroon, Stars 5-1 na Misri.

Wafungaji hatari: CAR ni Charlie Dopekoulouyen  wa Raja Casablanca na kiungo Hilaire Momi.

0
No votes yet