Tajiri anayeunda chama cha wafanyakazi


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 02 September 2008

Printer-friendly version
WAZIRI wa Kazi,  Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya

WAZIRI wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya amenukuliwa akiwaambia waajiri nchini kufanya kitu ambacho siyo cha kawaida.

“Serikali inawaagiza waajiri kuanzisha vyama vya wafanyakazi, lakini pia kushirikiana navyo kama sehemu ya kuleta maendeleo mahali pa kazi badala ya chuki,” amenukuliwa akisema na kwa wiki moja sasa hajakana kusema hivyo.

Kapuya alikuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Waajiri nchini (ATE) jijini Dar es Salaam. Je, kile ambacho waziri ananukuliwa kuagiza kinawezekana? Kina mantiki? Ni sahihi?

Niliwasiliana kwa simu na baadhi ya wananchi kuhusu suala hilo. Yafuatayo ni mawazo ya baadhi yao.

Tusubiri tuone lakini zaidi itategemea viongozi wa vyama hivi watakaoteuliwa; wao ndio waamue kumbana tajiri au kujiunga naye: 0754-627592.

Hapa kuna mambo mengi. Kwanza, mwenendo wa sasa wa vyama unafanya wafanyakazi wapoteze hamu na imani katika vyama vyao. Vimetekwa.

Pili, Mabwana/Mabibi Leba hawafanyi kazi yao ya kuamsha wafanyakazi kuona umuhimu wa vyama vyao. Tatu, wanaoitwa wawekezaji hawaoni umuhimu wa vyama hivyo na hawavihitaji. Wanaona vitawasumbua.

Nne, kwa wawekezaji hao, mfanyakazi siyo tena kipengele muhimu kijamii, kiuchumi wala kisiasa. Anachukuliwa kama bidhaa nyingine: 0754-550254.

Chama cha wafanyakazi kinaundwa na wafanyakazi wenyewe kwa maslahi yao. Waajiri nao wana chama chao kinacholinda maslahi yao. Maslahi ya wafanyakazi hayawezi kulindwa na waajiri wala ya waajiri kulindwa na wafanyakazi: 0754-324286.

Mwajiri? Amekuwa mtu wa kutilia mashaka wakati wote. Si mtu mzuri wa kuanzisha chama cha wafanyakazi: 0713-252337.

Naona vyama vitakuwa vya tajiri na viongozi wa wafanyakazi watakuwa mawakala wa matajiri: 0755-804526.

Kuna haja ya kulipinga wazo hili lililokosa mashiko na lenye mtazamo mufilisi; ni wazo lenye nia ya kuidhoofisha kabisa, kama si kuinyonga demokrasia: 0713-690637.

Mimi naona vyama hivyo vitakuwa kwa manufaa ya mwajiri maana vimeundwa na mwajiri. Vinastahili kuundwa na mfanyakazi mwenyewe kwa manufaa yake: 0712-419902.

Matajiri wanaweza kuunda kweli kwa ajili yetu sisi wapagazi wao. Lakini na hawa watu (bila shaka wanasiasa), huwa wanazungumza tu bila kujua athari za yale wayasemayo: 0755-312859.

Sikumsikia Kapuya anaongea lakini ni jambo la kushangaza kwa nini wafanyakazi wasiunde wenyewe vyama vyao. Basi chama cha aina hiyo kitakuwa cha waajiri: 0717-124979.

Mwajiri ana nafasi ya kazi. Mfanyakazi anatafuta nafasi ya kazi. Mwajiri anahitaji mwenye elimu, ujuzi, uzoefu na nguvu ya mwili na akili. Mfanyakazi anasema anavyo.

Watu hawa wawili, kila mmoja ana mahitaji yake. Tajiri anataka kazi yake ifanywe na mfanyakazi anataka elimu yake, ujuzi, uzoefu na hata nguvu ya mwili viajiriwe. Wanaingia kwenye mapatano ya mshahara na tabia, mwenendo na hata sheria za mazingira husika.

Kama kuna vyama basi kila mmoja aunde chake ili kutetea na kulinda maslahi yake; lakini hakuna hata mmoja awezaye kuunda chama kwa maslahi ya mwenzake: 0782-397252.

Maslahi ya mwajiri na mwajiriwa yanabadilika kila kukicha na katikati huota mivutano ambayo haiwezi kuondolewa kwa kuwa na chama cha wafanyakazi kilichoanzishwa na waajiri.

Sharti kuwepo vyama viwili. Kimoja cha waajiri na kingine cha waajiriwa. Mashauriano kati ya vyama hivyo ndiyo yaweza kusukuma mbele maendeleo: Private No.

Sijaamini kama anaweza kusema hivyo. Lakini kama amesema, basi atakuwa alikuwa “likizo” kwa muda mrefu: 0754-384850.

Aa bwana! Tumefika mbali…kwa mwendo wa kasi mpya! Suala ni tunaenda mbele au tunarudi nyuma? 0754-475372.

Hivyo vitakuwa siyo vyama vyenye kukidhi haja ya wafanyakazi: 0762-594494. Vyama vya waajiri? Wewe nani? 0756-771455.

Hii ni mara kwanza waajiri kupewa jukumu kama hilo. Tanazania imeweka rekodi ya kuwa na fikra pogo. Vyama vya kweli haviandikishwi. Vinawekewa pingamizi. Mimi hilo nina ushahidi wake: 0784-352552.

Baadhi ya viongozi wa wafanyakazi wanakatisha tamaa. Wengi hawajui hata jukumu la vyama vyao. Wanashikilia nafasi hizo kwa kutafuta umashuhuri tu lakini siyo kwa kujua majukumu yao. Hawa wanatumiwa na waajiri na wanasiasa.

Nakumbuka kuhudhuria kikao cha wafanyakazi, mara baada ya uchaguzi mkuu, ambako walikubaliana kutoa tamko na kuandamana eti kupongeza serikali kwa “kufanikisha uchaguzi huru na wa haki. Niliwashangaa. Hii si kazi ya vyama vya wafanyakazi.

Ukiishakuwa na vyama vya aina hii, watawala na waajiri wanafurahi na wanaweza pia kupongezana na kuhimizana kuanzisha vyama vya wafanyakazi. Ni hatari: 0782-397252

Kila mtu ana mawazo yake. Lakini kwa ufupi, tajiri siyo tu hapaswi, bali pia hastahili kuanzisha au kushiriki kuanzisha chama cha wafanyakazi.

0
No votes yet