Takwimu hizi za Rais Kikwete zimepikwa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MOJA ya matatizo makubwa serikalini ambayo Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliwahi kubaini ni ukadiriaji wa takwimu.
Mkapa aliwahi kusema alipelekewa pendekezo la kutoa chakula cha msaada kiasi cha tani 600 lakini aliidhinisha tani 60 na kikatosheleza wote waliokuwa wanakabiliwa na ukosefu wa chakula.

Tatizo hilo halijaisha, limerithiwa na Serikali ya Awamu ya Nne na Rais Jakaya Kikwete na viongozi wakuu serikalini wanabadilisha takwimu kama magoli ya mpira wa chandimu kila uchao.

Ilani iliyoandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ilionyesha kwamba uchumi wa Tanzania ulikuwa umekua kutoka asilimia 4.5 mwaka 1995 hadi asilimia 6.7 mwaka 2005.

Hii ni ilani iliyotumiwa na viongozi waliomnadi Jakaya Kikwete.

Kikwete, baada ya kuingia ikulu mwaka 2005 alisema matarajio ni kuweka mikakati kuhakikisha uchumi unakua hadi kufikia asilimia 10 mwaka 2010.

Mwaka huu viongozi haohao wa CCM wakakutana wakachakachua ilani ya mwaka 2005 wakabadili lugha kwa matumizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Ilani ya CCM iliyotumika kumwingiza tena madarakani Kikwete, katika kipengele cha Mafanikio ya Kiuchumi, inaonyesha katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya serikali yake uchumi umekua kutoka asilimia 4.5 hadi 6.7.

“Katika kipindi hiki Serikali imeweza kutekeleza mipango yake kwa ufanisi mkubwa na kuleta mafanikio ya kiuchumi yafuatayo--(a) Ukuaji wa uchumi ulifikia wastani wa asilimia 6.7 mwaka 2010 ukilinganishwa na wastani wa 4.5 mwaka 2005,” inasema ibara ya 13 ya Ilani ya CCM.

Nyaraka za Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinaonyesha kwamba kiwango cha ukuaji wa uchumi cha asilimia 6.7 kilifikiwa mwaka 2005.

Kwa hiyo, ilani ya CCM mwaka huu ilipaswa kuonyesha kufanikiwa au kushindwa kukuza uchumi kutoka asilimia 6.7.

Ripoti ya WB ya mwaka 2007 kuhusu biashara na uchumi nchini ilisema, “…uchumi wa Tanzania unakua kwa wastani wa asilimia tano hadi sita katika kipindi cha miaka 10 kutoka 1995 hadi 2007.”

Katika hotuba yake, aliyekuwa waziri wa biashara na viwanda, Basil Mramba katika Bunge la Bajeti mwaka 2005, alisema, “uchumi wa taifa umekua kwa asilimia 6.7”.

Sasa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hali ilikuwa ngumu katika kujenga uchumi wa nchi na kupunguza umaskini. 

  • Hicho ndiyo kipindi ambacho dunia ilikumbwa na misukosuko ya kiuchumi. Ilielezwa msukosuko huo uliozikumba nchi za Ulaya na Marekani usingefika Afrika na hasa Tanzania, lakini baadaye serikali ilirekebisha kauli ikasema msukosuko huo umeathiri uchumi.
  • Hicho ni kipindi ukazuka ukame uliokausha mazao ya chakula na kusababisha njaa maeneo mengi nchini. Serikali ilifanya mipango ya kununua na kugawa chakula kwa watu wapatao milioni nne.
  • Ukame huo ndio ulizusha balaa. Ulipokosekana umeme kutokana na mabwawa kukauka na hivyo mitambo kushindwa kuzalisha umeme, ikaibuliwa mipango ya kupata umeme wa dharura, mipango iliyosababisha kuibuka kashfa ya Richmond.
  • Mbali ya kudorora kwa uchumi duniani, njaa na kukosekana umeme, bei ya mafuta ilipanda kwa kiwango kikubwa na kusababisha gharama za usafiri na usafirishaji kupanda. Mitambo iliyokuwa inategemea mafuta kwa ajili ya kuzalisha umeme viwandani ikawa inafanya kazi chini ya uwezo.
  • Katika kipindi hicho shughuli za uwekezaji na uzalishaji na utalii zilidorora; mfumko wa bei ukatokea, uuzaji mazao nje ukapungua, mapato ya ndani yakashuka na kuathiri ukuaji wa kiuchumi.

Lakini Ilani ya CCM ya mwaka 2010 inaonyesha matatizo hayo ni ya kwenye makaratasi uchumi umekua kwa digiti 2.2 yaani kutoka asilimia 4.5 hadi 6.7.

Mshangao, katika taarifa ya Mwelekeo wa Uchumi kwa mwaka 2009/2013, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mukulo alisema pato halisi la taifa linakadiriwa kukua kwa asilimia 7 katika mwaka 2010.

Mkulo alisema kuwa katika mwaka 2011, pato halisi la uchumi litakuwa kwa asilimia 7.1, mwaka 2012 asilimia 7.4 na hadi kufikia mwaka 2013 pato halisi la taifa litafikia asilimia 7.8.

Lakini Septemba mwaka huu, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof, Beno Ndullu alisema licha ya mtikisiko wa kiuchumi duniani, kupanda bei ya mafuta na chakula, bado uchumi wa Tanzania umekua kufikia asilimia saba kutoka asilimia 6.5.

Halafu Alhamisi iliyopita Kikwete akachanganya zaidi kwa kutoa takwimu mpya akisema umepanda kwa asilimia 7.1 wala siyo asilimia 7 kama alivyokadiria Mkullo na si asilimia 6.7 kama ilivyosema Ilani ya CCM.

“Tulilazimika kufanya kazi ya ziada kuzuia uchumi wetu usiporomoke na nafurahi kwamba juhudi zetu zilifanikiwa…,” alisema Kikwete.

Kuhusu sekta ya utalii, Ilani ya CCM inasema  kutokana na juhudi hizo idadi ya watalii wa ndani iliongezeka kutoka wastani wa 436,000 mwaka 2005/2006 hadi 639,000 mwaka 2008/2009. Wakati huo huo idadi ya watalii waliotembelea Tanzania kutoka nchi za Asia iliongezeka kutoka 23,542 mwaka 2006 hadi watalii 26,070 mwaka 2009.

Katika masoko ya zamani, idadi ya watalii iliongezeka kutoka 612,754 mwaka 2005 hadi watalii 770,376 mwaka 2008. Sekta ya utalii katika kipindi hicho iliingizia Taifa jumla ya dola za Marekani 2.8 bilioni.

Katika hotuba yake bungeni Kikwete alisema utalii ni sekta inayoongoza katika kuliingizia taifa fedha za kigeni. “Kwa mfano, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2005-2009) sekta hii iliingiza jumla ya dola za Kimarekani 4,987.5 milioni.

Maswali

Kwa nini takwimu za ukuaji uchumi zinatofautiana? Uchumi umepanda lini hadi kufikia asilimia 7.1 maana hadi kampeni zinaanza ulikuwa asilimia 6.7? Nani aaminiwe Ilani ya uchaguzi, Mkullo au Rais?

Kama kuna mabadiliko, nani aliyefanya tathmini hii mpya tangu Agosti 2010 hadi Oktoba 2010 inayobadili mwelekeo wa uchumi? Kwa nini watu wasiamini kuwa takwimu hizi zimepikwa? Na kwa manufaa ya nani?

Pengine hii ndiyo sababu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipoombwa kutoa shukrani kwa hotuba ya Kikwete alisikitikia umaskini mkubwa wa watu tofauti na majisifu kwamba uchumi umekua.

Miezi mitatu wanapika uchumi umekua kwa asilimia 7 (Mkullo); 6.7 (Ilani); 7.0 (Ndullu) na 7.1 (Kikwete).

Ndiyo maana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikaona itumie fursa hiyo vema. Iliona watu 12 milioni walikuwa wamejiandikisha kupiga kura.

Namba zikamchanganya mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu akadhani ni 21 milioni, lakini mwenyekiti Lewis Makame alifinya macho akadhani kuna sifuri mahali akasema watu 20.1milioni walikuwa wamejiandikisha. Hesabu zikapikwa, matokeo yakapikwa na mshindi akapikwa nay eye anapika hali ya uchumi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: