Takwimu za NEC si sahihi


Dk. Noordin Jella's picture

Na Dk. Noordin Jella - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kiravu

TAKWIMU za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu idadi ya wapigakura, si sahihi na zinauweka uchaguzi wa mwaka huu katika mazingira magumu kuliko chaguzi zingine zote zilizopita.

Kutokana na takwimu zinazochapishwa na majarida ya kimataifa (Demographic segments) juu ya Tanzania, Afrika na nchi zinazoendelea duniani zinaonyesha watu wenye umri kati ya siku moja hadi chini ya miaka kumi na nane wapo kati ya asilimia 65 hadi 70.

Wenye umri wa kuanzia miaka kumi na nane na kuendelea ni kati ya asilimia 30 hadi 35.

Katika nchi za dunia ya tatu haijapata kutokea idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura ikazidi robo (asilimia 25) ya idadi ya wananchi katika nchi husika.

Lakini Tanzania yenye sifa zote ya kuwa katika kundi la nchi za dunia ya tatu, idadi ya waliojiandikisha ni karibu asilimia 55 ya wananchi wake.

Kulingana na wataalamu wa takwimu za wananchi wa nchi hizi za dunia ya tatu ni kwamba, takwimu za wananchi wa nchi hizi zina mfano wa umbo la “Pyramid” yaani watu wenye umri mdogo ndio walio wengi kwenye jamii na jinsi umri unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo idadi ya watu inavyopungua.

Nchi hizi za dunia ya tatu zinakuwa na tabia hii ya “Pyramid Demographic” kwa vile watu wa nchi hizi wana tabia za kuzaa watoto wengi, kuoa wanawake wengi, na watoto wengi ambao wanazaliwa nje ya ndoa.

Inafahamika pia kwamba idadi ya watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 18 ni ndogo kuliko ile ya watoto. Ni kwa sababu, taifa hili na mengine yaliyopo katika dunia ya tatu, yanakabiliwa na umaskini mkubwa.

Hali ya maisha ni ngumu, magonjwa ni mengi ambayo yanasababisha vifo vingi kwa wingi na umri wa kuishi mdogo kutokana na lishe mbovu na kazi ngumu.

Katika nchi zilizoendelea (First world or Developed Countries) wao idadi ya watu ina umbo la Cone au kwa kishahili ina umbo la “PIA” ile ambayo watoto wadogo huichezea.

Cone Demographic kwa vile wao wanaoa mwanamke mmoja, na wanazaa mtoto mmoja au wawili tu, na ya watu wazima –wenye umri zaidi ya miaka 18, hawaoi au hawaolewi kabisa.

Kuna idadi kubwa ya watu ambao hawapendi kuwa na watoto, na hata kama wataolewa au wataoa, lakini hawataki kuzaa.

Kwa mantiki hii, idadi ya wapiga kura kwenye nchi hizi hufika nusu ya wananchi wake na wakati mwingine hata huzidi nusu ya idadi ya raia wote wa nchi husika.

Kimsingi kwa taifa hili ambalo limekuwa Mwenyekiti wa kudumu wa nchi maskini duniani, na Katibu Mkuu wa kudumu wa nchi zinazoendelea duniani haiwezi kuwa na tabia ya idadi ya watu wa cone yaani “Characteristics of Cone Demographic!” Haiwezekani.

Kwa hapa nasema Jaji Lewis Makame hayupo sahihi, na kama anapinga madai yangu, basi naomba aruhusu tuunde tume huru tujadili na kufanya utafiti.

Tanzania kuna watu wapatao 40 milioni. Asilimia 65 ya watu millioni 40 ni watu milioni 26 ambao kwa mujibu wa takwimu za serikali wana umri chini ya miaka 18, na ambao kisheria hawakujiandikisha kupigakura.

Aidha, asilimia 35 ya watu milioni 40 iliyobakia ni watu milioni 14, ambao hawa ni watu wazima wenye umri wa miaka 18 na kuendelea. Hii ina maana kwamba watu waliokuwa na ruhusa ya kujiandikisha na kupiga kura ni asilimia 35 au watu milioni 14 tu.

Hata hivyo, kutokana na matatizo mbali mbali, ni vigumu kwa watu waliofikisha umri wa kupigakura waweze kujiandikisha.

Hata tukikadiria kwamba waliojiandikisha ni asilimia 75 ya wananchi wote wenye sifa ya kuandikishwa, basi unaweza kukuta kwamba kati ya watu milioni 14 wenye umri zaidi ya miaka 18, wanaopaswa kuandikishwa hawazidi milioni 12.5.

Kama watu wote waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 10.5 tu, sasa mbona (NEC) imetangaza kwamba watu waliojiandikisha kuwa milioni 19.6!? Hao wapiga kura milioni 9.1 wametoka wapi!? Je, hapa waliongezwa ni watu au majina ambayo yameongezwa kwenye kompyuta?

Je, kwa nini wananchi wasiamini kuwa hizo ndizo kura za vituo hewa zinazoweza kuleta utata na hata nchi kuingia katika matatizo, Mungu aepushilie mbali?

Lakini ukisilikiza maelezo ya Luteni Jenerali, Abdulraham Shimbo, mwenyekiti mwenza wa Mpango wa Elimu ya Utafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (REDET), Dk. Benson Bana na kampuni ya utafiti ya Synovate, bila shaka haraka unapata majibu.

Pamoja na NEC kukana mara kadhaa kuwa waliotajwa kuandikishwa, ndio wapigakura halali, lakini NEC lazima ifahamu kuwa uhalali na ukweli wa idadi ya orodha ya waliojiandikisha kupiga kura, bado imejaa utata.

Hata wanaoitwa Tanzania Burea of Statistics, hawewezi kuthibitisha kwamba taifa hili lina watu 43 milioni.

Maana wakikubali hilo, basi ni wazi kuwa watu zaidi ya 3 milioni watakuwa nje ya utaratibu wa bajeti ya serikali. Bajeti ya serikali iliyopita, haitaji kuwa taifa hili lina watu 43 milioni.

Hivyo basi, takwimu zilizotolewa, zisiporekebishwa kabla ya uchaguzi kufanyika, kunaweza kuwafanya baadhi ya wagombea kutokubaliana na matokeo.

Watalinganisha na mahudhurio ya mikutano yao ya kampeni na watalinganisha na wagombea wengine na alama za matokeo watakazopewa na NEC. Tusifike huko!

<p> Mwandishi wa makala hii, Dk. Noordin Jella, ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro. Amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa simu Na. 0773 000 131, emaili: norjella@yahoo.com</p>
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: