Takwimu za uandikishaji zasuta 'wachafuzi'


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

SIJATHUBUTU hata mara moja kusifia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Sijadanganyika. Wala si kawaida yangu kusifia mtumishi au taasisi, labda pale inapokuwepo sababu ambayo, nikiieleza kwenu wasomaji, mutaielewa.

Siku zote naamini mtumishi au taasisi inayofanya kazi vizuri inatimiza wajibu wake. Iweje niisifu? Si kazi yangu. Bali anayekwenda mrama na taasisi inayoshindwa wajibu naikosoa na kuelekeza njia. Sijali kitakachofuata.

Kuwepo kwangu Zanzibar kwa zaidi ya mwezi nikiwa likizo, kumenipa fursa ya kujua mengi; hata siri za Chama cha Mapinduzi (CCM) za kutafuta ushindi.

Baada ya kujua ukweli, hubadilisha mbinu kila uchaguzi ili kukidhi matakwa yao ya kubaki madarakani. Uchaguzi ujao haukusalimika. Mbinu mpya. Kila kitu mapema, ili siku ya kura, hesabu ziwe zimetimia.

“Unasemaje,” nilimuuliza kachero mmoja aliyenieleza siri ya 2010. Akadakia, “Alas, dunia itaona kila kitu safi siku hiyo kumbe mapishi yalishapikwa, kilichobaki karamu tu.”

Nikasikia wakubwa wanawasema wakuu wa Tume. Kama kawaida yao, wanapotaka kutimiziwa matakwa yao; pale waonapo mambo yao hayaendi vizuri, wakubwa hawa huirukia na kuishutumu tume.

Nao tume wakisikia shutuma za wakubwa hadharani wanaufyata. Wanajua maana yake; nini wanatakiwa kufanya kama ilivyo kawaida yao tangu uchaguzi wa 1995. Shutuma za mwisho walitoa walipojua wameshindwa. Kilichofuata? Wenye kazi yao wakaifanya na yaliyofuata, leo ni historia.

Ila niwakumbushe moja: Waandishi wa habari, wa Tanzania na wageni, tuliokuwepo makao makuu ya Tume 1995, tuliona ghafla aliyekuwa naibu katibu mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Ameir Mohamed, ametimka kutoka pale mara tu matokeo ya urais yalipotangazwa chini ya mtutu wa bunduki yakimtaja Dk. Salmin Amour Juma ndiye mshindi wa urais.

Mshangao wetu ulikuja kwa sababu tangazo hilo lilitolewa mud amfupi tangu kada huyo aishutumu ZEC kupendelea Chama cha Wananchi (CUF) na kwamba “CCM haitakubali matokeo.”

Kwa hivyo, Tume hutetereka na kugeuka mawe wakishatishwa. Watasahau hata walichotangulia kukisema na kuahidi kwa umma. Hawahofii kula matapishi yao.

Hawajabadilika kitu. Mwenyekiti wa Tume, Khatib Mwinyichande na makamishna wake wameapa ufichoni, “hawakubali kubeba aibu ya mtu yeyote safari hii.”

Hata hadharani, wapo kwenye kumbukumbu kwamba wamepata kuahidi kufanya kazi kwa kufuata sheria tu na siyo maelekezo au amri ya mtu au kikundi chochote.

Utasema wamejiamini. Kumbe, maskhara. Hawajui thamani ya dhamana waliyopewa. Hawaelewi kuwa mwisho wa siku lawama zitawashukia.

Wameshasahau yaliyosababishwa na wenzao katika tume zilizopita. Wamesahau nini alifanya Zubeir Juma Mzee mwaka 1995; Abdulrahman Mwinyijumbe mwaka 2000 na Masauni Yussuf Masauni mwaka 2005. Hawajali kwamwe yaliyotokea Zanzibar baada ya uchaguzi. Naapa wamesahau kabisa!

Ila kama wasemavyo wanasonga mbele, nasi tunaendelea kusema. Ni bahati njema sasa sura halisi ya Tume ya Mwinyichande inajianika. Hakika ni afadhali ya jana kama alivyoimba Mrisho Mpoto.

Tume hii ya wajumbe saba, wawili tu wakitoka CUF ikiwa imeundwa kwa kuzingatia muafaka wa pili, inaendeleza ubia na dola ya CCM. Haya yanaonekana kwenye takwimu wanazotoa wenyewe.

Kwa mujibu wa kifungu kilichoongezewa mwaka 2006 katika Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar ya 1985, kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ni sharti la mtu kuandikishwa kuwa mpiga kura na kuingia katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (DKWK) la Zanzibar.

Tungekuwa na serikali inayoamini kupiga kura ni haki ya kila raia si zawadi, kabla ya uandikishaji kuanza 6 Julai mwaka huu, ingekuwa imempatia kila mtu kitambulisho hiki.

Sivyo. Kitambulisho kinatolewa kibaguzi hata viongozi wa CUF kuamua kuiita “sheria ya kikaburu.” Ni ubaguzi kama ubaguzi mwingine.

Serikali imetengeneza utaratibu wa kirasimu kwa makusudi ili wale wasiowataka wasipate kuandikishwa. Kunyimwa kitambulisho ni mbinu makini. Wanaonyimwa ni pamoja na wale waliopiga kura uchaguzi uliopita.

Tangu 6 Julai, tume imekuwa ikiandikisha wapiga kura chini ya wanachoita “Uendelezaji wa Daftari.” Lakini inaonyesha wanafanya uandikishaji mpya. Vipi? Kwa kubadilisha shahada zilizotumika 2005, na kuandikisha wapiga kura wapya waliotimia umri wa kisheria wa miaka 18 pamoja na waliokosa, kwa sababu yoyote ile, kupiga kura uchaguzi uliopita, huwezi kusema ni uendelezaji daftari.

Uendelezaji ungekuwa unamtoa mwenye shahada yake. Huyu alipewa shahada na alipiga kura baada ya kuthibitishwa na tume. Wa kutolewa ni wale waliothibitika na Tume kuwa waliandikishwa zaidi ya mara moja. Hawa lazima tume inawajua ndio maana ilisema katika ripoti yake kwamba watu wapatao 3,000 walikutwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja.

Ni usaliti uliopangwa tu uliokwamisha watu hao kushitakiwa mbele ya sheria. Tume na wakubwa zake wanajua sababu ya kutoshitaki wavunja sheria hao kwa karibu miaka mitano sasa.

Ukweli, kila Mzanzibari anayetaka kushiriki uchaguzi ujao, lazima aende kituo cha kuandikisha wapiga kura ili kuandikishwa. Hata wale wenye shahada za uchaguzi uliopita, lazima nao waende kituoni na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi. Uendelezaji gani huu? Ni uandikishaji mpya uliolenga kutimiza dhamira mbaya.

Serikali imeshasema imeunganisha hifadhi ya kumbukumbu ya wapiga kura na wananchi wanaopata vitambulisho. Ndio kusema takwimu za wapiga kura zinafungamana na za vitambulisho.

Muungano huu wa kitakwimu, unamaanisha kuwa idadi ya wenye vitambulisho haipaswi kuzidi wapigakura walioandikishwa. Lazima hesabu ziwiane au wapiga kura wapungue kwa kuwa inawezekana mtu mwenye kitambulisho asitokee kujiandikisha.

Lakini haiwezekani idadi ya wapigakura izidi wenye vitambulisho. Na ikitokea, ina maana taasisi hizo mbili zimefanya udanganyifu katika kutoa huduma kwa wananchi.

Malalamiko ya watu kunyimwa vitambulisho yanaendelea kila mahali na tayari mamia wamekosa kuandikishwa katika majimbo tisa yaliyokamilisha uandikishaji. Kisa ni kukosa kitambulisho.

Bila ya shaka tume haitaandikisha wapigakura kama ilivyokisia kulingana na hesabu za 2005 na tathmini ya mwenendo wa ukuaji wa idadi ya watu.

Na hapa ndipo Mkurugenzi wa Idara ya Usajili na Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi, Mohamed Juma Ame, anaposema, “Nawapa challenge Tume hawataandikisha wapiga kura kwa idadi ya watu tuliowapa vitambulisho.” Kwake anaamini amepiga bao!

Idadi itafikiwaje penye urasimu wa makusudi uliolenga kupunguza wapigakura kwa kisingizio cha kitambulisho? Laiti serikali ingempa kila mtu kitambulisho kama sheria isemavyo, nani angekaa nje?

Hata wanasiasa wasingethubutu kuzuia watu kujiandikisha. Uzoefu unaonyesha Wazanzibari wako juu katika elimu ya uchaguzi. Ile kila mmoja kutaka aandikishwe licha ya mabomu na maji ya kuwasha ni ushahidi.

Uunganishaji takwimu za daftari na vitambulisho ni mbinu ya wakubwa kutafuta ushindi wa nguvu; tena kabla ya Oktoba mwakani. Wenyewe watakuja kuita “ushindi wa tsunami.”

Takwimu za Tume zinaonyesha katika baadhi ya shehia imeandikisha wapigakura kupita watu waliopata vitambulisho. Kwa mfano, jimbo la Tumbatu, watu 1,047 wamepata kitambulisho, walioandikishwa kupiga kura ni 2,644. Tofauti ni 1,597.

Jimbo la Tumbe, waliopata kitambulisho 120, walioandikishwa kupigakura ni 2,336. Tofauti watu 2,216. Jimbo la Ole, waliopata vitambulisho 144, walioandikishwa kupigakura 258. Tofauti ni 114. Shehia ya Bwereu Nungwi, waliopata vitambulisho ni 17 walioandikishwa ni 398. Tofauti ni 381.

Swali: Hawa waliozidi wameandikishwa kwa utaratibu upi?

Ama kweli, hali inavyojionesha; kauli za viongozi wa CCM, nguvu za dola zinazoshuhudiwa maeneo ya uandikishaji, na simulizi za siri, zinaleta picha kwamba Zanzibar kunaandaliwa uchafuzi mwingine, si uchaguzi.

Inshaallah nitawaeleza nilichojifunza ziarani Ofisi Kuu ya Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: