Tambo za kuingia ikulu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM Abdulrahman Kinana

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kina mtaji wa kutosha kukiwezesha kushinda na kubaki ikulu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya CCM Abdulrahman Kinana, amesema tayari wana wabunge 19 na madiwani 562 hata kabla ya uchaguzi. “Huu ni mtaji tosha,” ameongeza.

Anasema bajeti ya serikali kwa elimu imeongezeka kutoka Sh. 1 trilioni hadi Sh. 2.4 trilioni huku idadi ya wanafunzi chuo kikuu ikikua kutoka 38,000 kati ya mwaka 1961 na 2005 hadi 122,000 leo hii.

Kinana anasema pia kuwa chama chake kimetekeleza kwa zaidi ya asilimia 90 ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005.”

Kinana alikuwa akieleza kwa nini chama chake kinajitapa kushinda hata kabla ya uchaguzi kufanyika na matokeo kutangazwa.

Anasema kati ya vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huu, “ni CCM pekee iliyosimamisha wagombea ubunge katika kila jimbo na wagombea udiwani katika kila kata.” Nchi nzima ina majimbo ya uchaguzi 239 na kata 3,335.

Anasema mbali na vigezo hivyo, ni mgombea urais wa CCM pekee ambaye ameweza kutembelea majimbo yote ya uchaguzi na kuzungumzia hoja zinazohusu eneo alilotembelea.

Katika nafasi ya urais, Kinana anasema chama chake kinatarajia kushinda nafasi ya urais kwa zaidi ya asilimia 80 na kwa nafasi ya ubunge kwa zaidi ya asilimia 90.

Alipoulizwa iwapo mgombea wake hatafikia kiwango hicho cha ushindi atajisikiaje, Kinana alisema, “Asiposhinda hivyo basi, wapigakura watakuwa wameamua.”

Kuhusu nafasi ya upinzani kushinda nafasi hiyo, Kinana anasema vyama vya upinzani haviwezi kushinda nafasi ya urais kwa sababu mbili kubwa.

Kwanza, kwa kuwa ni vichanga na pili, kwa kuwa viongozi wa upinzani “wametumia muda mwingi kulalamika na kuzua mambo ambayo hayapo, badala ya kunadi sera.”

Kuhusu madai kwamba chama chake kimeanzisha vikundi vya vijana vinavyofahamika kama Green Guard ambapo mkoani Kilimanjaro wanaita “Interahamwe” kwa kuwa vimekuwa vikichochea vurugu, Kinana amekana madai hayo.

“Si kweli. Tuna vijana wa UV-CCM ambao jukumu lao ni kulea viongozi wa baadaye wa CCM, kuhamasisha mikutano ya kampeni na kusaidia wapenzi wetu na wanachama kwa jumla kwenda kupigakura.”

Alipong’ang’anizwa kwamba gazeti hili limepata ripoti ya UV-CCM ya mwezi uliopita, inayokiri chama hicho kuanzisha vikundi vya vurugu, Kinana amesema, “Hakuna mahali popote ambapo CCM imekubali jumuiya zake kuanzisha vikundi vya vurugu.”

Kuhusu kauli za Kikwete kuwa wanaotumia udini na ukabila wanataka kuleta maafa, huku UV-CCM wakikiri kuwa udini na ukabila ndivyo vilivyoleta mgawanyiko ndani ya chama hicho wakati wa kura za maoni, Kinana anajibu:
“Kila uchaguzi unapofika, ukabila na udini vinajitokeza. Lakini sisi wakati wowote tunapiga vita mambo haya,” anaeleza.

Akizungumzia maneno ya kuwa kura “zikiibiwa hatutakubali;” na kwamba hata chama chake kimekuwa kikiyatumia maneno hayo kama mtaji, Kinana alikana chama chake kuyatumia.

Alipoulizwa iwapo anaamini kuwa vita vinaweza kutokea pale CCM itashindwa, haraka Kinana alijibu, “Siamini kama CCM au chama chochote cha siasa, iwapo kitashindwa uchaguzi, kinaweza kuleta vita.”

Anasema kama kuna yeyote ambaye anaona hakuridhika na mchakato wa uchaguzi ulivyokwenda, anaweza kwenda mahakamani kupinga matokeo yatakayotolewa.

Alipoulizwa anaonaje hatua ya mgombea wake kutoa ahadi ambazo kama hazitatekelezwa, basi chama kitakuwa kimekufa; lakini zikitekelezwa hata kwa nusu, wanaweza kuendelea kujikongoja, Kinana alijitapa kwamba kila kilichoahidiwa kitatekelezwa.

“Kila ahadi ambayo mheshimiwa Kikwete ameahidi itatekelezwa. Ni kwa sababu, kila ahadi ameifanyia utafiti. Amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 20 akiwa waziri na mbunge. Amekuwa rais kwa miaka mitano sasa; anajua shida za wananchi,” anaeleza.

Kinana anasema, “Ni kweli baadhi ya ahadi alizotoa kama ilivyokuwa mwaka 2005 hazimo kwenye ilani ya uchaguzi ya chama chetu. Lakini zote hizo kama ilivyokuwa mwaka huo, zitatekelezwa.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: