TAMISEMI yachelewesha kanuni za uchaguzi


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 04 August 2009

Printer-friendly version

WAKATI uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji unafanyika nchini kote Oktoba mwaka huu, hadi sasa serikali haijatoa tangazo rasmi linaloelezea kanuni na taratibu za uchaguzi huu.

Tangazo hilo kwa mujibu wa sheria za Tanzania hulotolewa kupitia Gazeti la Serikali na Waziri anayehusika kisheria kusimamia uchaguzi huo. Huyu ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Tangazo hilo linafuta zile kanuni zilizotumika katika uchaguzi kama huo uliofanyika mara mwisho nchini, ambayo ni mwaka 2004. Hiyo inafanyika ili kuingiza mabadiliko na kanuni na taratibu. Waziri wa TAMISEMI ni Celina Kombani.

Hata hivyo, kuna taarifa kwamba rasimu ya kanuni za uchaguzi huo, iko tayari imeandaliwa. Hali inaonesha waliobahatika kuiona wana kitu kinachofanana na taarifa nilizonazo.

Kwa vile muda wa Tamisemi kuelimisha na kuhamasisha wananchi ushiriki wao katika uchaguzi huo ni mfupi, hebu tujadili dondoo za kanuni hizo zilizovuja kwa shabaha ya kuandaa watu kushiriki kikamilifu katika kutimiza mahitaji hayo ya kikatiba.

Kifungu cha 5(1) cha Kanuni hizo kinasema Waziri atatoa Tangazo la Uchaguzi kwa umma katika magazeti ya Kiswahili na Kiingereza yanayosambazwa nchi nzima siku tisini 90 kabla ya siku ya uchaguzi ili umma upate kujiandaa na uchaguzi huo.

Kifungu kidogo cha (2) kinasema tangazo litakalotolewa na waziri litaelekeza mambo yafuatayo: ratiba ya uchaguzi na shughuli zinazohusika na masharti muhimu ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni hizo.

Kutakuwa na utangazaji wa majina na mipaka ya vijiji na vitongoji ambako kutafanywa na Msimamizi wa Uchaguzi. Tangazo hilo litatolewa siku 50 kabla ya kutoa maelekezo kuhusu uchaguzi.

Wajumbe wa wa Halmashauri ya Kijiji hawatapungua 15 na hawatazidi 25, ambao ni Mwenyekiti wa Kijiji; Wenyeviti wa Vitongoji vilivyomo katika eneo la Kijiji; na Wajumbe watakaochaguliwa wakiwemo wanawake ambao idadi yao haitakuwa chini ya robo ya wajumbe wote wa Halmashauri ya Kijiji.

Kipengele hicho cha wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji ni muhimu kufahamika hasa miongoni mwa wanawake wanaopewa nafasi kwa kiwango kisichopungua robo ya wajumbe wote.

Kipengele hiki kimewekwa makusudi ili kuondokana na mfumo dume wa idadi ya wajumbe wanaume katika wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji kutawala ile ya wanawake.

Kanuni zinasema pia kwamba Afisa Mtendaji wa Kijiji atakuwa Katibu wa Halmashauri ya Kijiji.

Msimamizi wa Uchaguzi atatoa maelekezo kuhusu uchaguzi. Hii itakuwa ni siku 28 kabla ya siku ya uchaguzi. Maelekezo ya uchaguzi, kwa mujibu wa kanuni, yataelekeza mambo yafuatayo:

Tarehe ya kufanyika uchaguzi, muda na sehemu ya kuandikishia wapiga kura na muda na mahali pa kufanyia uchaguzi.

Msimamizi pia atatoa maelekezo yanayotaka wakazi wote wenye sifa za kupiga kura washiriki uchaguzi; kutaka wakazi wenye umri wa miaka 21 au zaidi wanaotaka kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji, Mjumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji wachukue fomu za kugombea. Fomu hizi zinapatikana kwenye ofisi ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.

Rasimu iliyovuja inasema tarehe na muda wa kuchukua na kurudisha fomu za maombi ya kugombea uenyekiti wa kijiji, ujumbe wa halmashauri ya kijiji na uenyekiti wa kitongoji zinaagiza muda wa kuchukua na kurudisha fomu za kugombea kuwa siku saba.

Kuna muda wa siku ambayo uteuzi utafanyika na mahali pa matangazo ya uchaguzi ambapo pia fomu za wagombea zitabandikwa ili wapiga kura wazione; muda wa kutoa pingamizi dhidi ya uteuzi na kusikilizwa pingamizi; na tarehe ya kusikiliza rufaa dhidi ya uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.

Kipindi cha kuendesha mikutano ya kampeni kwa mujibu wa kanuni hizo, hakitazidi siku saba (7) kuanzia siku ya uteuzi.

Uandikishaji orodha ya wapiga kura katika kitongoji kwa ajili ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji utafanyika siku sitini (60) kabla ya siku ya uchaguzi na utafanywa na watumishi wa umma.

Watendaji wa vijiji, Mitaa na Kata hawataruhusiwa kuandikisha na kuandaa orodha ya wapiga kura.

Uandikishaji wa orodha ya wapiga kura utafanyika kwenye majengo ya umma; pale itapokuwa hapana jengo la umma, uandikishaji utafanywa sehemu ambayo Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atakuwa amekubaliana na viongozi wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa.

Pingamizi dhidi ya mtu kuandikishwa kuwa mpiga kura litawasilishwa kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ambaye atalitolea uamuzi na kurekebisha orodha ya wapiga kura iliyotangazwa katika muda wa siku tano (5) kuanzia tarehe ya kuwasilishwa pingamizi hilo.

Mtu yeyote au chama cha siasa ambacho hakitaridhika na uamuzi wa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi kitawasilisha rufaa kwa Msimamizi wa Uchaguzi ambaye ataishughulikia rufaa hiyo katika muda wa siku tano (5) baada ya kupokea rufaa hiyo.

Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi kuhusu rufaa iliyowasilishwa utakuwa wa mwisho.

Kuhusu sifa za kupiga kura na kugombea, mkazi yeyote wa kitongoji atakuwa na haki ya kupiga kura lakini sharti awe raia wa Tanzania, mwenye umri wa miaka 18 au zaidi; mkazi wa kawaida wa eneo la Kitongoji; na hana ugonjwa wa akili.

Sifa za kugombea uenyekiti wa Kijiji au ujumbe wa Halmashauri ya Kijiji au uenyekiti wa Kitongoji ni mtu kuwa raia wa Tanzania; umri wa miaka 21 au zaidi; uwezo wa kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza na kipato halali cha kumwezesha kuishi;

mkazi wa kawaida wa eneo la Kitongoji; mwanachama na amedhaminiwa na chama cha siasa.

Sifa nyingine za kugombea ni mtu kutokuwa amewahi kupatikana na hatia kwa kosa la utovu wa uaminifu na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi sita (6) au zaidi au adhabu ya kifo; na hana ugonjwa wa akili uliothibitishwa na daktari anayetambulika na Serikali au Bodi ya Utabibu.

Kwa kifupi umri wa kupiga kura ni zaidi ya miaka 18, wakati umri wa kugombea ni zaidi ya miaka 21. Kila mgombea lazima adhaminiwe na chama cha siasa.

Ndio kusema utaratibu wa ugombeaji binafsi katika uchaguzi – ugombeaji usiokuwa wa kuwakilisha chama cha siasa – ambao tayari umeamriwa na Mahakama ya Kuu mwanzoni mwa mwaka huu kutaka Serikali iutekeleze katika uchaguzi unaofuata (kuanzia huu wa Serikali za Mitaa), haujazingatiwa katika kanuni hizo za uchaguzi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: