Tamko la viongozi wa dini


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 27 May 2013

Printer-friendly version

WIKI mbili zilizopita, Maaskofu Peter Kitula (CCT), Tarcisius Ngalalekumtwa (TEC), David Mwasota (PCT) na Mark Malekana (SDA) –walikutana na Rais Jakaya Kikwete, ikulu jijini Dar es Salaam. Kabla ya mazungumzo na rais, viongozi walimsomea tamko ambalo linachapishwa hapa chini:  

UTANGULIZI

Mheshimiwa Rais, awali ya yote tunashukuru kupata nafasi hii ya kukutana nawe na kuzungumza juu ya masuala yanayogusa mustakabali wa Taifa letu.

Pili, tunapenda kukupa pole kwa majukumu yako mazito. Tunaunga mkono juhudi zako katika maeneo mengi ya maendeleo na kukuombea mafanikio.

Hata hivyo, tunapenda kugusia masuala kadhaa ambayo kama hayatashughulikiwa haraka na kwa umadhubuti mkubwa yanaweza kulitumbukiza taifa letu katika migogoro ya hatari.

AMANI NA USALAMA WA TAIFA LETU

Kwa kipindi cha takribani miongo mitatu hali ya usalama na uhusiano wa dini mbalimbali nchini kwetu imekuwa si nzuri. Mtiririko wa matukio unaonesha kuwa tangu zilipoanza chokochoko za mihadhara ya kidini na baadae kuchochewa na madai ya Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu Duniani (OIC) katika miaka ya 1990 hali ilianza kubadilika.

Kwa wakati mbalimbali hali hii ilikemewa vikali na ikatulia. Kadiri siku zinavyokwenda ndivyo uhusiano kati ya wakristo na waislamu unavyozidi kuzorota na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa wananchi.

Tarehe 15 Januari 2011, kundi la waumini wa madhehebu ya Kiislamu walikutana katika ukumbi wa Diamond Jubilee na kutangaza kuwa nchi hii inaongozwa kwa Mfumo Kristo. Kwamba mfumo kristo umeenea nchi nzima; mfumo huo kristo uliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Wanaendelea kudai kuwa wakristo hupendeleana katika kupeana nafasi za uongozi, huapishwa makanisani na maaskofu; na kwamba wakristo wamekuwa wakipewa fedha na serikali kujenga shule na hospitali kupitia Memorandum of Understanding (MoU).

Walidai kwamba hata Baba wa Taifa mwaka 1972 alijenga hospitali ya Bugando jijini Mwanza kwa fedha iliyotolewa na wafanyabiashara wa Kuwait badala ya kujenga barabara toka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kusini na maeneo mengine mengi ya nchi.

Viongozi hawa wa Kiislam wamezunguka nchi nzima kueneza uchochezi mwingi na kutangaza vita dhidi ya Ukristo. Wanadiriki kusema kuwa kuwa Muungano wetu ni kichaka cha mfumo Kristo. Kundi hili la Waislamu walihitimisha makongamano yao yaliyofanyika nchi nzima 16 Oktoba 2011 kwa kuazimia kuua na kuuawa.

Serikali yetu haijwahi kukanusha juu ya madai na tuhuma hizo na wala haijawakamata wahusika.

Mara kadhaa tumeinua sauti yetu kuelezea hali hii na imefika mahali tunashawishika kuamini kuwa wale wanaohusika na waliopa kuilinda katiba ya nchi yetu; katiba iliyojengwa juu ya misingi ya kuheshimiana, na kujenga taifa lenye mshikamano, umoja na amani wanaipuuzia sauti yetu na wanapuuzia mustakabai wa taifa letu.

Hatujui kupuuzia huku katika jambo muhimu kama hili ni kwa faida ya nani. Kutokujibu wazi masuala yaliyoibuliwa na matamko mawili ya Jukwaa la Wakristo (Desemba 2012 na Machi 2013) kunatufanya tufikirie kuwa serikali inapuuza yale tunayouiuliza.

Tatizo la mihadhara ya kidini (kupitia misikiti, radio, televisheni na magazeti) inayokashfu na kutukana ukristo imekuwa ikiendelea bila ya wahusika kuchukuliwa hatua.

Mihadhara hii inafanyika katika nyumba za ibada na nje ya nyumba za ibada bila kificho. Dhima ya mihadhara hii imekuwa uchochezi na kupandikiza chuki dhidi ya ukristo, kitangaza nia ya kuua viongozi wakanisa na kupambana na kanisa.

Yamekuwepo matukio ya mashambulizi na mauaji ya viongozi wa kikristo, uchomaji wa makanisa na vitisho visivyokoma kupitia mihadhara hii ya kidini. Wanaendesha mihadhara na makongamano hayo wanafahamika vizuri. Lakini watu hao hawachukuliwi hatua. Katiba yetu hairuhusu mtu kuingilia uhuru wa mtu yeyote wa kuabudu.

Vipo vituo vya mafunzo ya Jihad huko Ukerewe, Kiwalani, Morogoro na kwingineko. Tumejitahidi kuwasiliana na ofisi husika mpaka za juu kabisa katika taifa letu, tukitoa malalamiko yetu na vielelezo (CD, DVD, VCD) zinazoonesha wazi jinsi ambavyo baadhi ya watu hapa nchini wanavyochochea na kwa makusudi kutikisa misingi ya amani na umoja wa kitaifa.

Lakini hatujapewa majibu yoyote na wala hatuoni hatua madhubuti zikichukuliwa li kudhibiti hali hii. Badala yake, Wakristo ndiyo wanazuiwa wasione DVD na CD hizo, ili wasijue kinachohamasishwa dhidi yao.

Daima yamekuwepo matamko mpesi mepesi yanayotoka kwa viongozi wa serikali, matamko ambayo katika yenyewe hayaoneshi kuwa na nguvu ya kugeuza hali inayoendelea kukua na kuota mizizi katika taifa letu. Na zaidi sana umeendelea kutolewa mwaliko wa Wakristo na Waislam kukaa na kutatua tofauti zao.

Kanisa halina ugomvi na Uislam wala Waislamu, bali linaitaka serikali kukemea uchochezi na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.

Imefika mahali ambapo imedhihirika wazi kuwa sheria haichukui tena mkondo wake; na wale waliopa kulinda na kuitetea katiba hawafanyi hivyo. Badala yake wanabaki kutoa maelezo yasiyotoa ufumbuzi kwa tatizo hili na kuwaacha wale wanaolivunja taifa kwa misingi ya dini wakiendelea na kampeni yao bila kuzuiliwa.

Kauli nyepesi nyepesi zinazotolewa juu ya hatari kama hii zinazidi kutia hofu. Hata kama kauli zingekuwa nzito lakini kama haziendani na kuchukuliwa kwa hatua nzito; na ikajulikana kuwa hatua nzito zimechukuliwa, zinazidi kulipasua taifa letu vipande vipande.

Maelezo ya kwamba viongozi wa dini wakae pamoja kujadili uvunjifu wa amani wakati serikali haishughulikii hali hii kwa nguvu zote hayasaidii kutatua mgogoro uliopo. Kwa maneno mengine, serikali inapolisukumia tatizo hii linalopaswa kudhibitiwa kisheria kwa viongozi wa dini, ni kujivua wajibu wake wa kuwahakikishia raia wote wa nchi hii amani na usalama wa maisha na mali zao.

Kwa yeyote anayelitakia mema taifa hili, hawezi kutulia anapoona vitendo vya uvunjifu wa amni na kukosa kuvumiliana vikizidi kushamiri. Hali hii inatusukuma kujiuliza na kuuliza kama ni kweli tumefika mahali pa kushindwa kudhibiti hali hii na kujenga taifa lenye amani, mshikamano, kuheshimiana na kuvumiliana.

Usalama na amani ya taifa letu unamgusa kila mtu na wakristo hatufurahi damu ya mtu yeyote kumwagika. Lakini kinasa linapopaza sauti yake kuitaka serikali itimize wajibu wake, Kanisa linaambiwa kuwa linatumiwa na wanasiasa na sasa wakristo wanamilikishwa UCHADEMA, na hatujui wasiokuwa wakristo wamemilikishwa chama gani.

MGOGORO WA NANI ACHINJE, NANI ALE

Katika mwendelezo huo huo, leo taifa limeingia kwenye mgogoro mwingine wa nani anayeruhusiwa kuchinja. Mgogoro huu umegharimu maisha ya Mchungaji Matayo wa kanisa la Pentecostal Assemblies of God of Tanzania (PAGT) aliyeuwawa Buseresere, mkoani Geita na baadhi ya waumini wa dini ya kiislam na uharibifu wa mali.

Mgogoro huu unazidi kulipasua taifa na viongozi wetu wamekuwa wakilitolea maelezo ambayo hayakidhi na ambayo katika yenyewe yanavunja sheria na katiba ya nchi hii ibara ya 19 inayosema: “Kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini…”

Mgogoro wa uchinjaji wa wanyama umepanuliwa na viongozi wa serikali kupitia matamko yao na melekezo yao (ushahidi wa vielelezo tunavyo).  

Tanzania siyo taifa la kwanza kuwa na mgogoro wa kuchinja. Ni muhimu kuondoa kigugumizi na kuweka bayana misingi ya katiba na sheria katika hili. Tunapendekeza kwa kuwa kuchinja kwa wenzetu waislamu ni ibada, hata hivyo wakristo wasilazimishe kushiriki ibada za wengine.

Ipo hofu ya nchi kugawanyika kwa misingi ya dini. Ni kweli maana ndani ya nchi yetu kuna taasisi ya halal, kuna Islamic bank ndani ya taasisi ya serikali, wanafunzi wanavaa hijab na wengine kofia za kidini shuleni, nk.

Mlolongo huu na madai yanayoongezeka ya kurasimisha dini moja ni mwendelezo wa ufa unaozidi kupanuka. Leo hii, udini umeingia mashuleni na katika vyuo vyetu vya elimu ya juu, hasa chuo kikuu cha Dodoma na kufanya hali kuwa tete; na serikali imeichia hali hiyo kukua.

Mheshimiwa Rais, taifa linasubiri tamko zito kutoka kwako: Usisimame katikati na kujaribu kuufurahisha kila upande au kutaka kuonesha usawa kwamba kila upande una makosa.

Si sawa kulichukulia tendo la mtoto aliyekojolea Koran kana kwamba limetendwa na mtu mzima au ni mpango wa wakristo. Si sawa kulichukulia tendo la kumwagiwa tindikali Sheikh Soraga kuwa sehemu ya uwiano wa matendo wanayotendeana Wakristo na Waislam.

Tunapenda kuweka wazi kwamba wale amabo wanaoichukulia sauti ya kilio chetu cha kuikumbusha serikali wajibu wake kuwa ni mpango wa kikiristo kuiondoa serikali iliyo madarakani wanapotosha ukweli kwa hasara ya taifa hili.

Viongozi wa kikristo, kama raia wa nchi hii wanaamini kuwa wana wajibu wa kusaidia kulijenga taifa na kusaidia kujenga mustakabari mwema wa Tanzania ya leo na Tanzania ya vizazi vijavyo. Na siyo vizuri kuwagawa viongozi wa dini ya kikristo yanapozungumzwa masuala yanayolihusu taifa zima. Wachache wenye nia zao binafsi wanaweza kuleta uchonganishi baina ya serikalina viongozi wa dini ya kikristo. Tanzania ni yetu sote.

Viongozi wa kikristo wangependa kuiona serikali yetu ikiongoza umakini katika kushughulia viashiria vya chokochoko nchini, iwe ni vya kidini, kikabila au vya kiusalama. Zaidi sana viongozi wa kikristo wangependa kuona fursa ya mazungumzo na rais juu ya masauala mazito yanayohusu mustakabari wa taifa letu yanafanyika kwa wakati muafaka na hatua madhubuti zinachukuliwa.

Tungependa serikari yetu itolee ufafanuzi na kujibu hoja zetu hasa zifuatazo: Je, serikali yetu inaendeshwa kwa mfumo kristo?

Memorandum of Understanding (MoU) ya 1992 ina maana gani?

Je, ruzuku inayotolewa katika hospitali za taasisi binafsi ni matokeo ya hiyo MoU ya mwaka 1992? Ni kweli kwamba serikali inatoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa shule na hospitali za makanisa? Waislamu wamekuwa wakidai kuwa wakristo na maaskofu wao wameunda chama, ni nini msimamo wa serikli katika jambo hili?

Tunauliza hivyo kwa sababu baadhi ya wanasiasa wa chama tawala wamediriki kulieleza Bunge kwamba CHADEMA ni chama cha wakristo.

Vilevile, kuna madai kuwa kanisa katoriki lina majeshi ya vita, hivyo ndivyo serikali inavyofahamu?

Kwa upande wetu sisi Wakristo tungependa kujua nini hasa kosa la Askofu Augustine Mpemba wa kanisa la Tanzania Field Evengelism, anayetafutwa na vyombo vya dola, na kwa nini atafutwe.

Serikali inapokaa kimya bila kuyatolea maelezo masuala haya, nani atakuja kuwaeleza waislamu na wananchi kwa ujumla kuwa maelezo yao si ya kweli.

Mwisho, mheshimiwa rais, baada ya utangulizi huu mfupi, tungependa kujadiliana nawe kwa kirefu juu ya masuala haya na mengine yanayoweza kujitokeza.

0
No votes yet