TANESCO na giza la kujitakia


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 30 September 2008

Printer-friendly version

MGAWO wa umeme uliotangazwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) unaweza kuelezwa kuwa wa “bandia.”

Kwani taarifa za ndani ya shirika hilo zinasema, “Kwa vyanzo vya umeme vilivyopo nchini, na kiasi cha fedha ambazo Tanesco inadai wateja wake, kusingekuwa hata na ndoto ya kukosa umeme.”

Wiki iliyopita Tanesco ilitangaza mgawo wa umeme nchi nzima ikisema kuna upungufu wa megawati 40 katika mahitaji yake kutokana na kuharibika kwa mitambo miwili ya kampuni ya Songas inayozalisha umeme wa gesi.

Tanzania ina matumizi ya megawati 670 kwa siku, lakini Tanesco ina uwezo wa kuzalisha na kununua megawati 1,033 kwa siku.

Mgawo wa umeme umekuja siku tatu tangu kuharibika kwa mitambo ya umeme ya Songas na mwezi mmoja tokea Tanesco itangaze kusitisha mkataba wake na kampuni ya Dowans iliyorithi mkataba wa kitapeli wa kuzalisha umeme wa kampuni ya Richmond.

Aidha, mgawo wa umeme umetangazwa baada ya serikali kuacha kununua umeme kutoka kampuni ya Aston.

Habari za ndani ya Tanesco zinasema mgogoro upo kwenye utawala wa sasa wa shirika hilo ambao hauna mipango ya muda mrefu, ya kati wala ya muda mfupi na kwamba kama mipango hiyo ipo, basi imefungiwa makabatini.

Kwa mfano, wakati Tanesco ikivunja mkataba wake na Dowans na kuacha kununua umeme wa IPTL na Aston, ilistahili kuwa imeweka njia mbadala za kuziba pengo hilo. Hakuna ushahidi kuwa imefanya hivyo.

Nchini kuna mitambo inayotumia dizeli ambayo imeunganishwa kwenye gridi ya taifa lakini hivi sasa haifanyi kazi kwa maelezo kuwa inahitaji ukarabati.

Mitambo hiyo ni ile iliyopo Ubungo jijini Dar es Salam, Zuzu mkoani Dodoma, Iyunga iliyoko mjini Mbeya, Nyakato ya jijini Mwanza na Tabora.

Inakadiriwa kuwa mitambo hiyo ina uwezo wa kuzalisha megawati kati ya 40 na 100 na inahitaji ukarabati unaokadiriwa kugharimu kati ya Sh. 30 na 50 bilioni.

Kinacholeta faraja kwa wanaojali Tanesco na wanaoona mbali ni kwamba hivi sasa shirika hilo linadai wateja wake zaidi ya Sh. 250 bilioni ambazo hata nusu yake tu ikikusanywa mashine za dizeli zinaweza kukarabatiwa.

Hata kabla ya kukusanya fedha kutoka kwa wadaiwa, hadhi ya Tanesco inaruhusu shirika hilo kupata mkopo kutoka benki yoyote ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, gharama za kukarabati mitambo ni kidogo sana zikilinganishwa na mapato ya shirika kutokana na nishati yake inayoendesha viwanda, maofisi na sekta nyingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idrissa Rashid alitangaza mapema mwaka huu kuwa shirika lake limepata mkopo wa zaidi ya Sh. 270 bilioni kutoka mabenki mbalimbali ili kuboresha utendaji wake.

“Uko wapi uboreshaji wa shirika kama siyo kuweka mipango ya kuongeza uzalishaji wa aumeme na kuhakikisha nchi haikai gizani,” anasema Aloyce Kimaro, Mbunge wa Vunjo (CCM).

“Lakini kuna nini kwenye umeme? Mbona kila siku matatizo tu? Au kuna njama hapa ili sisi tuliokuwa tunapigania mambo haya tuonekane wapuuzi na waweze kurejesha makampuni yaliyofukuzwa?” anauliza Kimaro.

Anasema kusije kuwa na hila na njama za kurudisha Dowans “tuliyoifukuza na Aston ambao mkataba wao umekwisha.”

MwanaHALISI imeambiwa, hata hivyo, kuwa Dk. Rashid alishauriwa na wataalam wa shirika kutumia sehemu ya fedha za mkopo kwa ajili ya ukarabati wa mitambo hiyo ya dizeli lakini hakukubaliana nao.

Miongoni mwa wadaiwa wakuu wa Tanesco ni serikali inayodaiwa Sh. 23 bilioni, serikali ya Zanzibar Sh. 7 bilioni na watu binafsi Sh. 220 bilioni.

Madeni katika serikali mbili za Muungano na Zanzibar, yanayofikia Sh. 30 bilioni yanalingana na kiasi ambacho shirika limekadiria kutumia kukarabati mitambo ya dizeli. Bado watawala Tanesco hawastuki.

Badala ya kufanya hivyo, Tanesco imeendelea kulipa mamia ya wafanyakazi wanaofanya kazi katika mitambo iliyoharibika na ambao hawazalishi chochote.

Kwa hiyo, kwa kuzingatia fursa zilizopo za shirika kujiimarisha, kama utawala ungekuwa makini, na kama serikali ingejali, kusingekuwa na uhaba wa umeme wala mgawo.

Tangu wiki iliyopita uvumi umeenea jijini Dar es Salaam kuwa gesi ya Songo Songo imepungua na kwamba huo ndio msingi wa kuanzisha mgawo.

Pamoja na kwamba huo ni uvumi, maofisa wa Tanesco walioongea na mwandishi wa makala hii walisema, “Uliza hata huko serikalini kama kuna mipango yoyote ya kuongeza miundombinu ili gesi hiyo ipatikane kwa wingi na inayokidhi mahitaji.”

Taarifa zinasema Tanesco, wakati wa neema,  imekuwa ikizalisha megawati 535 kupitia mabwa yake. Mabwawa yamekuwa yakichangia wastani wa megawati 80 bwawa la Mtera; Kidatu (200), Kihansi (180), Pangani (66), Nyumba ya Mungu (8) na Hale (21).

Aidha, shirika limekuwa likinunua umeme unaokadiriwa kuwa: IPTL (mw 100), Aston (40), Songas (40), Aggreko (40), ex-Warstila (100) na Dowans (100).

Hata hivyo, kumekuwa na hotuba za bajeti na ahadi mbalimbali za serikali kuhusu uendelezaji miradi ya nishati ya umeme.
 
Miradi ambayo imekuwa ikitajwa mara kwa mara ni ile ya Rusumo (Ngara, Kagera), Rumakali (Makete, Iringa), Mpanga (Ruvuma), Masigira (Iringa) na Stigler’s Gorge (Pwani).

Vilevile kumekuwa na matamko ya serikali ya kuunganisha gridi ya taifa na umeme kutoka Zambia. Hili na mengine hapo juu, yamebaki kauli za kisiasa katika kujibu hoja za wabunge.

Mgodi wa mkaa wa mawe Kiwira ni chanzo kingine cha nishati ya umeme. Serikali imekuwa ikisema kuwa utaanza kutoa megawati 50 za mwanzo (kati ya megawati 200) ifikapo Machi mwakani.

Hili nalo halina ushahidi iwapo litatekelezwa ili kuondoa taifa katika adha ya giza; kushindwa kuzalisha viwandani na katika maisha ya kawaida ya wananchi wanaotegemea umeme kwa biashara zao ndogo.

Karibu yote haya yanategemea uongozi wa shirika lililokabidhiwa jukumu la kukuza vyanzo vya nishati ya umeme na kusambaza umeme nchini.

Katika hili, Dk. Rashid anawajibika kuwaambia wananchi juu ya uendelezaji miradi hii, ahadi za serikali katika eneo hili na kama kuna mipango, basi imefikia wapi.

Kwa mfano, anapaswa kueleza, umeme unaozalishwa na vituo vya dharula, kama Aggreko, unatumikaje na kwa kiasi gani?

Kauli za sasa, kwamba mtambo mmoja au miwili ikikwama hapo Ubungo, basi mgao wa umeme umeanza mara moja, haiwezi kukubalika.

Hata Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja ni viongozi wa kushangaa kwa kauli zao za haraka katika kuunga mkono watendaji Tanesco.

Mbona waziri mkuu na waziri wake hawawaulizi watawala wa Tanesco wanafanya nini ili mgao usitokee tena. Hapa kuna ubia wa kauli tu.

Kuna kila sababu ya kuangalia upya nani wanapaswa kuongoza shirika la umeme; wale wanaojua kwamba giza likiingia, basi litakuwa limeingia pia katika ajira zao.

Ilivyo sasa, watawala wa Tanesco wataendelea kutangazia umma kuwa hakutakuwa na umeme. Wao watawasha jenereta na kuendelea kwenda ofisini. Kwa nini hali hii isiishe leo?

0
No votes yet