TANESCO: Kampuni ya 'kuleta giza'


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete amepata kusema "Taifa halitaingia gizani," kauli ambayo inakuja baada ya Shirika la Umeme (TANESCO), kuonekana kukata tamaa.

Watani ambao husubiri majanga ndipo waje na kejeli, tayari wamesema TANESCO imegeuka shirika la “kuleta giza.” Hii inatokana na malumbano yasiyoisha na hoja zisizo na ncha kuhusu kupatikana kwa umeme nchini.

Leo hii, mikoa yote inayotegemea umeme kutoka gridi ya taifa inapata umeme kwa mgao. TANESCO ilisema Ijumaa iliyopita kuwa muda wa kukaa gizani umeongezeka na kuwa saa saba kwa siku badala ya saa tano za awali.

Jumatatu iliyopita, waandishi wa habari walifurika ukumbi Na. 10 wa Ofisi za Bunge, Dar es Salaam wakitaka kufahamu kinachoendelea kuhusu ufumbuzi wa tatizo la umeme nchini.

Waandishi walikuwa wanakabiliana na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dk. Idris Rashid; Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, William Shellukindo; na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima.

Kwa kuzingatia hali mbaya ya uchumi na usalama, kutokana na mgao wa umeme, hakukuwa na mwenye kiu wala njaa ya kufahamu sababu za kuwepo mgao.

Maswali ya waandishi wa habari yalithibitisha hilo. Yote yalilenga kufahamu hatua zilizoafikiwa kuchukuliwa ili kuliondolea taifa adha ya giza. Hata hivyo, ililazimu wahusika wapate mahali pa kuanzia kwa kueleza kiini cha mgao.

Kuharibika kwa mitambo kwenye vituo vya kuzalisha umeme vya Kihansi, Hale na Songas, pamoja na kupungua kina cha maji katika baadhi ya maeneo ya vyanzo vya umeme, ndizo sababu kubwa mbili za mgao wa umeme zilizotajwa.

Ufumbuzi wa matatizo hayo ulielezwa kuwa ni mitambo husika kukarabatiwa. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika katika muda usiopungua mwezi mmoja. Mtambo mmoja kati ya miwili ya Hale hauwezi kukarabatiwa katika siku za karibuni.

Wakati wa mkutano huo, ilibainishwa kuwa sababu kubwa zaidi siyo kuharibika kwa mitambo ya Hale, kwani hata kama yote ikiwa salama, huwa haifanyi kazi wakati mmoja; hupokezana.

Adam Malima alisema ufumbuzi wa tatizo la Hale ungekuwa kuchimba bwawa la kutunzia maji ya ziada. Hata hivyo, ilielezwa kuwa shughuli hiyo inakabiliwa na changamoto za shughuli za mazingira na za kijamii, mathalani kilimo.

Ufumbuzi mwingine ulitajwa kuwa ni kununua mitambo miwili ambayo mmoja utazalisha megawati 100 kwa ajili ya Dar es Salaam na mwingine megawati 60 kwa ajili ya Mwanza.

Mpango wa ununuzi wa mitambo unaelezwa na Waziri Malima kuwa utachukua miezi 12 kutoka sasa. Kwa hiyo hautaleta ufumbuzi wa haraka.

Ni dhahiri kwamba mwitikio wa waandishi wa habari uliotarajiwa kurejesha taarifa angalau zenye kuleta matumaini ya kumalizika mgao wa umeme siku za karibuni, haukufanikiwa.

Mmoja wa waandishi alimuuliza Dk. Rashid, “Machi mwaka huu ulieleza ulimwengu kupitia kwetu wanahabari, kwamba serikali isiporidhia ununuzi wa mitambo ya DOWANS nchi itakuwa gizani na usilaumiwe.”

Mwandishi alimweleza mkurugenzi kuwa aliyosema sasa yametokea na kuuliza, “Unaweza kufafanua kauli yako ya awali na hali hii ya mgao ili tuweze kuuelimisha umma kuwa mgao unaoendelea nchini siyo hujuma kama ambavyo dhana imejengeka kufuatia kauli yako ya awali?”

Dk. Rashid hakutoa kauli yenye uzito sawa au zaidi ya kauli yake ya awali; badala yake alisema, “Kama kusema nilishasema. Sipendi kuzungumza nisije nikaharibu maelezo mazuri yaliyotolewa na Waziri (Malima) na Mwenyekiti (Shellukindo).”

Mwandishi mwingine aliyekuwa ametembelea vituo vya kuzalishia umeme, kushuhudia hali halisi na kulinganisha hali hiyo na maelezo ya wataalamu wa TANESCO alielekeza swali jingine kwa Dk. Rashid.

Huyu alitaka kujua kwa nini mtambo wa Kihansi uliharibika 7 Septemba mwaka huu kama ilivyo kwa mitambo ya Hale na Songas ambayo pia iliharibika mwezi huohuo na kwa tarehe zinazokaribiana.

Dk. Rashid alisema, “Kama kuharibika, imeharibika; sasa niseme nini? Mitambo huharibika mara nyingi; sema huwa inatengenezwa bila wananchi kufahamishwa, labda kwa sababu huwa hakuna mgao wa umeme kama ilivyo sasa.”

Shellukindo naye aliulizwa iwapo kuna lolote linalohusu mitambo ya Dowans lililojadiliwa na kikao baina ya kamati anayoongoza, uongozi wa TANESCO, viongozi wa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo na viongozi wa wizara husika.

“Mitambo hiyo haikuwa katika hadidu za rejea za kikao,” alijibu Shellukindo na kuongeza, “Kwanza hoja ilishazikwa. Kikubwa serikali iharakishe kupata vyanzo mbadala vya umeme, visivyotegemea maji. Kama tatizo ni taratibu za manunuzi ya mali za serikali, ziharakishwe.”

Kimsingi hadi dakika hiyo hakuna lolote lililoelezwa ambalo liliashiria kuwepo mpango wa kupunguza na kukomesha mgao wa umeme.

Ni mazingira hayo yaliyochochea mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kuibuka na sura nyingine juu ya mgao wa umeme na mitambo ya Dowans, akishauri serikali kuitaifisha mara moja.

Awali, Zitto alithubutu kuwaonya wanasiasa wenzake waliopinga pendekezo la TANESCO kununua mitambo hiyo na kuwataka kutenganisha siasa na mambo mengine yenye maslahi kwa taifa.

Mitambo ya Dowans iko nchini kwa kizuizi cha mahakama kufuatia ombi la TANESCO. Hatua hiyo ilifikiwa na TANESCO baada ya Dowans kuishitaki kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi, Paris, Ufaransa ikilalamikia mkataba wake kuvunjwa kabla muda wake kuisha.

TANESCO ilivunja mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura uliofikiwa mwaka 2006 kutokana na kampuni ya Richmond Development Corporation ambayo haikuwa na fedha wala uwezo kitaaluma na ambayo iliuza mkataba kwa Dowans.

Ilikusudiwa mitambo hiyo itaifishwe endapo mwishoni mwa kesi TANESCO ingeshinda na Dowans kushindwa kuilipa TANESCO gharama ilizotumia kuendesha kesi.

Miongoni mwa sababu za kuvunjwa kwa mkataba huo ni kukiukwa kwa sheria Na. 21 ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka 2004.

Wakati kesi hiyo ikiendelea huku mitambo ikiwa chini ya hati ya zuio la mahakama, pendekezo la kununua mitambo hiyo lilitolewa na TANESCO, jambo lililoibua mjadala mzito uliobeba hisia tofauti.

Kukwama kwa juhudi za kununua mitambo ya Dowans kulitokana na msimamo wa bunge lililokuja na hoja kwamba sheria hairuhusu serikali kununua mitambo iliyokwishatumika au chakavu.

Bali katika serikali kukataa ushauri wa Zitto ulioitaka itaifishe mitambo ya Dowans, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amesema pendekezo lake haliwezi kutekelezwa kwa kuwa serikali “haina utaratibu wa kutaifisha mali” za watu au makampuni binafsi.

Hadi hapo taifa linaendelea kuwa gizani hatua kwa hatua. Lakini rais amesema taifa “halitaingia gizani.” Wananchi wanasubiri hatua za kiongozi mkuu wa nchi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: