Tanesco, Ngeleja na giza


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 15 December 2010

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki
Waziri  wa Nishati na Madini, William Ngeleja

RAIS Jakaya Kikwete amepata kusema "Taifa halitaingia gizani." Naye Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wiki iliyopita amejiapiza, “Serikali italiweka tatizo la mgao wa umeme kwenye kumbukumbu za historia.”

Kauli ya Ngeleja ilikuja siku moja baada ya Shirika la Umeme (TANESCO), kutangaza usitishaji mgao wa umeme nchini.

Ilifuatia kile serikali ilichoita, “Kuongezeka kwa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme; kutengemaa kwa mtambo wa kufua umeme wa Songas; na kukamilika kwa kazi ya ufungaji transfoma mpya katika kituo cha Kipawa, Dar es Salaam.”

Je, nani anaweza kuamini kauli ya Ngeleja kuwa serikali imejizatiti kukabiliana na tatizo la umeme nchini? Iko wapi mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu ya serikali inayoonyesha umakini katika kukabiliana na suala hili?

Kwanza, mgawo wa umeme uliotangazwa kusitishwa na Tanesco wiki iliyopita, si jambo la leo.

Ulianza tokea wizara hiyo ikiongozwa na Jackson Makweta, Dk. William Shija, Jakaya Kikwete, Dk. Abdallah Kigoda, Edgar Maokola Majogo, Daniel Yona, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Kutokana na usugu wa tatizo, baadhi ya wananchi kuna wakati walihoji: Kuna nini kwenye umeme? Mbona kila siku matatizo tu? Wengine waliupachika jina la “mgao wa bandia.”

Hii ni kwa sababu taarifa kutoka ndani ya shirika zilisema, “Kwa vyanzo vya umeme vilivyopo nchini, na kiasi cha fedha ambazo Tanesco inadai wateja wake, kusingekuwa hata na ndoto ya kukosa umeme.”

Aidha, wimbo wa kutokuwepo kwa mgao wa umeme nchini, umeendelea kuimbwa miaka nenda, miaka rudi.

Kwa mfano, kati ya 9 Septemba 2009 na 3 Oktoba 2009, wimbo huu uliimbwa kwa zaidi ya mara kumi na Meneja wa Uhusiano wa shirika hilo, Badra Masoud.

Mara zote hizo msemaji wa Tanesco alisisitiza kuwa hakuna uwezekano wa kuwapo mgao.

Kiherehere cha Badra kilikoma 4 Oktoba 2009, pale aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Tanesco, Dk. Idris Rashid alipotangazia ulimwengu mgao wa umeme kwa kile kilichoitwa, “kupungua kwa maji kwenye mabwawa madogo ya Kihansi na Pangani.”

Sababu nyingine ambayo Dk. Rashid alisema ilisababisha mgao, ni kuharibika kwa mitambo ya kuzalisha umeme ya Songas na Hale.

Badra aliendelea na king’ang’anizi chake cha kutokuwapo mgawo, hadi Oktoba mwaka huu.

Hata pale mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA), ilipotoa tahadhari Septemba 2010 kwamba mikoa 14 iko hatarini kukumbwa na ukame kutokana na kukosekana kwa mvua za vuli, Badra aliendelea kusisitiza kutokuwapo kwa mgawo.

Akizungumza na waandishi wa habari 15 Septemba 2010, Badra alisema, licha ya taifa kukabiliwa na ukame, shirika lake “limejipanga” kuhakikisha hautokei mgawo.

Alitaja mradi wa kuzalisha megawati 160 unaotarajiwa kujengwa jijini Dar es Salaam na mwingine wa Mwanza kuwa ni suluhisho la matatizo yaliyopo.

Hakuishia hapo. Alisema mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi, Nyumba ya Mungu, Mtera na Kidatu yana uwezo wa kuzalisha umeme kwa miezi mitano ijayo.

Wakati huo, Tanesco ilisema kina cha maji katika bwawa la Mtera kilikuwa mita 694.80 juu ya usawa wa bahari.

Pamoja na kwamba taarifa ya Badra haikusema kima cha juu ni mita ngapi katika bwawa la Mtera, lakini inaelezwa kuwa kima cha juu katika bwawa hilo, ni mita 698.50 na kima cha chini kabisa ni mita 690.

Hata hivyo, haikuchukua muda serikali ikatangaza mgawo wa umeme. Tatizo lilianza kwa kuharibika kwa transfoma kubwa ya kuzalisha megawati 45 iliyopo eneo la Kipawa, Dar es Salaam.

Muda si mrefu, mgawo uliongezeka kutokana na kupungua kwa maji yanayoingia kwenye bwawa dogo la kituo cha Kihansi, mkoani Iringa.

Jingine ambalo lilichangia mgawo ni hitilafu za kiufundi kwenye vituo vya New Pangani Falls, Ubungo na Songas.

Kufikia hapo, si Badra, serikali wala Ngeleja waliojitokeza hadharani kueleza lini mgawo utafika ukomo na kuwa “historia.”

Pili, hadi 30 Novemba 2010, mahitaji ya umeme unaongia katika gridi ya taifa yalikuwa megawati 865. Uzalishaji wa umeme nchini hauzidi megawati 985.

Ukichanganya na mikoa ambayo haijaunganishwa na gridi ya taifa, mahitaji yanaongezeka hadi kufikia megawati 906.

Sasa kama mahitaji ni hayo na uzalishaji ni huo, Ngeleja anapata wapi ujasiri wa kujiapiza kuwa “mgawo utakuwa historia?”

Nini kinamhakikishia kutokuwapo mgawo wakati mashine zinaweza kuharibika, au ina cha maji kupungua kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme?

Tatu, tangu kuondoka kwa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, serikali haijawekeza vya kutosha katika eneo hili.

Miradi mikubwa minne iliyopo sasa – Kidatu wenye uwezo wa kuzalisha megawati 204, Mtera (megawati 80), Hale (megawati 21) na Nyumba ya Mungu (megawati 8), yote ilijengwa wakati wa utawala wa Nyerere.

Katika kipindi hicho pekee cha Nyerere, uzalishaji ulizidi mahitaji. Hata pale hitilafu zilipotokea, serikali haraka iliweza kukabiliana na tatizo kwa kuwa kulikuwa na vyanzo vya uhakika vya umeme.

Tawala mbili zilizofuata baada ya Nyerere kuondoka madarakani – Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, hazikujishughulisha kuwekeza katika miradi iliyoachwa na Nyerere.

Badala yake, serikali ilijikita katika “miradi ya chapuchapu” ya umeme wa dharula.

Kwa mfano, katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Mwinyi na 10 ya utawala wa Mkapa, serikali iliwekeza katika ujenzi wa miradi ya umeme katika vituo miwili tu:

Kituo cha kuzalisha umeme cha Kihansi ambacho kina uwezo wa kuzalisha megawati 180 na New Pangani kinachozalisha megawati 68.

Lakini Mwinyi na Mkapa wataendelea kukumbukwa katika taifa hili, ingawa kila mmoja na lwake.

Mtambo wa IPTL unaotumia mafuta ya dizeli; una uwezo wa kuzalisha megawati 100.

Wakati Mwinyi atakumbukwa kwa kuingiza nchi katika mkataba tata na wa kinyonyaji kati ya serikali na kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Mkapa  hatasahauliwa kwa hatua yake ya kuingiza taifa katika mkataba wa Songas.

Mradi wa Songas unazalisha megawati 180. Mikataba hiyo miwili kila mmoja unalamikiwa na wananchi kuwa unatafuna rasilimali za taifa.

Si hivyo tu. Mkapa atakumbukwa pia kwa hatua yake ya kuichukua Tanesco na kuikabidhi kwa kampuni ya kigeni kutoka Afrika Kusini, Net Group Solution.

Katika kipindi chote ambacho Tanesco ilikabidhiwa kampuni ya kigeni, shirika hilo lilishindwa kujenga hata mradi mmoja wa umeme.

Naye Kikwete, mbali na kukamilisha mradi wa Ubungo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 na kituo cha umeme kinachotumia gesi cha Tegeta (MW 45), atakumbukwa kwa kuingiza taifa katika mradi mchafu wa Richmond/Dowans, mwaka 2006.

Tayari serikali inatakiwa kulipa kampuni ya Dowans, ambayo haijulikani mmiliki wake, Sh. 185 bilioni kutokana na hatua yake ya kuvunja mkataba.

Pamoja na kwamba serikali inajua kuwa miradi ya aina hii si endelevu; ni ghali kuileta nchini; na hubebwa na kipengele cha “Capacity Charge” – gharama za kuweka mitambo hata bila kuitumia –  lakini bado iliendelea kuing’ang’ania.

Kibaya zaidi, aliyeingiza nchi katika mradi huu (Kikwete), ndiye aliyekuwa waziri wa nishati na madini wakati Tanesco inafunga mkataba na IPTL.

Uzoefu unaonyesha kuwa miradi inayotekelezwa kwa utaratibu huu, imekuwa ikisababisha mzigo mkubwa kwa taifa na watumiaji wa umeme kwa jumla.

Mara kwa mara, mikataba hii huilazimisha Tanesco kupandisha bei ya umeme ili kukidhi gharama za uendeshaji.

Nne, serikali haina mpango wowote endelevu na unaotekelezeka wa kuzuia kuwapo mgawo.

Badala yake, Tanesco na hasa serikali imejikita katika miradi ya umeme iliyojivisha kilemba cha “umeme wa dharula.”

Hakuna anayezungumzia, kwa mfano, mpango wa kutumia wawekezaji binafsi wa ndani kuzalisha umeme. Tayari kuna taarifa kuwa zaidi ya megawati 100 zinaweza kupatikana kupitia mradi wa umeme wa upepo.

Kilichokwamisha mradi huo ni serikali kushindwa kufunga mkataba na wawekezaji waliojitokeza.

Mradi wa aina hiyo unaweza kutekelezwa katika kijijiji cha Kititimo, mkoani Singida, Makambako, mkoani Iringa, Mgagao, wilayani Mwanga, Katesh wilayani Mbulu, Karatu mkoani Arusha na Usevya, mkoani Rukwa.

Pamoja na Shirila la Maendeleo la Denmark (DANIDA) kukubali kutoa fedha kufadhili miradi hii, serikali imeendelea kukalia mapendekezo ya wawekezaji wa ndani.

Ziko wapi juhudi za serikali za kuhakikisha kampuni ya Urusi (BORODINO) ambayo inasemekana kuwa ipo tayari kujenga kituo cha umeme wa nguvu ya maji eneo la Rumakali (MW 222)?

Aidha, zipo wapi juhudi za serikali kuleta miradi ya Stigler’s Gorge, Mchuchuma, Rusumo na Ruhudji ambayo inaonekana katika kile kinachoitwa, “Power Sector Master Plan” – mpango kamambe wa muda mrefu wa sekta ya umeme?

Mpaka pale Ngeleja atakaposema, ni miradi ipi itakayotekelezwa na wakati gani, ili kuongeza ziada ya umeme, ndipo umma unaweza kukubaliana naye kuwa “mgawo utakuwa historia.”

Bila kuyafanya haya, ni vema Ngeleja akanyamaza. Au kama anataka kusema, basi aeleze ukweli, kwamba chini ya utawala wa sasa uliochoka, ulioishiwa mbinu za uendeshaji wa shirika na uliokumbatia watuhumiwa wa ufisadi katika sekta ya umeme, mgao hauwezi kuepukika.

Kama Ngeleja na wenzake hawajaeleza nani mmiliki wa Dowans/Richmond, hawezi kusema atamaliza tatizo lililopo.

Aeleze mgawo utaendelea kila baada ya mashine moja kuharibika, au bwawa  kukauka.  

Aseme bila kutafuna maneno kuwa hata katika hili la kujaa kwa mabwawa ya kuzalisha umeme, Tanesco haijasema ukweli.

Kwamba hadi 10 Desemba 2010, kima cha maji katika bwawa la Mtera kilikuwa mita 692.70 usawa wa bahari. Kila siku shirika lake linatumia sentimeta 2 hadi 3 za maji hayo kuzalishia umeme.

Kutokana na hali hiyo, uwezekano wa maji hayo kukauka iwapo mvua hazitaendelea kunyesha ni mkubwa.

Ni vema Ngeleja akajitazama kwanza kabla ya kuahidi kumaliza tatizo la uhaba wa umeme.

Wananchi bado wanakumbuka kauli yake bungeni kwamba kabla ya mwaka wa fedha wa 2000/2010, serikali ingekamilisha mradi wa umeme wa megawati 160 utakaojengwa Ubungo, Dar es Salaam na megawati 60 mkoani Mwanza.

Hata katika bajeti ya mwaka 2010/2011, Ngeleja alirejea kauli hiyo. Alisema mtambo wa Dar es Salaam utatumia gesi, huku ule wa Mwanza ukitumia mafuta mazito.

Mpaka sasa, mitambo hiyo haijajengwa na Ngeleja hajaeleza kilichosababisha hilo kutofanyika. Je, mbona hili hataki kulieleza, badala yake anakuja na hadithi mpya?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: