Tanganyika ‘yaibuka’ kinyemela


Josephat Isango's picture

Na Josephat Isango - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version

MICHUANO ya Chalenji inayoshirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati ambayo ina fanyika nchini mwaka huu, imenisukuma kwenye jambo moja kubwa.

Nalo ni hili: Kumbe inawezekana kuwapo serikali mbili ndani ya Jamhuri ya Muungano?

Ni kwa sababu ya ushiriki wa timu ya taifa ya Kilimanjaro Stars,  katika mashindano haya.

Nijuavyo mimi, hakuna taifa linaloitwa Tanzania Bara. Kuna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndani ya Tanzania kuna Zanzibar, ambayo kwa mujibu wa katiba ya sasa ya visiwani, hiyo ni nchi kamili.

Serikali ya Zanzibar ina jeshi lake - Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Chuo cha Mafunzo (Magereza), Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Zimamoto na Valantia.

Ndani ya katiba, Zanzibar imejieleza vema kuwa inaye rais ambaye ni kiongozi wa majeshi hayo.

Kwa sasa, kiongozi huyo ni Dk. Mohamedi Shein.

Rais wa Zanzibar anaweza kuamua jambo lolote kuhusu idara hiyo, bila kumshirikisha rais wa Muungano na bila kuhitaji kibali chake.

Katika mashindano haya, Kilimanjaro Stars inashiriki kama mwakilishi kutoka nchi ya Tanzania Bara.

Lakini iko wapi serikali ya Tanzania Bara? Yuko wapi rais wa Tanzania Bara? Yuko wapi rais wake? Yuko wapi waziri mkuu wake?

Nijuavyo mimi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, ni Jakaya Kikwete. Waziri wake mkuu, ni Mizengo Pinda.

Wakati Zanzibar wana wimbo wao wa taifa, bendera yao yenye rangi za bluu, nyeusi, Kijani na Njano, Tanzania Bara haina bendera, haina wimbo wala haina mtawala.

Katika mazingira haya, tunaishi ndani ya serikali tatu, lakini tunahubiri serikali Mbili!

Kwa mtazamo huo, Rais Jakaya Kikwete analo jukumu zito la kuhakikisha unapatikana Muungano wenye usawa na unaoridhiwa na pande zote mbili.

Kwa mfano, kama Zanzibar wanaweza kuwa na serikali yao, jeshi lao, rais wao, kwa nini Tanzania Bara nao wasiwe na utawala wao?

Kama Zanzibar inaingia kwenye baraza la mawaziri la Bara, kwa nini bara wasiingie kwenye baraza la mawaziri la Zanzibar?

Je, uhalali huu wa upande mmoja utatokana na nini?

Matatizo ya Muungano ni mengi. Hili la mashindano ya Cecafa, pamoja na ile inayoandaliwa na shirikisho la mpira la Afrika (CAF), ni sehemu tu ya kile kinacholalamikiwa.

Mathalani, wakati raia wa Zanzibar wanaruhusiwa kugombea uongozi kwenye Jamhuri ya Muungano na kuchagua viongozi wake, raia wa Jamhuri ya Muungano hawaruhusiwi kuchagua viongozi kutoka Zanzibar.

Aidha, kwa mujibu wa Katiba ya Muungano, masuala yote yanayohusu Muungano kama vile Katiba ya Tanzania yamekasimiwa kwa vyombo vya uwakilishi vya serikali ya Muungano yaani Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Lakini Baraza la Wawakilishi Zanzibar, lina mamlaka ya kutunga sheria katika Zanzibar, “... juu ya mambo yote yasiyo mambo ya Muungano...”

Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Muungano, Bunge la Jamhuri linawakishwa na asilimia 23.5 ya wabunge kutoka Zanzibar.

Kimsingi yote haya yanaweza kurekebishwa iwapo viongozi waliopewa dhamana watasukumwa na utashi wa ksiasa na uelewa mpana juu ya hatari inayoweza kutokea, iwapo haya yataendelea kufunikwa.

Mwandishi wa makala hii, Josephat Isango amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anapatikana kwa simu Na. 0786-426414.
0
No votes yet