Tanzania bila Kikwete inawezekana


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

KISWAHILI kina hazina kubwa ya misemo na methali kwa ajili ya kuonya, kuelimisha, kuadilisha, kuadabisha na hata kuiburudisha jamii.

Methali ni kongwe hakuna, miongoni mwa watumiaji wa sasa, ambaye anaweza kutamba kwamba amebuni methali fulani au msemo fulani. Ndiyo maana watumiaji huanza kwa kusema, “wahenga walisema…”

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekamata methali moja na kuishikilia kwa nguvu zote kwa vile inawatia ujinga wananchi ili kiendelee kutawala.

Usalama wao ni katika methali hiyo isemayo, “Alalaye usimwamushe, ukimwamsha utalala wewe” au msemo, “Wajinga ndio waliwao”.

CCM wanajua madhara ya kuwapa wananchi elimu ya uraia ili wajue haki zao, matumizi ya raslimali ya nchi yao, wajibu wao kwa taifa na wizi mkubwa unaofanywa na viongozi wa serikali yao. Wanataka wabaki wajinga maana wajinga ndio waliwao.

CCM inataka wananchi wabaki washangiliaji na kuimba nyimbo zisizo na tija wakati viongozi wanahujumu uchumi kwa ushirikiano na wafanyabiashara.

CCM inataka wabaki walalamikaji wa uporwaji wa mali na viwanja vyao, wabaki wakilishwa uongo na ahadi zisizotekelezeka maana wakiwaamsha watalala wao.

Kampeni zao ni za uongo. Mei mwaka jana ulifanyika uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Busanda wilayani Geita, kujaza nafasi iliyoachwa na Mbunge, Faustin Lwilomba.

Katikati ya kampeni, CCM ikiwa imeelemewa, ilifanya usanii. Ikashinikiza serikali ipeleke ‘migogo’ ikisema inatekeleza ahadi za kupeleka umeme katika jimbo hilo kama ilivyoahidi mwaka 2005.

Safari hii, mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete alisahau kuwa watu wake waliahidi uongo, alipoenda Geita alilzimika kumwita Waziri wa Madini na Nishati, William Ngeleja afanye usanii tena—wakazomewa.

Kila mmoja wenu atakuwa anakumbuka tukio baya la kuvamiwa ofisini na kushambuliwa vibaya Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Halihalisi, Saed Kubenea, na Mhariri mshauri wa taaluma, Ndimara Tegambwage.

Rais Jakaya Kikwete alimtembelea Kubenea hospitalini Muhimbili alikokuwa amelazwa na akaahidi kumlipia gharama za matibabu ya nje.

We! Alisubiri, akasubiri weeeeee, alipokaribia ‘kuozea’ Muhimbili akisubiri mteremko wa matibabu, muuguzi mmoja akamshauri atafute pesa aende India kwani, aliona dalili za ahadi hiyo kutotekelezeka.

Ndivyo ilivyotokea, ahadi haikujatekelezeka badala yake alitafuta pesa kutoka kwa marafiki na wasamaria wema akaenda India ambako alilazwa kwa matibabu na bado anakwenda huko kila baada ya miezi kadhaa kufanyiwa uchunguzi.

Si hivyo tu, JK aliahidi kuua mchwa unaokula pesa za umma kwenye halmashauri, lakini ni kinyume chake, umeshamiri na umejenga siyo vichuguu bali mahekalu ya ajabu.

Nenda wilaya za Korogwe, Lushoto na Muheza waulize kama wametekelezewa ahadi ya kujengewa kiwanda cha matunda. Usanii mtupu!

CCM haitaki haya yaanikwe kwa sababu yatawaamsha wananchi na wakierevuka CCM watalala na kutoweka katika ulingo wa siasa.

CCM hawataki kusikia vyama vya upinzani vikihubiri ukombozi wa nchi kutoka kwenye ukoloni wa chama tawala, hawataki kusikia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikiwataja wazi wezi wa mali za umma.

Vilevile hawataki wananchi wasikie ufunuo wa Chama cha Wananchi (CUF) kwamba, katika miaka mitano iliyopita, viongozi wa serikali wametafuna Sh trilioni 11 takriban sawa na bajeti ya mwaka huu.

Serikali ya CCM inafanana sana na serikali ya nchi ya Kusadikika, kitabu kilichotungwa na mwandishi mahiri, hayati Shaaban Robert.

Katika riwaya hiyo Shaaban Robert aliweka wazi ubaya wa serikali hiyo chini ya Mfalme Jeta na Waziri mkuu, Majivuno.

Mtunzi huyo mahiri wa riwaya nyingine za ‘Kufikirika’, ‘Utu bora mkulima’, ‘Maisha yangu baada ya miaka 50’, alisema Mfalme Jeta alikuwa anakula kila kitu tena bila kusaza na hashibi—maji ya mito na bahari yalimiminika kinywani lakini alijisikia kiu, alitafuna miamba, miti, wanyama na samaki lakini alijisikia njaa.

Shaaban Robert alikusudia kuisema serikali ya kikoloni iliyokuwa inachota raslimali za nchi kama vile mito (samaki), bahari (mafuta), miamba (madini), hewa (gesi), miti (mbao), wanyama (vipusa) na kuiacha nchi maskini.

Shaaban Robert anaeleza namna wajumbe sita jasiri (wana mapinduzi) walivyosafiri nchi za mbali kuchota ujuzi na kurudi nao Kusadikika.

Kila mjumbe alitumwa na serikali kupeleleza(kusoma) jamii za nchi nyingine zilizokuwako ng’ambo ya mipaka yao, ili wawaletee Wasadikika mawazo mapya yenye kufaa kutoka kwa mataifa yaliyofanikiwa kimaendeleo.

Miongoni mwa mashujaa hao ni Karama aliyesimulia hila, uonevu, manyanyaso waliyopata wenzake watano na kufungwa. Wajumbe wote walikuwa watu wenye uhodari, ujasiri, na vipawa vingi na walijitolea ili walihudumie taifa lao kwa kadiri walivyoweza na wawe mashujaa halisi wa nchi yao ya Kusadikika.

Mashujaa hao walikuwa Buruhani, Fadhili, Kabuli, Auni, Ridhaa, na Amini (ambao leo wanaweza kuwa kina Augustine Mrema, Prof Ibrahim Lipumba, Seif Sharrif Hamad, Freeman Mbowe, Dk Sengodo Mvungi). Walivumilia majaribio mengi wakisafiri katika nchi ngeni, na wakarejea Kusadikika na mbinu nzuri kutoka nchi walizozitembelea.

Lakini licha ya habari nzuri waliyowaletea Wasadikika, walishtakiwa kila mara kwa ajili ya mawazo mageni haya, na kufungwa mpaka sasa, yaani wakati wa hukumu ya Karama.

Sababu kubwa ni kwamba watu wa serikali waliogopa kubadilisha desturi zao na kujifunza kutoka kwa jamii nyingine (upinzani). Baada ya mfalme na wanabaraza kusikia maelezo ya Karama, waliupata ufahamu mpya wa hali ilivyokuwa. Mabadiliko yalifanywa na wajumbe wote wakafunguliwa.

Tanzania ya leo ina mashujaa kama Dk Willibrod Slaa wa CHADEMA na Prof Ibrahim Lipumba wa CUF ambao wanapita nchi nzima kueleza udhalimu wa Serikali ya CCM.

Dk. Slaa na Prof Lipumba wanawaambia wananchi “amkeni”, CCM wanakula nchi bila kusaza kama Mfalme Jeta kwa njia ya mikataba mibovu ya madini—tanzanite Mererani, dhahabu Bulyanhulu, Buzwagi na Nyamongo (North Mara). Walivyonenepa kutokana na rushwa ya rada na ndege na wanavyochukua posho mbili kwa kazi moja.

Wanasema amkeni mshuhudie walivyojigawia migodi ya Kiwira, Meremeta na walivyoingiza dude Richmond/ Dowans ambalo liliruhusiwa kufyonza Sh 152,000,000 kwa siku.

Prof Lipumba na Dk. Slaa wanawaambia mmepuuzwa na CCM kiasi cha kutosha, mmenyanyaswa kiasi cha kutosha, mmeonewa kiasi cha kutosha, unyonge wenu ndio uliofanya muonewe, mnyanyaswe, na mpuuzwe.

Sasa wanataka mapinduzi, mapinduzi yatakayowaondoa katika kuonewa, kupuuzwa na kunyanyaswa na mkoloni mzalendo CCM.

Kama Tanzania imewezakana bila mwasisi wa taifa Mwalimu Nyerere, inawezekana pia bila CCM na bila Kikwete.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: