Tanzania kugeuzwa kinara wa ukoloni mamboleo!


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 30 September 2008

Printer-friendly version

KUNA ukweli katika usemi kwamba, “historia hujirudia.” Ukweli huu unajidhihirisha leo ambapo Afrika inanyemelewa na ukoloni mpya kwa njia na kwa mtindo ule ule uliotumika karne ya 19 zilizopita.

Tunauliza, wana nia gani mabeberu wanapotoka nje ya nchi zao kuteka na kuitawala dunia?

Kwa mfano, kitu gani kilichowafanya wakoloni wakongwe miaka 124 iliyopita (1884), wakae meza moja mjini Berlin kuigawa Afrika? Je, kuna mfanano wowote kati ya wakoloni wa kale na wakoloni wapya?.

Je, kuna kitu kinachoitwa ukoloni mpya (neo-colonialism), au ni kitu tu cha kutunga ndani ya mawazo yetu? Na kama kipo, kina tofauti gani na ukoloni mkongwe?

Je, mababu zetu waliotia sahihi mikataba ya kilaghai miaka 124 iliyopita na kuigawa Afrika hatua kwa hatua, chini ya himaya ya  wakoloni, walielewa walichokuwa wakifanya na athari zake kwa vizazi  vijavyo? Tunajifunza nini kutokana na ujinga au hekima zao kwa hilo?

Septembe 2007, tulikaribisha nchini meli ndogo ya kivita ya Marekani, yenye urefu wa futi 509, iliyobeba silaha za misaili zilizotumika katika vita vya Ghuba miaka ya 1990. 

Meli ilibeba mabaharia (askari!) 280 na makomandoo 20 ambao walifanya shughuli za kijeshi pamoja na askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).

Kabla ya hapo kulikuwa na taarifa kwamba Marekani ilikusudia kuanzisha barani Afrika ngome kuu ya kijeshi ya ulinzi (American African High Command-  AFRICOM ifikapo Desemba 2008 au baada ya hapo.

AFRICOM ilibuniwa mwaka 2006 na aliyekuwa Waziri wa ulinzi wa Marekani, Donald Rumsfeld kwa kile kinachoitwa kuisaidia Afrika “kuimarika kiusalama kwa njia ya utawala bora, utawala wa sheria na kutoa fursa ya maendeleo ya kiuchumi, biashara na uwekezaji”

Moja ya shughuli za AFRICOM imeelezwa,  kuwa ni kupambana na vitendo vya kigaidi katika ukanda wa Afrika ambapo Marekani imesema “nchi zingine itabidi zitangaze” kama ziko upande wa Marekani au Magaidi”.

Ziara ya meli hiyo ya kivita ilifuatiwa na ziara ya siku nne ya Rais wa Marekani, George Bush nchini Februari 16 – 19 mwaka huu. Hiyo ilikuwa ni ziara ndefu kuliko zote  zilizowahi kufanywa na rais yeyote wa taifa hilo kwa nchi moja.

Katika ziara hiyo, Bush alitoa msaada wa dola 800 milioni kwa ajili ya kupambana na janga la UKIMWI.

Naye Waziri wa mambo ya nje, Condoleeza Rice Julai 2007, aliwahi kumwalika Rais Amando Guebuza wa Msumbiji nchini mwake na kumwahidi msaada wa dola 500 milioni ili aruhusu vituo vya kijeshi nchini mwake.

Nchi zingine zilizoonesha nia ya kuruhusu AFRICOM ni pamoja na Benin, Liberia, Uganda na Rwanda.  Wakati huo huo,  Marekani inaimarisha vituo vya Manowari katika Bahari ya Mediterania hadi Bahari ya Pacifiki Magharibi, kukabiliana na wanachokiita “mapigo kutoka mataifa korofi”.

Wakati huo pia inakamilisha ujenzi wa mtambo mkubwa wa Nyuklia huko Alaska; na mwingine wa silaha kali za anga (space to space Lasser weapons), kwa hofu kwamba huenda “mataifa korofi” yaweza kuzipiku na kuziharibu Setelaiti zake zaidi ya 185 angani ifikapo mwaka 2010. 

Mataifa hayo korofi yanatajwa kuwa ni pamoja na Urusi, Pakistani, Iran, India, Korea Kaskazini na China.

Kwa kufurahia ziara yake hapa nchini, Bush aliwaita Watanzania pamoja na Rais Jakaya Kikwete kuwa ni “rafiki mkubwa wa kweli wa Marekani.”  

Tayari Kikwete ametembelea Marekani mara saba, na kuvunja rekodi ya Marais duniani kutembelea taifa hilo kubwa kwa kipindi kifupi kama hicho.

Kuna tofauti gani kati ya urafiki wa Bush na viongozi wa Kiafrika sasa,  na urafiki kati ya waasisi wa ukoloni barani Afrika, kina Carl Peters, Cecil Rhodes, George Goldie na wengine,  dhidi ya watemi kama kina Mangungo, Lobengula na wengineo, waliopokonywa uhuru na nchi zao kwa mikataba ya kilaghai? 

Je, usawa uko wapi kati ya viongozi hao “marafiki wa kweli” na Marekani?.

Ujio wa Rais Bill Clinton mwaka 2000, alipohudhuria kikao mjini Arusha cha kutiwa sahihi mkataba wa amani na makundi hasama ya Burundi, ulitanguliwa na ujumbe wa mashushuu kutoka Marekani  mwezi mmoja kabla.

Lakini safari ya rais Kikwete Marekani haitanguliwi na mashushuu. Sasa kwa nini hilo halifanyiki kama wote wako sawa?.

Rais Clinton alipokuwa Arusha, shughuli zote za usalama zilifanywa na wanausalama wa Kimarekani na mawasiliano yote yalikatika.

Si hivyo tu, gari la Rais Mkapa lilipekuliwa na mbwa wa Marekani alipokwenda kumpokea uwanja wa ndege wa KIA. 

Na wakati wa mkutano, walinzi wote wa Marais wa Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda waliohudhuria, hawakuruhusiwa kuingia.  Na vivyo hivyo ilivyokuwa wakati wa ziara ya Bush hapa nchini; akiwa Dar es Salaam na Arusha.

Juni 2008, Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Leon Sullivan kama jukwaa la Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, wakiongozwa na aliyewahi kuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Andrew Young. 

Serikali iligharamia mkutano huo kwa Sh. 2.5 bilioni ili  kuitangaza nchi kwa wawekezaji kutoka nje.

Ikumbukwe kwamba familia ya George W. Bush na Andrew Young mwenyewe  zina hisa katika Makampuni yanayochimba dhahabu hapa nchini, hususan kampuni ya  Barrick. 

Utafiti umeonesha pia kuwa, nchi yetu ina akiba kubwa ya aina mbali mbali za madini (ikiwamo Uranium safi) na mafuta. 

Je, msaada wa Marekani wa dola 800 milioni ni kitu gani kwa uvunaji na uporaji rasilimali usiodhibitiwa ambao unafanywa na wawekezaji? Iko  wapi tofauti, kati yetu na Machifu Mangungo na Lobengula?.

Tunafahamu kwamba, migogoro ya kiuchumi ya karne ya 19 ilisababisha kujitanua kwa ubwanyenye wa Ulaya.

Kwa sababu hii, sera za nje na udubwana wa Marekani unapambana na changamoto kubwa kutoka kwa wavuja jasho wa dunia hii –ambayo Marekani inauita ugaidi, ambapo kwa ubabe huo imeangusha serikali katika nchi 100 na imevamia 59.

Katika kipindi cha miaka kumi kile kinachoitwa ugaidi ni kisingizio tu, tishio kubwa la Marekani ni maasi ya mataifa  dhidi ya uonevu na ukoloni mamboleo ukiongozwa na Marekani.

Urafiki wa Marekani na Afrika na kuanzishwa kwa AFRICOM, una lengo la kuihakikishia Marekani maeneo ya ushawishi ( sphere of enfluence)  dhidi ya mataifa mengine katika zoezi la kuigawana Afrika, hata kama italazimu kutumia  nguvu za kijeshi,  kama ilivyofanya Iraq.

Kuna sababu kuu mbili: Moja,  kupora utajiri wa nchi hizi, hasa mafuta na madini. Pili, ni kupambana na ugaidi ambao kusema kweli ni upinzani wa umma dhidi ya kutawaliwa na wageni

Tuna kila sababu ya kujiuliza, kwa nini nchi yetu imegeuka kuwa kipenzi cha Marekani, kuliko huko nyuma, ilipoongoza harakati za mapambano ya wanyonge wa dunia ya tatu?

Kwa hili, viongozi wetu wanapaswa kujibu, wakielewa kwamba dunia ya wanyonge na  wanaoonewa inawaangalia kwa macho makavu.

0
No votes yet