Tanzania: Nchi moja, ma-rais wawili


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 10 November 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Rais Jakaya Kikwete

JAKAYA Mrisho Kikwete amewataka waandishi wa habari kusaidia kuponya majeraha “yaliyotokana na uchaguzi mkuu.”

Wito huo unatoka kwa anayeendelea kukaa ikulu kwa miaka mitano mingine, lakini kwa ushindi wa utata; huku mpinzani wake mkuu, Dk. Willibrod Slaa akirejea kwenye ngome ya shina la chama chake.

Bali ni wito unaotoka kwa anayeonekana kukiri kuwa kuna utata; kuna mgogoro; kuna hasira zinazofura mithili ya mawimbi ya bahari wakati wa upepo mkali; lakini pia kuna jicho lililoona na linalosuta.

Kuponya majeraha ni kupatanisha; ni kusuluhisha; ni kufuta nyayo za uchafu. Ni kuleta maafikiano na kuondoa tuhuma, lawama na hata kuleta fidia kwa wahusika na kusema yaishe.

Je, hicho ndicho Kikwete anataka? Kama ndicho, yuko wapi mwandishi wa habari wa Tanzania mwenye uwezo wa kusuluhisha katika hili? Naomba kuwasilisha kuwa, hayupo.

Kwa jinsi kampeni zilivyoendeshwa na jinsi uchaguzi ulivyofanywa, kuna kila sababu kwa Kikwete kutaka msaada katika kuleta suluhu. Lakini asitegemee msaada huo kutoka kwa waandishi wa habari.

Upatanishi anaotaka Kikwete ni kwamba Dk. Slaa anyamaze. Asilalamike. Hata akilalamika sauti isiwe kubwa. Hata ikiwa kubwa isiende mbali kiasi cha kuvuka mipaka ya nchi.

Anataka hata sauti ya Dk. Slaa ikivuka mipaka, basi isibebe maudhui makali yanayotaka uchaguzi urudiwe au kupeleka mashitaka mbele ya umma wa Tanzania.

Hayo yakifanyika – Dk. Slaa akikubaliana na haya – maana yake ni kwamba wawili hawa – Kikwete na Slaa – watakuwa wanatawala pamoja; mmoja yuko ikulu na mwingine yuko nje anapoza umma ili usilipuke.

Tutake tusitake, hivi ndivyo watawala wangetaka. Dk. Slaa asilalamikie kuibwa kwa kura; asidai uchaguzi kurudiwa; asiandae wananchi kuingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi uliomrejesha Kikwete ikulu.

Hivyo ndivyo wangetaka wale walioingia ikulu; kwamba Dk. Slaa akae kimya. Asionyeshe hata ushahidi wa mgongano wa taarifa za vituoni na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kikwete anataka kutawala na Dk. Slaa lakini kimyakimya – bila kumtangaza; kwani ukimya wake ndio pekee unaoweza kumpa usingizi yule bwana aliyeingizwa ikulu bila kishindo alichokuwa ameahidi.

Hoja hapa ni kutaka isifahamike nani chanzo cha kutishia wananchi kuwa upinzani ukishinda kutakuwa na vita na mauaji kama Rwanda na Burundi.

Hoja ni kutaka kuficha mdororo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliosababisha serikali kuhaha katika kukitetea, hata kusababisha viongozi wakuu jeshini kutoa taarifa ambazo hazikuwa za lazima.

Woga uliosambazwa miongoni mwa wananchi; uchochezi ulioingizwa majeshini kwamba CHADEMA wanataka kuleta vurugu; ni mambo ambayo watawala wasingependa Dk. Slaa ayaweke wazi ili wananchi waweze kutoa hukumu.

Iwapo Dk. Slaa atasema, hataweza kuacha kujadili nafasi ya askari mdogo wa polisi au jeshi ambaye alimpigia kura na ambaye anakiri kuwa naye anataka mabadiliko.

Hatasita kujadili wafanyakazi wa kawaida na maofisa wa ngazi za chini katika Usalama wa Taifa ambao wanaona ukombozi katika utawala mpya nje ya kwapa la CCM.

Hataogopa kuonyesha ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wachache wa ngazi za juu ndani ya majeshi na baadhi ya viongozi wa serikali katika kukuza lawama, tuhuma na vitisho.

Lakini kubwa zaidi, Dk. Slaa hatasita kueleza jinsi vitisho, vilivyobuniwa na serikali, CCM na baadhi ya viongozi wa majeshi, vilivyoweza kufanya baadhi ya wapigakura kusita kwenda vituoni.

Rais anajua kuwa waandishi wa habari hawawezi kumsaidia katika hili; hata wakijipinda kama nane na kutumia misamiati yote ya kazi waliyojifunzia ndani au nje ya darasa.

Waandishi hawawezi kusaidia lolote labda kukataa kuandika kile ambacho Dk. Slaa atasema. Kwa mfano, juu ya matumizi ya mabavu.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya uchaguzi nchini (Tanzania bara), kila palipotarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kwa mgombea wa CCM, walimwagwa askari wengi.

Mara hii pia, askari walikuwa na mavazi yenye mafundo na pingili kiasi cha kufanana na nzige anayetaka kuruka: sura za kuogofya na zilizozungushwa mijini ili kupenyeza hofu.

Ni hivi: Watoto wa wakulima na wafanyakazi maskini ndio walio katika magwanda; wanatamani mabadiliko pia katika maeneo yao ya kazi na wangependa wazazi wao wapumue na kutembea kifua mbele katika maisha bora.

Yote haya Dk. Slaa atayasema. Ayaache kwa gharama gani? Kwa mapatano gani? Kwa CCM kujisalimisha kwake?

Dk. Slaa anajua vema kuwa NEC ni tume ya rais. Nani atasuluhisha wananchi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo kwa miaka mitano, imeshindwa kufanya maandalizi ya kupiga kura?

Tume ambayo haijui nani waliuokufa na nani wako hai? Haijui wala kujali umbali wa vituo kutoka makazi ya wapigakura. Haijui idadi kamili ya walioijiandikisha bali inabakia kutoa takwimu zinazosigana kila kukicha.

Nani atasuluhisha wananchi na Tume ambayo wasimamizi wake majimboni ni watumishi wa serikali wanaotishiwa kuwa iwapo wagombea wa CCM hawatashinda, basi “watakiona kilichomnyoa kanga manyoya shingoni?”

Kama kuponya majeraha ni kupatanisha; ni kusuluhisha na kuleta maafikiano, nani atasuluhisha wananchi na tume inayotoa tarakimu zinazosigana?

Nani atapatanisha walioshindwa kupiga kura kutokana na uzembe wa tume ya uchaguzi ya rais?

Nani atapatanisha wananchi na waliokuwa wakipita nyumba hadi nyumba; wakinukuu namba za shahada za kupigia kura?

Au wale walionunua shahada za wengine au kutembea na chupa ya wino ili kila anayetosa kidole mtaani na kuonyesha kuwa amepiga kura tayari, basi apewe Sh. 2,000 au Sh. 3,000?

Chama gani kilikuwa kinafanya hayo na kwa faida ya nani, ni mambo ambayo Dk. Slaa anaweza kuwa na ushahidi nao na kuweka wazi. Nani atapatanisha wananchi na ghiliba na wizi huo?

Nani mwenye uwezo wa kupatanisha wema na uovu? Yuko wapi? Waandishi wa habari ambao rais anaomba washiriki kuponya majeraha, wanaweza kuwa hoi kuliko anavyofikiria.

Siyo rahisi basi kuponya “majeraha” yaliyofikisha wawili ikulu na wengi wengine bungeni.

Kuna njia mbili za kuchukua. Kwanza, rais aliyeko ikulu kuona na kukubali kinacholalamikiwa na kufanya marekebisho; au kuendelea na shughuli zake kana kwamba hakuna kilichotendeka.

Pili, rais aliyeko nyoyoni mwa wengine, Dk. Slaa kuandaa shinikizo la mabadiliko, hatua ambayo inaweza kuwa ghali kwake na wananchi; au kuanza upya kukata mbuga, akijiimarisha kuanzia mashina hadi taifa na kujiweka tayari kwa ushindi miaka mitano ijayo.

Katika hatua ya pili kwa upande wa Dk. Slaa, ndipo pana utamu: Kuwaeleza wananchi kwa mapana kuwa kama ni fujo, machafuko na hata vita, wenye uwezo wa kuleta vita ni watawala wasiotaka kukubali kushindwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: