Tanzania sasa nchi ya kuteka, kutesa


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version

ULIMWENGU unayugayuga. Nchi inayawayawa kama machela. Dunia hii inanitisha! Niende wapi nifarijike? Ninatembea kidogokidogo nikinyatanyata nikitamani kuunyakua uzima wa milele! Ee Mungu Baba nishike mkono, Ulimwengu huu utanipeleka wapi?

Dk. Steven Ulimboka sasa wewe kufa tu, ili liwalo na liwe, liwe na liwalo! Dunia imekwisha imebakiwa utupu! Ukiwa umetanda katika nchi yetu! Matumaini yamefutika katika vifua vya Watanzania! Maisha yao sasa ni ya wasiwasi! Mioyo yao imejaa hofu nyingi na hasira kali! Bomu la gesi lililomo ndani ya vifua vyao, ltakapolipuka itakuwa  liwe na liwalo!

Utu umekwisha umebakia unyama! Shetani amekwisha kufanya kazi yake. Mioyo ya watu wa Mungu imepondekapondeka kwa kukata tamaa! Nchi gani hii iliyojaa migomo kila mahali? Mashaka yanatawala, faraja imepotea kwakuwa shetani ameamua liwalo na liwe!

Dk. Ulimboka sasa wewe kufa tu ili liwalo na liwe, liwe na liwalo! Kifo ni kazi ya Mungu mateso ya Dk. Ulimboka ni kazi ya shetani! Nani ataishi milele? Sote tu marehemu watarajiwa! Hukufa leo, utakufa kesho! Wanaoua leo, nao watakufa kesho. Anasa za dunia hii zinatupeleka wapi mpaka kutenda unyama huu? Nani anafuata! Wataua wangapi ili wabaki katika anasa zao! Liwalo na liwe, bas, liwe na liwalo!

Rafiki yangu mmoja amenitumia ujumbe uliosomeka, “Yaliyomtokea Dk. Ulimboka yanahuzunisha sana na kunifanya nikumbuke alivyouawa kinyama Dk, Robert Ouko aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Kenya.” Vifo vya kishenzi kama kilichomsibu Sajenti Samuel Doe wa Liberia ni mambo tuliyokuwa tunayasikia tu kutoka nchi za wenzetu.

Yaliyomkuta Dk. Ulimboka yanatia simanzi na majonzi kwa kila atakayeyakumbuka baadaye. Atakayesimuliwa atashindwa kuelewa ni kwa kiasi gani binadamu anaweza kuwa mkatili kwa binadamu mwenzake kiasi hiki!

Liwalo na liwe limekuwa blanketi zito jeusi la simanzi; limeufunika gubigubi uso wa nchi yetu. Nani atasimama kuwaokoa watu wa Mungu kutoka kwenye mkono wa giza la mauti?

Hatujajua nani wa kumkamata kwa unyama huu. Lakini tunalojua ni kwamba kuna mgogoro mkubwa kati ya madaktari na serikali. Pia tunajua kuwa Dk. Ulimboka ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania na ndiye anaongoza mgomo wa madaktari. Hivyo, kusema Dk. Ulimboka alikuwa katika ugomvi mkubwa na serikali ni sahihi kabisa.

Mwanadamu alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu ni kwamba, maafa yanapomkuta mtu yeyote, wa kwanza kushikwa uchawi ni yule aliyenaye katika ugomvi wakati huo. Wanaofikiri kuwa serikali ndiyo imetenda unyama huu dhidi ya Dk. Ulimboka, wanafikiri kibinadamu! Kumbe wafikirije? Ni haki yao kufikiri hivyo. Liwalo na liwe, sasa liwe na liwalo!

Njia pekee kwa serikali kujitoa katika tuhuma hii ya kusikitisha nikuwakamata wanyama waliohusika na tukio hili na kuwaonyesha hadharani kwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wakahukumiwe. Siyo kukataa kwa kutumia midomo iliyozoeleka kwa kauli za mashaka!

Bila kufanya hivyo liwalo na liwe, damu iliyomwagika ya Dk. Ulimboka, itabaki juu ya vichwa vya watu wa serikali kwa wale wanaofikiri kibinadamu, mpaka siku yao ya mwisho.

Kwa kuwa imani iliyopo ni hiyo, basi haitakuwa sahihi hata kidogo kwa polisi, ambacho ni chombo cha serikali kuunda tume ya kuchunguza tukio hili la kuhuzunisha.

Ikumbukwe kuwa Pande ni Pande tu! Iwe Mabwe-Pande au msitu wa Pande ukiunganisha na polisi vichwani mwa wananchi inaibuka kumbukumbu ya kutisha inayokumbusha tukio la kinyama lililowasibu wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge na dereva teksi wa Dar es Salaam.

Waliuawa kwa kupigwa risasi visogoni bila kuwa na hatia yoyote. Polisi walidai ni majambazi lakini Tume Huru iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete ilibainisha wazi kwamba polisi ndio walioua.

Kosa likafanyika, polisi wakafungua kesi, wakavuruga ushahidi mahakama ikawaachia washirika wa mauaji ila ikaagiza polisi muuaji akamatwe. Huu ni mwaka wa saba, polisi hawahawa wanaotaka kuchunguza suala la Dk. Ulimboka, wamekwepa kumkamata mwenzao aliyeua wafanyabiashara wale.

Mgomo wa madaktari haukuanza leo. Kama ulivyo mbuyu ambao huota ukiwa mdogo kama mchicha, baadaye hukua na kuitwa mbuyu kwa ukubwa wake. Mgomo wa madaktari umekuwa mbuyu mkubwa, hivyo, serikali inapojaribu kuukata kwa panga inastaajabisha.

Madaktari waliporudi kazini mwezi wa pili niliandika kuitahadharisha serikali kwamba, ingawa madaktari wamerudi kazini, mgomo wao haujaisha. Watu ambao mioyo yao imepondekapondeka kurudi kazini hakuwezi kumaliza tatizo.

Ni bahati mbaya kuwa makosa yaliyofanyika katika kumaliza  mgomo mara ya mwisho yanajirudia. Vitisho na kutishia ni dalili za mtu aliyepoteza mwelekeo katika mapambano.

Huwezi kujivunia madaktari wa Jeshi ambao nao wana wagonjwa wao wa kutosha. Madaktari wa Jeshi hawagomi, lakini ni mshahara upi mkubwa kati ya ule wa kijeshi na wa udaktari?

Waliojenga hospitali za serikali wakatenga kuwa hizi zitumiwe na jeshi na hizi zitumiwe na raia walikuwa na fikra kubwa. Una akili gani kutaka kuuvuruga utaratibu huo? Ni kupotoka kunakoashiria maafa zaidi kwa raia na kwa wanajeshi pia.

Je, siyo kweli kuwa ukiwajumlisha madaktari wote, wanajeshi, wa hospitali binafsi na hawa waliogoma nchi bado ina upungufu wa madaktari? Unazibaje upungufu kwa kutumia upungufu? Viongozi wetu wanahangaika sana huku wakifanya kazi ya bure.

Umri wa kustaafu ukifika mtu aliyechoka anapumzika. Kuna akili gani kumrudisha mchovu shambani? Hao madaktari wa kigeni wanaletwa kujitolea? Hawatalipwa?

Madaktari wanadai vitendea kazi. Wamechoka kuona wagonjwa wakifariki kwa kukosa hata oksijen tu! Wamechoka kuwalaza wagonjwa chini au kuwalundika katika kitanda kimoja wenye magonjwa tofauti tofauti. Wamechoka kuwaandikia wagonjwa dawa ambazo hazipo hospitalini lakini kwenye Bohari Kuu ya madawa zipo. Wanaitaka serikali inunue.

Wanadai wanaohusika na ununuzi wa mitambo ya kitabibu kwa bei mbaya, lakini mibovu waondolewe. Wanaoruhusu madawa feki waondolewe. Haya mbona hayasemwi na serikali? Imeng’ang’ania moja tu, madaktari wanataka fedha.

Kuagiza madaktari kutoka nje ni kutapatapa kwa mfa maji. Hao madaktari watakuja na vitendea kazi vyao? Wataleta madawa yao, vitanda vyao na vifaa vingine? Kwanini hizi Sh. 200 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya madaktari kutoka nje, zisitumike kumaliza kadhia hii kama serikali ina dhamira ya kweli?

Kesho walimu watakapogoma tutaagiza walimu kutoka nje! Busara iko wapi hapa? Tukiendekeza fikra mufilisi kama hizi iko siku tutajikuta tunaagiza hata Rais kutoka nje! Kama kauli ya “liwalo na liwe” imekuwa hivi kwa Dk. Ulimboka, basi liwe na liwalo.

Mungu wa Ibrahim, Mungu wa Yakobo aturehemu waja wake!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: