Tarime: Jumapili njema!


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version

JUMAPILI ijayo, wananchi wakazi wa jimbo la uchaguzi la Tarime, mkoani Mara, wanaandika historia. Ni kunyakua au kunyang’anywa ushindi. Basi.

Hakuna haja ya kubashiri wanataka nini. Ni ushindi tu; kuukosa ni msiba, hasa baada ya uwanja wa mapambano kumeza mate, jasho na damu vya waliomo na wasiokuwemo.

Siku hiyo, tarehe 12 Oktoba, ndiyo siku ya kupiga kura kuchagua Diwani wa kata ya Tarime Mjini na Mbunge wa kuziba pengo lililoachwa na Chacha Wangwe aliyefariki kwa ajali ya gari zaidi ya miezi miwili iliyopita.

Siku hii inasubiriwa siyo kwa ajili ya kupiga kura tu, bali pia kusitisha vita vya maneno; misuguano ya kauli, vijembe vilivyojaa kejeli; uwongo uliokithiri, matusi na vitisho vya kila aina.

Kibwagizo kikuu katika ushindani ndani ya Tarime kimekuwa “Tarime ni ya wana-Tarime na wao wachague yule wanayemwona atakuwa mtumishi bora.”

Siku hiyo haifiki haraka. Wana-Tarime  wanasubiri ifike na kuondoka. Wanatamani mwisho wa uwongo. Wanaomba siku ifike askari waondoke mitaani na vijijini.

Wana-Tarime wanatamani mwisho wa kauli za viongozi wa vyama vingi zilizogongana na kuwapa kazi ya kupembua kila kukicha au kuwaletea kizunguzungu na utata. Lakini Tarime haitakuwa ileile ya zamani. Itakuwa imebadilika.

Vumbi litakapokuwa limetua, wadadisi wataanza kujiuliza na kuuliza wengine, iwapo Tarime ulikuwa uwanja wa elimu au uwanja wa ghiliba. Au Uwanja wa Fujo?

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ndicho mpinzani mkuu wa CCM. Kimepata kuwa mpinzani mkuu kwa sababau kadhaa.

Kwanza, kinatafuta kuziba pengo la mbunge wake; kwani aliyefariki alikuwa anatoka Chadema. Pili, ni chama ambacho kimeandamwa zaidi na CCM inayotambua nguvu ya Chadema jimboni.

Tatu, ni Chadema ambayo imekuwa ikishambuliwa huku na kule na CCM na baadhi ya vyama vya upinzani, kwa madai, shutuma na tuhuma kadha wakadhaa.

Tano, ni Chadema ambayo, kwa kazi yake, imesababisha CCM kuomba msaada zaidi wa askari.

Christopher Mtikila wa DP akiomba msaada wa ulinzi, ni jambo ambalo linaweza kueleweka. Lakini CCM kuomba kujihifadhi kwenye kwapa la askari, ni kiroja na historia imenukuu.

Kitendo cha chama tawala kuomba “askari zaidi” kinaweza kutafsiriwa kama woga tu wa kushindwa, au hata nia mbaya ya kutaka kutumia askari kwa manufaa yake.

Alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa aliyesema atamwambia Rais Jakaya Kikwete aongeze idadi ya askari Tarime ili kukabiliana na “fujo” au maasi (?).

Kama Tarime inahitaji askari zaidi na sharti makamu mwenyekiti wa chama tawala aombe msaada wa rais, basi huko mbele kuna matata makubwa.

Kama Tarime inahitaji “askari zaidi,” na ni jimbo moja tu, itakuwaje wakati wa uchaguzi katika majimbo yote? Si itabidi rais afanye safari nyingine Marekani kuomba majeshi yanayotarajiwa kutoka Iraki?

Sita, ni Chadema iliyofaulu kubomoa ngome ya CCM, kuotesha mtafaruku hadi chama hicho kilichopanga ikulu kumeguka kimawazo na kuondoa hata wapigadebe wake kwenye misafara ya kampeni.

Saba, ni Chadema, kwa kazi yake, na kwa kuungwa kwake mkono na wanachama na wasiokuwa wanachama wa vyama vingine, ambayo inatishia kibarua cha Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM.

Hakika kushindwa kwa Makamba na CCM huko Tarime kutahusishwa na kutokuwa na uwezo wa kutumia “zana za kisiasa” alizopewa na kushindwa “kuongoza majeshi.”

Kutoelewana na ugomvi katika kambi ya Makamba-CCM, kutachukuliwa kuwa mapungufu makubwa kwa upande wa yule aliyejiita “Yohana Mbatizaji.”

Mambo hayo saba yanaiweka Chadema kwenye kinyang’anyiro na CCM. Aidha, kunaipa Chadema matarajio makubwa ya kushinda; bila kukataa uwezekano pia wa CCM kupata mbunge kwa njia ilizozoea – “teknolojia!”

Jumapili yaweza kuwa siku nzuri kwa wanaolipenda taifa lao; wale ambao watakataa kuiba kura na watakaoepuka kupiga kura mara mbili.

Yaweza pia kuwa siku nzuri kwa askari watakaokataa vishawishi vya kuonea upande unaopambana na CCM; kukataa kupiga kura na na kukubali kuwa watumishi wema bila woga wala aibu.

Ni Jumapili hii ambayo itawaadabisha watumishi wa Tume ya Uchaguzi (NEC) ili wawe waangalifu; watumie busara na mwishowe watangaze mshindi. Mshindi yupi? Wana-Tarime wanajua.

Na ije Jumapili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: