Tarime waweza kumkataa mbunge wa kuchongwa


Stanislaus Kirobo's picture

Na Stanislaus Kirobo - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version

KWA mtazamo wowote ule, vita kali ya kampeni zinazoendelea katika uchaguzi mdogo katika jimbo la Tarime, mkoani Mara, ni vita kati ya wanaopinga ufisadi na wale wanaoutetea.

Kwa muda sasa, harakati za kutokomeza ufisadi nchini zimekuwa zikiendelea. Ni viongozi wa Chadema  waliofichua tuhuma nzito za wizi wa mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya EPA ya Benki Kuu – pamoja na ufisadi mwingine.

Na viongozi hao wameendelea kuibana serikali ili iwachukulie mafisadi hatua za kisheria, zikiwamo zile za kuwafikisha mahakamani.  

Lakini kwa upande wao, wezi hao, bila shaka kutokana na uwezo wao mkubwa wa fedha hizo hizo za wizi, na ukaribu walionao kwa wakubwa wa nchi hii, wameweza kuzivuruga na kuzidhoofisha jitihada za wale wote wanaotaka waadhibiwe.

Hayo yanafanyika kwa mbinu mbalimbali kubwa ikiwemo ile ya kutumia baadhi ya vyombo vya habari, hususan magezeti na wahariri wao kuandika habari za ufisadi kwa namna ya kuwasafisha.

Aidha, wameweza pia kuvitumia baadhi ya vyama vidogovidogo vya upinzani kuendesha kampeni dhidi ya Chadema, ambacho kimeonekana kuinuka na kukua kwa miaka ipatayo mitatu sasa.

Baadhi yao wamediriki hata chama hicho kwamba kilihusika na mauaji ya aliyekuwa mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, aliyefariki kwa ajali ya gari mjini Dodoma.

Wananchi wenye akili timamu wanaona wazi kabisa kuwa wanaoendesha kampeni hizi wanajaribu tu kufunika au kupindisha ukweli, kwani bila shaka wao ndiyo wahusika wakubwa.

Wananchi wengi wanasema iwapo wanao ushahidi, basi mahali pa kutoa ushahidi huo ni polisi, na si katika majukwaa ya makampeni.

Ikumbukwe kuwa CHADEMA walipoamua kuibua hoja ya ufisadi majukwaani, walikuwa wamejaribu kupitisha hoja hiyo bungeni, lakini waliwekewa vikwazo na wahusika.

Kwa hivyo, inaonekana kwamba CCM wameamua kutumia hoja ya kifo cha Wangwe kama mbinu tu ya kisiasa ya kuipiku CHADEMA, na kujaribu kuwachafua viongozi wake ili kupunguza makali ya vita ya ufisadi.

Ni wazi pia kwamba wameamua kuwatumia baadhi ya wapinzani wenye njaa kukamilisha lengo lao chafu, lakini wananchi wameshagundua ujanja huu.

Ni vigumu kwa watu wenye akili timamu kuamini ghiliba za CCM kabla serikali haijachukua hatua zozote makini dhidi ya mafisadi.

Na sasa CCM wanatumia nguvu nyingi za dola na pesa kuwahadaa wananchi wa Tarime. Wanatumia ufisadi huo huo kununua kura na kutisha wapiga kura.

Na licha ya baadhi ya vyama vya upinzani kuthubutu kuishambulia CHADEMA badala ya CCM, nguvu ya vyama hivyo haionekani, na kauli wanazotoa zinashambuliwa CHADEMA badala ya CCM.

Kwa sababu hiyo, iwapo CCM watachukua jimbo la Tarime kwa mbinu zozote, utakuwa ushindi mkubwa sana (walau kwa muda) wa mafisadi.

Na kama CHADEMA wakishinda, basi itakuwa ni ushindi kwa umma mzima wa Tanzania.

Nguvu ya fedha ni kubwa sana, kwani huweza kumfanya mtu kupoteza kabisa utu wake pamoja na kile ambacho daima hukiamini, na hivyo kumpotezea kabisa msimamo wake na heshima pia mbele ya umma.

Kwani mtu huyo anajikuta anatetea yaliyo maovu, na hata giza kuliita mwanga, na pia kinyume chake.

Kwa upande wa chama tawala, hali hii inasikitisha sana. Wengi wanaona kuwa iwapo chama hicho kimefika hapo, basi yumkini ndiyo mwanzo wa mwisho wake, kwani katika historia ya dunia, hakuna kundi la watu lenye kujitumbikiza katika maovu likaendelea kuwapo daima dumu.

Lakini pia hebu fikiria hili: CCM ina zaidi ya viti 280 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Kwa upande wao wapinzani wana viti vipatavyo 65 tu – huku CHADEMA yenyewe ikiwa na viti kama 10 tu.

Kwa hivyo, hicho kiti kimoja ambacho CCM inakigombania kwa udi na uvumba, kitawapa nini cha ziada? Kitawaharibia nini wakikikosa?

Lakini CCM wako tayari kukichukua, liwalo na liwe, hata kama kwa kufanya hivyo itabidi wamwage damu ya wananchi wa Tarime. Tayari kuna watu huko Tarime wamepoteza maisha au kujeruhiwa kutokana na kampeni chafu.

Lakini lengo kubwa kwa ushindi wa CCM ni kuuonyesha umma wa Tanzania kuwa ajenda ya “ufisadi” inayoenezwa na viongozi wa  CHADEMA na baadhi ya wabunge wa CCM ni uzushi tu.

Lakini vyovyote itakavyokuwa, ushindi wa CCM utakuwa ni “onyesho” linalolazimishwa kwa nguvu ya fedha na zile za dola, kwani wananchi wanajua kuwa mamia ya askari wamemwagwa huko kutokana na ombi la Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa.

Kampeni zimewashinda, wakakimbilia kutumia polisi kutisha wananchi. Hata hivyo, CCM wanapaswa watambue kuwa wakilazimisha kumpitisha mtu wao kwa nguvu, kinyume cha matakwa ya wana Tarime, mtu huyo anaweza asikanyage Tarime.

Wana Tarime, kwa jinsi tunavyowajua, wana uwezo wa kumkataa mbunge wa kuchongwa. Ni heri wakae bila mbunge kuliko wawekewe mtu ambaye hawakumchagua.

Kwa sababu CCM na serikali yake wameshindwa kusimamia haki, na kwa sababu wanaamini kwamba amani ya Tarime inaweza kusimamiwa na polisi badala ya haki, wasije kushangaa iwapo Tarime itakumbwa na machafuko makubwa zaidi kama utakuwapo ushindi wa wizi.

Yaliyotokea Kenya mapema mwaka huu, yawe fundisho kwa CCM na serikali.

Kama Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Samuel Kivuitu, asingemtangaza (kwa shinikizo) mgombea aliyeshindwa kuwa ndiye ameshinda; umma wa Wakenya usingeingia barabarani na kuleta ghasia tulizosikia.

Amani ya Tanzania, na sasa katika Tarime, inachezewa na wanasiasa wa chama tawala wanaodhani kwamba hila zao ndizo zinawakilisha matakwa ya wananchi. Ni aibu kwamba watawala hawaoni ghasia inayowanyemelea kutoka Tarime.

Hata kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupoteza majina ya wapiga kura katika wiki ya mwisho ya kampeni, ni onyesho la jeuri ya watawala kutumia nguvu zote kushinda kwa hila.

NEC inasahau kuwa hasira za wananchi wa Tarime zinaweza kuwageukia maofisa na wakurugenzi wa Tume hiyo hiyo, kama njia pekee iliyobaki ya kujitetea.

Kwa hiyo, ili kuepusha umwagaji damu Tarime, serikali na CCM wakubali kusimamia haki. Atakayeshinda kihalali ndiye atangazwe.

Lakini hayo yote yatategemea mchakato mzima hadi siku ya uchaguzi kama umekuwa wa haki au dhuluma.

Tusisubiri kulaumu wananchi kwa matokeo ya hasira za kuibiwa kura. Tutambue kuwa wananchi wana uwezo wa kufanya watakalo, pale wanapobaini kwamba serikali imeziba njia zote za wao kujitetea na kujipatia haki kihalali.

Wana uwezo wa kumkataa hata mgombea aliyepewa ushindi bandia. Kama hili halijawezekana kwingine, Tarime linawezekana.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: