TASWA imemuona Kado, vipi Maximo!


Alloyce Komba's picture

Na Alloyce Komba - Imechapwa 21 January 2009

Printer-friendly version

KLABU ya Mtibwa Sugar yenye maskani yake Turiani, mkoani Morogoro, ndio mabingwa wa Kombe la Tusker wa mwaka 2008/2009. Wamedhihirisha ni waibuaji wa vipaji vya wanasoka kwani wametoa wachezaji wengi wenye mchango mkubwa katika taifa na klabu kubwa za Dar es Salaam.

Wachezaji waliowahi kuibukia Mtibwa Sugar na kung’ara walipoingia Taifa Stars ni pamoja na aliyekuwa nahodha wa muda mrefu wa timu hiyo, Mecky Mexime, Nizar Khalfan, Abdi Kassim, Shaaban Nditi na beki wa kati mhimili wa sasa, Salum Sued Kusi.

Wakati tulipofunga mwaka 2008 kwa michuano ya Kombe la Tusker, Mtibwa ilionyesha kiwango cha soka cha hali ya juu ikiwa chini ya kocha wake mhamasishaji, Salum Mayanga.

Wachezaji waliong’ara sana katika michuano ile naona walikuwa ni pamoja na mlinda mlango wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado, beki Chacha Mwita na washambuliaji Zahoro Pazi na Uhuru Selemani.

Hivi karibuni, Chama cha Waandishi wa Habari wa Michezo Tanzania (TASWA) kiliteua mwanamichezo bora wa mwezi Desemba 2008 akiwa ndiye aliyehitimisha orodha ya wanamichezo bora wa mwaka uliopita kwa mtazamo wa TASWA.

Aliyeibuka kidedea ni Athumani “Chuji” Iddi. Hata hivyo kulikuwa na wanasoka wawili waliopata kura wakimfuatia Chuji: Shaaban Kado na Zahoro Pazi. Hawa wote ni wa Mtibwa Sugar.

Namchambua huyu Kado kutokana na jinsi alivyohimili mashambulizi ya timu zenye wachezaji wazoefu katika michuano ya Tusker hasa pale timu yake ilipopambana na bingwa mtetezi, Yanga. Mtibwa ilishinda mechi hiyo kwa bao 1-0 kama ilivyoilaza URA ya Uganda katika pambano la fainali.

Kado alipanga vizuri mabeki wake akina Kusi na yeye mwenyewe kutulia golini akifuata vilivyo mipira ya krosi na ya adhabu. Alitukumbusha enzi zile za akina Juma Pondamali Mensah au Iddi Pazi “Father”, mtoto wa kipa wa zamani aliyeng’ara nchini, Iddi Pazi. Halafu Kado alikuwa akileta burudani uwanjani kutokana na kunyaka mipira kwa staili ya kushangaza huku akipiga kelele zenye kuwakumbusha mabeki wake kukaba au kufungua nafasi.

Swali langu la leo ni: Kama TASWA walimuona mlinda mlango huyo mwenye umri mdogo alivyocheza kwa umakini uwanjani na kuiwezesha timu yake kutwaa kombe, medali na kitita cha Sh. 40 milioni.

Je, kocha mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo au wasaidizi wake wa benchi la ufundi nao walimuona? Wanasemaje? Hawaoni kwamba Kado anafaa kuongezwa katika timu ya taifa? Au yumo katika wachezaji sita ambao inasemekana Maximo aliwaona katika michuano hiyo kama alivyonukuliwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema?

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwalimu Sunday Kayuni, anasemaje? Hawezi kumshawishi kocha Maximo amjumuishe Kado katika kambi ya timu ya taifa itakayojiandaa kwa michuano ya nchini Ivory Coast mwezi ujao? Maana tumeachana na kumpigia debe Juma Kaseja ambaye ni kama vile amefungiwa milango daima kwa geti la chuma, na Maximo!

Natambua pia Maximo hana mpango wa kukibadili kikosi chake kilichoipeleka Taifa Stars kwenye fainali za CHAN, ingawa katika maandalizi anaweza kujumuisha wachezaji chipukizi kadhaa ili wapate uzoefu. Wapenda soka wengi tunakubaliana naye kwamba asibadili timu hata kama katika michuano ya Challenge haijafanya tulivyotarajia ila imejifunza isijiandae kiufundi tu bali pia kisaikolojia ikiwemo nidhamu na kutokukata tamaa.

Pia Maximo anapaswa kuziba pengo la kuwepo makipa watatu lililoachwa na aliyekuwa mlinda mlango namba moja (Tanzania One) na swahiba mkubwa wa Maximo, Ivo Mapunda, ambaye hana sifa tena za kucheza michuano ya Ivory Coast kwa vile sasa ni mchezaji wa kulipwa.

Hata kama Farouk Ramadhani wa Zanzibar atakuwepo tena kuungana na akina Shaaban Dihile na chipukizi wa miaka 19 aliyeng’ara kwenye Challenge ya Uganda, Deo Boniventure “Dida”, Kado anahitajika kuitwa ili naye aanze kuzoea mazingira ya kambi ya Taifa Stars.

Makocha wa timu zote zitakazoshiriki fainali za CHAN wapo katika harakati za kuimarisha vikosi vyao hasa katika safu ya ulinzi inayojumuisha walinda milango. Wanafanya hivyo kwa kutambua kuwa ni afadhali kutoka sare au suluhu michezo yote au kufungwa mabao machache kuliko kuwa na safu ya ulinzi yenye kuruhusu mabao mengi. Hiyo inakuwa ni aibu kubwa. Ndio maana timu za nchi za Waarabu kama Misri, Morocco, Algeria na Tunisia huwa hazikubali kufungwa kirahisi kwa kuwa zina ngome ngumu.

Kwa kuwa mfumo wa Maximo ni ule anaouita mwenyewe “Compact System” unaohimiza wachezaji kukaba sana hasa katikati, huku mabeki wa pembeni akina Shadrack Nsajigwa na Juma Jabu wakipanda kwa kasi katika wingi ya kulia na kushoto ili kusaidia washambuliaji, tunahitaji walinda mlango watatu mahiri wanaopaswa kufundishwa namna ya kusoma mchezo na kuwasiliana haraka na mabeki. Hii ni katika kuepuka madhara kama yaliyotokea Kampala pale Kilimanjaro Stars ilipolala 2-1 kwa Harambee Stars ya Kenya.

Kukiwa na ngome imara yenye akili ya ukabaji na kujipanga vizuri wakati wa krosi au kona au mipira ya kufa (adhabu ndogo au kubwa) inayotuumiza mara nyingi, itakuwa nafasi kwa walinda milango wenye kujiamini kama Kado kuokoa hatari.

Huwa inasemekana kuwa katika uundaji wa timu ya taifa, lazima kuhakikisha wanapatikana walinda mlango mahiri miongoni mwa wachezaji wengi waliomo nchini. Hivyo ndivyo wafanyavyo nchi kama Cameroon walikokuwa akina Thomas Nkono na Joseph Antoine Bell. Na hapa Tanzania ilikuwa ni hivyo zamani ndio maana tukawa na akina Omar Mahadhi bin Jabir na Juma Pondamali.

TFF wangetafakari haya kwa kujiuliza: iwapo TASWA imemuona huyu Kado, vipi kwa Maximo? Tukumbuke hata akina Danny Mrwanda, Mrisho Ngasa na Mussa Hassan Mgosi walikuwa wakipigiwa debe na vyombo vya habari ikiwemo kupata tuzo mbalimbali za michezo.

0
No votes yet