Tatizo la ma-First Lady wetu


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 17 March 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Mke wa Rais, Salma Kikwete

MWAKA 1919, aliyekuwa Rais wa Marekani, Woodrow Wilson, aliugua kiharusi kilichopunguza uwezo wake wa kufanya kazi.

Katika kipindi hicho, mkewe, Edith, inasemwa ndiye aliyekuwa akifanya kazi za urais .

Edith alikuwa akipanga miadi yote ya Ikulu, akimsainisha rais Wilson maamuzi aliyoona yanafaa kuridhiwa na kukataa kumsainisha yale aliyoona hayafai kwa taifa.

Kwa hivyo, Edith ndiye alikuwa akitambuliwa kiongozi wa nchi.

Kwa bahati nzuri, kwa muda ambao alifanya kazi za urais, Edith hakupata tatizo la kiutendaji. Wamarekani waliona kila kitu kinakwenda sawa.

Mtazame Cherie Booth, mke wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.

Hawa walikutana chuo kikuu ambako inaelezwa Cherie alimzidi Blair kwa akili ya kusoma.

Cherie alikuja kuajiriwa mapema kuliko Blair, katika kampuni kubwa ya masuala ya kisheria.

Bado Cherie aliendelea na kazi yake ya uanasheria huku Blair akiwa waziri mkuu.

Wote ni wasomi. Wote wana bongo zinazochemka. Uwezo wao wa kujenga hoja unafanana.

Tumeona pia namna Hillary Clinton alivyopambana na Barack Obama kwenye mchakato wa kuwania uteuzi wa kugombea urais ndani ya chama chao cha Democrat mwaka jana.

Clinton hakutaka kuwania urais kwa sababu aliwahi kuwa First Lady wa Marekani. Alifanya hivyo kwa sababu aliamini katika uwezo wake kama msomi wa kiwango cha juu na mwanasiasa.

Na Marekani isingekuwa na tatizo lolote kama angekuwa rais wao.

Tazama namna mke wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Jimmy Carter, Rosalyn, alivyokuwa akishiriki vikao vya baraza la mawaziri kwa sababu mawziri wote waliamini alikuwa na uwezo mkubwa.

Na Wamarekani wataendelea kumkumbuka Eleanor Roosevelt kwa alivyokuwa mwanaharakati mkubwa enzi mumewe, Franklin, alipokuwa rais.

Kwa nchi zinazoendelea, zikiwemo za Afrika, tofauti ni kubwa mno.

Tazama Ufilipino, na mfano mzuri utakuwa kwa aliyewahi kuwa mke wa Rais Fernando Marcos, aliyekuwa akiitwa Imelda.

Mwanamama huyu mrembo alikuwa akifahamika sana kwa tambo na matanuzi yake. Alipata kumiliki jozi zipatazo 1,000 za viatu.

Kuwa mke wa rais, kwake ilimaanisha kuvaa vizuri, kula vizuri na kusafiri kila mahali duniani.

Hatujasahau Oktoba 2005 aliyekuwa mke wa Rais Olusegun Obasanjo wa Nigeria, Stella, alipofariki dunia hospitalini Hispania alikokwenda kwa operesheni ya uso ili kumfanya apendeze zaidi ya alivyokuwa.

Alitaka aonekane kijana zaidi ya umri wake. Apendeze sana kuliko alivyokuwa.

Kwake, kuwa First Lady, aliamini alipaswa kuwa mzuri isivyo kawaida ili kila anayemuona ampe tabasamu.

Grace, mke wa rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, amepewa jina la utani la First Shopper. Ni kwa sababu ya tabia yake ya kupenda manunuzi utadhani maduka yote yatafungwa siku ya pili. Mpenda starehe babkubwa.

Kenya yupo Lucy, mke wa Rais Mwai Kibaki. Anapenda ugomvi, tena wakati mwingine usio na sababu.

Anapenda kuheshimiwa japo si lazima yeye kujiheshimu. Mtu asipomheshimu, au akamdharau mumewe, atajuta.

Ajuavyo, kama mama wa nyumba kubwa, First Lady, lazima aogopwe na kupapatikiwa na kila mtu, bila ya kujali kama ana elimu, uwezo au hoja.

Kukosana na rais umekosana naye. Na kukosana naye umemkosea rais na usisahau yeye analala kitanda kimoja na mheshimiwa sana!

Wake wa marais Afrika wana matatizo kiasi kwamba wangekuwa na kiwango cha uwezo na hoja kama za Hillary au Cherie, Afrika ingekuwa mbali.

Katika nchi ambazo uongozi ni mipango ya muda mrefu siyo zimamoto, suala la mke wa kiongozi ni jambo la kuzingatiwa sana.

Ndiyo maana si ajabu kwa wenzetu walioendelea, kuamini kwamba “nyuma ya mafanikio ya mwanamume yupo mwanamke.”

Na mifano ya namna wenzetu wanavyotafuta wake iko wazi. Anayetaka kuitafuta, ataipata tu.

Chukulia mfano wa Rais Abraham Lincoln wa Marekani. Mkewe, Mary Todd, alikuwa na elimu nzuri kumzidi.

Lakini kubwa zaidi, Mary Todd alitoka katika familia yenye uwezo mkubwa kifedha.

Isingekuwa utajiri huo, pengine mwanamke huyo asingekuwa rais wa Marekani.

Kwa hiyo, ingawa hawakupatana kwa mambo mengi, Abe alijua mwanamama huyo angemsaidia kufika Ikulu kwa elimu yake na kwa fedha zake.

Napata taabu sana kuona namna ambavyo Kenya ingekuwa iwapo Kibaki angepatwa na tatizo lolote la kiafya halafu Lucy ndiyo akawa anakaimu kama ilivyokuwa kwa Edith.

Au, katika namna ya kipekee, kama Mama Lucy angewania urais, kama ilivyokuwa kwa Hillary Rodham Clinton, na kushinda.

Fikiria Kenya ingekuwa ya namna gani chini ya uongozi wa Lucy Kibaki? Nani angethubutu kuandika lolote kuhusu uozo wa serikali anayoongoza?

Haiwezekani rais wa nchi akawa na mwanamke ambaye tamaa yake kubwa ni mali na kuvaa vizuri na bado nchi ikaendelea.

Kwa kuwa watu kwa kawaida wamezoea kuwaogopa viongozi wao, mkewe ni lazima atakuwa mtu wa mwisho kumuogopa. Kama kuna ukweli wa kumwambia atamwambia.

Hata aina ya mijadala watakayokuwa nayo kabla ya kulala, itakuwa ni ya manufaa kwa taifa. Watazungumzia uchumi, siasa, utamaduni na kadhalika.

Lakini, kama mke wa rais ni dizaini ya wengi waliopo Afrika (na Tanzania), rais atakuwa anapewa habari za umbeya, majungu, madogoli, ushirikina na zile zinazolenga kumfurahisha tu mama.

Kwa kujua umuhimu wa wake za marais, nchi kama Uingereza au Marekani, zimeamua kuanza kuwahoji wake za wagombea urais kabla ya uchaguzi.

Wanavyoamini ni kwamba ukimfahamu mke wa rais, ni rahisi kufahamu mumewe ni mtu wa aina gani.

Hii ni kwa sababu kama rais au waziri mkuu ameshindwa kuchagua mwanamke mzuri wa kuishi naye maishani, atawezaje kuchagua la manufaa kwa taifa lake?

Wenzetu wanaamini, kama mwanamke wa rais ni ovyo, na rais mwenyewe atakuwa wa ovyo tu.

Wanaamini mawazo ya rais yanaathiriwa sana na maoni ya mkewe. Hii ni kwa sababu, huyu, pengine, ndiye mtu wake wa karibu zaidi kuliko wote awaonao duniani.

Tazama namna Wafaransa wanavyomuadhibu Nicolas Sarkozy kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaoendelea.

Ni kwa sababu amemuoa Carla Bruni, mwanamitindo aliyewahi kupiga picha kibao za uchi. Wanajua tu kwa First Lady huyu, Sarkozy hawezi kujenga hoja nzito za kuikwamua nchi yake kutoka msukosuko wa kiuchumi.

Badala ya kuwazia matatizo ya Ufaransa, atakuwa anawaza tu kuhudhuria hafla ambazo zitamtoa ajitanue kwenye fukwe na kujianika kwenye viti vya uvivu.

Itakuwa umefahamu sasa kwa nini Tanzania inaendelea kujichimbia kwenye dimbwi la ufukara.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: