Tatizo la ma-First Lady wetu 2


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 30 March 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Mke wa Rais, Salma Kikwete

UKISOMA asili ya jina la First Lady, unaweza kupatwa na mshangao kidogo. Kwa mara ya kwanza, lilitamkwa hadharani na Rais wa 12 wa Marekani, Zachary Taylor, mwaka 1849.

Taylor aliyetawala kwa miezi 16 tu, alitaja jina hilo wakati wa msiba wa Dolley Madison aliyekuwa mke wa rais mwingine wa zamani wa nchi hiyo, James Madison.

Alisema kwa kifupi tu, “She was the Lady of the White House, and by courtesy, the First Lady of the Land. Tangu hapo jina la First Lady, kwa maana ya mke wa rais, likashika chati.

Zaidi ya miaka 150 baada ya kauli ya Taylor, dhana, dhima na wajibu wa ma-First Lady umekwenda mbali zaidi.

Ma-First Lady sasa wana hadhi ya kipekee katika nchi nyingi duniani. Katika siku za nyuma, walikuwa na nguvu kubwa lakini pengine hawakujulikana sana. Lakini leo, ma-First Lady ni maarufu kuliko baadhi ya mawaziri wa serikali.

Nchini Tanzania, kwa maoni yangu, Mama Anna Mkapa ndiye alikuwa mke wa kwanza wa rais kufanya shughuli nyingi za kijamii kuliko ilivyokuwa kwa Mama Maria Nyerere na Mama Sitti Mwinyi.

Nionavyo sasa, Mama Salma Kikwete anaweza akawa amefanya shughuli nyingi za kijamii kuliko waliomtangulia iwapo mumewe atakamilisha miaka yake kumi madarakani kama watangulizi wake.

Bali kabla ya kujadili mambo ya hapa nchini, pengine nieleze kuhusu First Lady maarufu zaidi wa Marekani, Eleanor Roosevelt aliyekuwa mke wa Rais Franklin Delano Roosevelt ambaye aliitwa kwa ufupisho wa FDR.

Huyu alikuwa mwanaharakati kabla na baada ya  mumewe kuwa. Alikuwa akifahamika kama mtetezi wa haki za binadamu.

Kwa hiyo haikuwa ajabu yeye kuwa miongoni mwa wale waliotengeneza ule Mkataba wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa na pia uanzishwaji Taasisi ya Kusaidia Maendeleo ya Watu wasiokuwa Weupe nchini Marekani (NAACP).

Na katika kipindi kirefu kabla na baada ya urais wa FDR, mama huyu alijihusisha na masuala ya haki za binadamu.

Kwanza kabisa, na hili ni muhimu sana, ifahamike kuwa First Lady si cheo bali ni hadhi ambayo mtu anapewa.

Hiki si cheo kilichopo kikatiba. Hii si nafasi ambayo iko katika mtiririko wa kiserikali. Ni heshima tu ambayo mke wa rais anapewa kutokana na nafasi ya mumewe.

Lakini katika dunia ya sasa, First Lady hawezi kuendelea kuwa “Mama wa Ikulu” tu. Anatakiwa kutoka nje ya ikulu na kukutana na jamii pana. Sasa swali ni anakwenda kukutana na jamii katika aina ipi na vipi?

Katika nchi ambazo zina mawaziri na wizara nyingi kama Tanzania, ni wazi maeneo mengi yanakuwa na watu ambao wanawajibika moja kwa moja katika majukumu tofauti.

Hii inamaanisha kwamba wakati Mama wa Ikulu anapoamua kutoka ikulu, ni lazima awe na kile ambacho ameamua kukipigania katika kipindi chote cha kushikilia “taji” hilo.

Na hapa kuna njia mbili. Kwanza, kama alikuwa  mwanaharakati anayefahamika tayari, anaweza kuendelea na shughuli hizo hata akiwa ikulu.

Hii ni kwa sababu watu watakuwa wamemfahamu kabla hata hajaingia ikulu. Wananchi watafahamu kuwa anafanya kile kinachotoka moyoni mwake.

Pili, ni yule ambaye alikuwa hafahamiki kabla. Huyu anaweza kuamua kuwa na kitu kimoja au viwili atakavyopigania hadi mwisho. Ni kweli kwamba wapo watakaolalamika, lakini kama ataamua kuwa na jambo moja, watu watamwelewa.

Lakini unahitajika mstari mnene kati ya shughuli za First Lady na zile za serikali. Hili litafuta minong’ono kwamba “Mama” anafanya kazi za rais.

Kwani kwa mujibu wa katiba na muundo wa utawala nchini, mume wa First Lady ndiye mwenye ridhaa ya wananchi na yeye pekee ndiye anayewajibika kwa wananchi. Peke yake.

Sasa katika Tanzania hali iko vipi? Kwa mazoea tu, mke wa rais anapotembelea mkoa, wilaya au hata kata, hakika anakuwa mgeni wa maana sana kama inavyotakiwa, lakini anakuwa “mgeni ghali.”

Mapokezi peke yake, kwa ngazi yoyote ile, yanahusisha, siyo tu itifaki za chama cha mumewe, bali hata serikali.

Wakuu wa wilaya na mikoa na watendaji wa ngazi mbalimbali watakuwepo kwenye mapokezi. Muda mwingi unatumika. Fedha za walipakodi zinatumika pia.

Si hayo tu. Mke wa rais akisafiri zaidi ya makamu wa rais, “wambeya” watalalamika. Akihutumia mikutano ya hadhara ambayo ilikuwa uhutubiwe na mawaziri na wakuu wa mikoa, watatokea “kilomolomo”m na kudai First Lady kavuka mpaka.

Ikitokea Fisrt Lady akaongelea masuala ya uhusiano wa kimataifa, kana kwamba anamwakilisha rais au waziri wa mambo ya nchi za nje, wachunguzi watasema kavamia maeneo yasiyomhusu.

Wanaosoma magazeti tando (blogu) kwenye wavuti, watakumbuka jinsi taarifa zilivyovumishwa, Novemba mwaka jana, kwamba Mama Salma anamsafishia njia mume wake kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba. Hii ilitokana na ziara zake nyingi mikoani.

Chukua mfano wa ziara ya Mama Salma mkoa wa Mbeya. Wakati Rais Jakaya Kikwete akimaliza ziara yake katika mkoa huo, Mama Salma alikuwa akitoka ziarani katika mkoa wa Rukwa na alikuwa anaanza nyingine mkoani Mbeya. Hapa yatatokea maneno.

Maneno yatazidi pale wafuatiliaji watakapokumbuka kuwa majuzi Mama Kikwete alikuwa Mtwara kwenye maadhimisho ya siku ya Utepe Mweupe na baadaye wiki hiyohiyo akaenda Arusha kwa shughuli zake nyingine.

Kwa hiyo, utaona hapa kwamba First Lady amekuwa na shughuli na safari nyingi kuliko hata baadhi ya viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri.  

Kuvinjari kwa aina hii ni muwafaka. Bali kuingilia mamlaka ya serikali kupitia bawa la rais, hiyo ndiyo muhali.

Je, kuna haja ya kuelekeza kisheria wake wa marais wafanye nini, wapi na hata kuwawekea mipaka ili wasikanyage “vidole vya serikali?”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: