Tatizo ni serikali, si walimu


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

MATOKEO ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne kwa mwaka jana yamewashtua wengi. Katika matokeo hayo, nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani huo mwaka 2010, walifeli. Hili halijawahi kutokea katika miaka ya nyuma.

Maswali mengi yameulizwa kutokana na matokeo hayo. Wengi wamehoji kuhusu viwango vya walimu wanaofundisha katika shule za sekondari sasa na wengine kuhusu miundombinu iliyopo katika shule zilizopo.

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, ana jibu rahisi kuhusiana na tatizo hili la kushuka kwa ufaulu nchini.

“Kama serikali kweli inataka wanafunzi wafaulu katika mitihani hawana pa kwenda zaidi ya kwenye shule zinazofanya vizuri. Ukiangalia katika orodha ya shule zilizofanya vizuri mwaka jana na katika miaka mitano iliyopita, shule binafsi zimefanya vizuri kuliko zile za serikali.

“Kwa hiyo, tiba ya kupambana na kufeli ni kuangalia tu wale waliofanya vizuri walifanya nini na serikali iige. Unaangalia mazingira ya kujifunza, idadi ya wanafunzi kwa mwalimu, maslahi ya mwalimu na mindombinu ya shule. Ukifanya kama wanavyofanya wanaofaulisha, nawe utafaulu pia,” anasema.

Mukoba anasema shule zinazomilikiwaa watu binafsi zimekuwa zikifanya vizuri kila mwaka kwa kuwa wamiliki wake wanawapa motisha mara kwa mara wanafunzi na walimu wao wanapofanya vizuri katika masomo

Anasema serikali haiwajali walimu wanaofundisha katika shule zake mna hivyo wamepoteza motisha na morali ya kufanya kazi, jambo linalohatarisha mustakabali wa sekta ya elimu nchini.

“Mwalimu wa shule binafsi akifaulisha wanafunzi wake kwa daraja A au B anapata motisha, lakini huku shule za Serikali wakipata A au sufuri hakuna kinachobadilika ndiyo maana wamekata tamaa na matokeo yake mmeona madudu katika matokeo ya kidato cha nne mwaka jana.

“Sasa kama hakuna tofauti yoyote kati ya mwalimu aliyesababisha sifuri katika wanafunzi wake na yule aliyeleta A nyingi unafikiri kuna atakayejituma? Na kama hakuna kujituma kupita kiasi, unafikiri nini kitafuata?”anahoji Mukoba.

Mukoba alizungumza na gazeti hili mara baada ya kuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya wanafunzi wa kidato cha sita ya Shule ya Sekondari Tusiime iliyoko Tabata jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye mahafali hayo, Mkurugenzi wa shule hizo, Albert Katagira, aliiomba Serikali ishirikiane na wamiliki wa shule za watu binafsi kufahamu siri ya shule hizo kufanya vizuri kila mwaka.

“Tunaomba Serikali itutambue na ituthamini sisi watu wa shule binafsi na wakifanya hivyo watajua siri ya shule zetu kufanya vizuri kila mwaka, unajua ukiwa na walimu wazuri na watumishi wenye moyo na kazi lazima wanafunzi watafaulu tu,” alisema Katagira.

Alisema Shule ya Msingi ya Tusiime katika matokeo mwaka jana ilikuwa ya kwanza kiwilaya na ya pili kimkoa na kwamba hali hiyo inasababishwa na moyo wa kujituma walionao walimu.

Mukoba anazungumza kwa mifano na kusema; “walimu ni sawa na jeshi lililokata tamaa, “kwa mfano ukimpa silaha mwanajeshi aliyekata tamaa na kumwamrisha aende vitani hivi unatarajia matokeo gani kama si kushindwa hiyo vita?” anahoji.

Akizungumzia uamuzi wa serikali kutaka kuwafanyisha mitihani walimu wa shule za msingi katika masomo ya Hisabati na Kiingereza, Mukoba alisema CWT haikubaliani na uamuzi huo kwa vile uko kinyume cha taratibu.

“Kwenye taaluma ya ualimu kuna kitu kinaitwa aptitude test ambayo ndiyo kipimo cha walimu. Kuna namna ambayo walimu hupimwa viwango vyao katika jinsi iliyokubaliwa kitaaluma na namna hiyo ni aptitude test.

“Unapompa mwalimu mtihani wa darasa la saba maana yake nini? Akifaulu sana unampa nini? Unamwongeza cheo au unampa zawadi au anajiunga na chuo kingine? Na akifeli unamfanya nini wakati kwa mfano kwenye aptitude yake anaonekana amefanya vizuri?

“Uamuzi huu wa serikali hauwezi kukubaliwa na CWT. Walimu hawaogopi mitihani lakini wanachotaka ni kuheshimiwa kwa taaluma yao. Maamuzi kama haya (ya kuwafanyisha mitihani walimu) hutolewa tu na watu wasioheshimu taaluma za wenzao,” anasema.

Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita katika uzinduzi wa Mpango wa Mafunzo ya Walimu Kazini kwa Elimu ya Msingi (MWAKEM), ambayo yatakuwa yakitolewa katika ngazi ya shule, Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema mitihani hiyo itakuwa na lengo la kupima uwezo wa walimu.

Dk Kawambwa alisisitiza akisema: “Mimi kama Waziri kuna siku wanafunzi wa darasa la saba wakimaliza mtihani wao wa kuhitimu elimu ya msingi kwa masomo haya, nami nitawaita walimu wa shule husika ili wafanye mtihani huo huo tuone kama uwezo wa walimu wetu ni mkubwa.”

Alisema walimu wanatakiwa kujiongezea zaidi maarifa, hivyo wanoe zaidi ‘silaha’ zao ili wawe mahiri katika ufundishaji wa Hisabati na Kiingereza, hali itakayowafanya pia wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao.

0
No votes yet