Tatizo si makocha ni mfumo mbovu


Elius Kambili's picture

Na Elius Kambili - Imechapwa 19 October 2011

Printer-friendly version

TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars, kwa miaka 31 sasa haijafuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika. Kwa nini?

Baadhi ya wadau wa soka nchini wanasema tatizo ni kiwango kidogo cha wachezaji waliopo na wapo wanaodai inatokana na kuongozwa na viongozi ‘wasio’ wa mpira.

Wengine wanadai makocha wa kigeni hawafai. Kigezo chao ni kwamba Taifa Stars ilipofuzu kwa mara ya kwanza mwaka 1980 ilikuwa chini ya makocha wa kizalendo, hayati Paul West Gwivaha na Joel Bendera.

Wadau wengine wanasema mfumo mbovu wa soka ndiyo kikwazo namba wani. Tangu mwaka 1980 hadi sasa, si makocha wa kigeni wala wazalendo waliofanikiwa kuiepeleka Taifa Stars kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika wala Kombe la Dunia . Kwa nini?

Pamoja na jitihada mbalimbali za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha soka yetu inapiga hatua, hali bado ni mbaya na hakuna dalili za Taifa Stars kufanya vizuri.

Tatizo ni mfumo mbovu wa kubaini wachezaji, kulea vipaji, kuvikuza chini ya misingi halisi ya uendelezaji soka. Jambo pekee la kufanya ili Taifa Stars isiendelee kufanya vibaya katika michuano mbalimbali ni kurekebisha mfumo huu mbovu wa soka ambao wachezaji wengi wanapatikana bila kuwa na msingi thabiti wa soka.

Tanzania imewahi kufundishwa na makocha wengi wa kigeni ambao walijitahidi kadiri ya uwezo wao kuhakikisha Taifa Stars inafanikiwa kufanya vizuri katika soka Afrika, lakini matokeo yamekuwa machungu kwa mashabiki wa soka nchini.

Mathalani, makocha wote wa kigeni walioifundisha Taifa Stars kuanzia mwaka 2000 wameshaingia katika lawama kwa kushindwa kuhakikisha Taifa Stars inafuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika.

Lawama hizo zilipungua kidogo baada ya Mbrazili Marcio Maximo kuiwezesha Taifa Stars kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani mwaka 2009 huko Ivory Coast.

Hebu tujiulize ni kweli makocha, TFF na serikali ndiyo pekee wanaohusika katika maendeleo mabovu ya soka nchini? Harakaharaka majibu ni ndiyo ‘mchawi’ wa soka ya Tanzania ni TFF na serikali.

Hao ndio wenye jukumu la kutengeneza mfumo bora wa ufuatiliaji wa vipaji hadi ngazi ya chini ya vijiji. Serikali ndiyo yenye viwanja (vya shule vingi vibovu) na TFF, ikisaidiwa na vyama vya soka vya mikoa na wilaya, ndiyo inaandaa taratibu nzuri za michuano ya wakubwa na vijana.

TFF ikiwa na michuano ya vijana katika ngazi ya taifa, mikoa na wilaya pia itakuwa na michuano hiyo. TFF ikipuuza uwepo, ubora na umuhimu wa michuano hiyo, mikoa na wilaya itapuuza pia.

Wachezaji bora hawaibuki ukubwani, wanaandaliwa kuanzia wakiwa wadogo, na michuano hiyo, kama ya Umitashumta na Umisseta ikisimamiwa vizuri na kuchezeshwa na waamuzi wajuzi itatoa nyota.

Historia ya mafanikio ya Taifa Stars mwaka 1980 ndivyo inaonesha hivyo, kwamba wachezaji walitokana na mfumo mzuri uliowalea wa Umisseta na klabu kuwa na timu za vijana.

Hakuna muujiza katika soka. Hata Nigeria baada ya enzi za kina Samson Siasia, ilisubiri kwa miaka kadhaa kupata akina Nwankwo Kanu ambao sasa wanaachia kina Peter Odemwingie watawale katika mpira wa miguu.

Aidha, Ghana walipotoka kina Abedi Ayew ‘Pele’ wakaja kina Samuel Kuffour na sasa wapo kina Michael Essien.

Hata kama Nigeria haijafuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 20212, soka yao imepiga hatua na vijana wengi kutoka nchi hiyo wamejazana katika miji mbalimbali ya Tanzania wakitafuta nafasi za kucheza soka.

Siri ni moja tu inayowainua wenzetu, uwepo wa shule kadhaa za kukuza vipaji vya soka na mawasiliano mazuri kati ya klabu za Ulaya na mawakala wa soka kutoka nchi husika ambapo wengi wao ni wachezaji wakongwe wa nchi hizo waliotamba katika soka Ulaya.

Wakati wenzetu wana ‘academy’ kadhaa za kukuzia vipaji vya soka, academy za Tanzania ni chache na inayoweza kujivunia mafanikio kiasi ni Rollingstone ya Arusha.

Wachezaji wengi wanatokea katika timu za mitaani zinazofundisha vijana bila ya kuwa na wataalam wa soka, hivyo chipukizi wengi hukosa misingi ya soka.

Baadaye chipukizi hao ndiyo wanaoitwa kwenye klabu za daraja la kwanza kasha Taifa Stars. Baada ya vijana hao kuitwa Taifa Stars ndipo huanza kufundishwa mambo ya msingi badala ya mbinu.

Kwa mfumo huu, makocha wa kigeni akiwemo Jan Poulsen raia wa Denmark hupata wakati mgumu wa kuwaelekeza wachezaji wasiokuwa na elimu ya msingi wa mpira wa miguu.

Kwa wastani, Taifa Stars hukaa kambini si zaidi ya wiki mbili kabla ya mechi ya kufuzu. Katika muda huo Poulsen atagundua tatizo, atafundisha namna ya kupiga pasi kisha atatoa mafunzo ya mfumo wa uchezaji. Hili ni tatizo, kwani kocha wa timu ya taifa anapaswa kufundisha mfumo tu wa kiuchezaji.

Hii ndiyo sababu baadhi ya wadau wanawalaumu wachezaji, wengine makocha na wengine shirikisho la soka na serikali, na sasa wengine wanapendekeza mkurugenzi wa ufundi wa TFF, Sunday Kayuni aondolewe.

0713 801 699
0
No votes yet