TBC1 ilivyojikwaa kwa Dk. Slaa


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version
Uvumi na siasa za njiapanda
Dk. Willibrod Slaa

VYOMBO vya habari – kwa mfano magazeti, redio na televisheni – vikifungwa au vikinyamaza, ni wapi wananchi watakimbilia kupata taarifa sahihi?

Soma hapa: Hawana pa kukimbilia; bali fursa mwanana hujitokeza na kujaza pengo. Ni fursa ya uvumi unaibuka, kuenea kwa kasi ya moto wa kiangazi na kuaminika zaidi.

Chukua mfano huu: Waziri Mkuu Mizengo Pinda anawasilisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni. Hotuba inatangazwa nchi nzima kupitia 'televisheni ya umma' – TBC1.

Dakika chache baada ya hotuba ya waziri mkuu, spika anamwita Dk. Willibrod Slaa, msemaji wa upinzani katika masuala ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Wakati Dk. Slaa anawasilisha bajeti mbadala, televisheni ya umma haipo hewani. Kulikoni? Mwezi mmoja na siku nne baadaye, anajitokeza mkuu wa televisheni ya umma. Ana ujumbe. Huu hapa.

Anasema na kunukuliwa na vyombo vya habari kwamba anasikitika kuwa TBC1 iliugua mafua ghafla na 'kushindwa' kutangaza hotuba ya Dk. Slaa.

Vyovyote ilivyokuwa, hotuba ya Dk. Slaa haikusikika na kuonwa moja kwa moja. Waliokuwa wakisubiri Pinda amalize wapate upande wa pili, walijawa na maswali mengi.

Hata wabunge wa chama cha waziri mkuu, baada ya kujua ukimya wa ghafla, walipigwa na mshangao na wengine kusema, 'Kwa mtindo huu wananchi watasema sisi ni woga.'

Katika kipindi cha mwezi mmoja na siku nne, wananchi wamekuwa wakilishwa kauli mbalimbali kutoka kwa watu mbalimbali juu ya mitazamo mbalimbali kuhusu watu mbalimbali waliofanya vitu mbalimbali kwa sababu mbalimbali za kuzuia Dk. Slaa asisikike akisema mambo mbalimbali.

Huo ndio uvumi. Hivyo ndivyo uvumi hufanya kazi. Ni hivyo jamii hulishwa, kwa kasi ya radi, kile ambacho waanzilishi wa uvumi huwa wamedhamiria kusambaza.

Kwa kudhamiria au hata bila kudhamiria, waanzilishi wa uvumi wanakuwa wameziba pengo lililoletwa na upungufu na kukosekana au kuondolewa kwa taarifa ambayo jamii ilikuwa ikitegemea.

Lakini kila uvumi huwa na chembechembe za ukweli. Katika kilicholeta mafua ya ghafla kwa TBC1 kuna ukweli kwamba hotuba ya Dk. Slaa ililenga kutoa darasa kwa waziri mkuu.

Ni hotuba iliyosheheni taarifa za kupingana na kauli za waziri mkuu kiasi kwamba wasikilizaji wengi wangeona amedhalilishwa.

Pamoja na mengine, ilikuwa hotuba ya takwimu juu ya wanaodaiwa kuwa mafisadi – watu binafsi na makampuni – viwango vya fedha vilivyokwapuliwa, hundi kwa malipo mbalimbali na mabenki ambamo malipo yalifanyika.

Ukifikia hatua hii ya chembechembe za ukweli ndipo unakumbana na maswali: Nini kilisababisha TBC1 kutotangaza hotuba ya Dk. Slaa?

Twende taratibu katika kupitia majibu kutoka mtambo wa uvumi. Hapa kuna huyu anayesema: Uongozi kutoka juu uliagiza, 'Kata mara moja.'

Uongozi wa juu ni wa akina nani? Tido Mhando, Mkurugenzi Mkuu wa TBC? Utaambiwa kuwa Tido naye anaamuriwa.

'Si yule waziri wa habari George Mkuchika? Alitoa amri kwa Tido kwamba Pinda akimaliza, basi kata; akisisitiza kwamba serikali haitaki kusikia kiongozi wake akidhalilishwa na vineno vya upinzani,' nyongeza hiyo.

Hapa kuna mwingine. Huyu anasema amri ya kukata matangazo ilitolewa na ikulu. Hasemi nani huyo ndani ya ikulu: Rais, Katibu Mkuu Kiongozi au Mkurugenzi wa Mawasiliano Salva Rweyemamu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi ya TBC?

'Mimi sijui nani alisema, lakini taarifa nilizonazo ni kwamba amri ilitoka ikulu. Unajua, ilifahamika kuwa hotuba ya Slaa imejaa mambo ya EPA, Richmond, Meremeta, Tangold na takwimu ameapa kuzimwaga hadharani,' anaeleza huyu ambaye ni mbunge kwa vipindi vitatu sasa.

Anasisitiza kwa kuuliza, 'Wewe hukumbuki Slaa anavyojibizana na polisi kwamba ana nyaraka nyingi za serikali? Si za kuumbua hizo? Sasa aachwe kuzimwaga hadharani mbele ya luninga? Unadhani watawala ni wajinga?'

Ndani ya bunge nako mambo yanachemka. Wabunge wanajiuliza. Unakuja uvumi kuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma ilimwita Tido Mhando na kumuuliza kwa nini TBC1 haikutangaza hotuba ya Dk. Slaa.

Wakati hawa wanasema Tido alijitetea kuwa mitambo iliharibika, wengine wanasema alipata wakati mgumu na kuomba radhi na kusema, 'Naomba yaishe wazee wangu.'

Aidha, taarifa ya Tido ya kuomba radhi, aliyotoa siku 34 tangu siku ya tukio ambalo wengi wameanza kuita 'kashfa,', inatajwa kulenga kusaidia waziri wa habari.

Tido ameomba radhi zikiwa zimebakia siku mbili tu waziri wa habari kuwasilisha bajeti yake bungeni. 'Huku ni kujikosha tu. Huoni kuwa amelenga kusaidiana na waziri? Kesho ndio waziri anawasilisha bajeti yake,' alisema mmoja wa wafuatiliaji wa masuala ya bunge mwishoni mwa wiki.

Serikali imefikishwa pabaya, anasema mama mmoja na kuongeza, 'kama serikali inaogopa hata yale ambayo hayajasemwa, basi inakwenda mrama.'

Kwa ufupi, kuziba taarifa au habari ni kuandaa mazingira ya kuibuka kwa uvumi. Uvumi unaweza kuwa wa viwango vidogo, vya kati na vikubwa kuhusiana na somo husika wakati huo.

Uvumi huweza kunufaisha aliyeusababisha au kumdhoofisha na hata kumwangamiza. Kitendo kama kile cha TBC1, kwa kukusudiwa au bila kukusudiwa, kina madhara makubwa kwa watawala kwani uvumi unaotokana nacho hudhoofisha kwa kasi isiyomithilika.

Vivyo hivyo kwa chombo cha habari ambacho kimepatwa na mkasa au ambacho kimetumika kuzima habari au taarifa. Hiki huandamwa na uvumi mkali na hadhi yake kufifia na hatimaye kufa.

Hii ndiyo maana, kwa watu makini, chombo cha habari kikipatwa na mkasa, sharti kiweke wazi na mara moja, kile kilichokisibu na kutoa maelezo yasiyo na chembe ya mashaka.

Kwa TBC1kuwasha mitambo kumdaka na kumtagaza waziri mkuu, lakini kuzima au kuzimika na kumzamisha Dk. Slaa, ni jambo linalotoa mwanya kwa uvumi uangamizao.

Labda hili laweza kuwa somo kwa vyombo vyote vya habari na ushauri wa bure kwa wahusika ili kuepuka siasa za njiapanda katika vyombo vya habari.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: