TBC sasa kwa fukuta


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 29 December 2010

Printer-friendly version

MKATABA wa ubia wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kampuni ya China ya Star Communication Network Technology Co. Ltd (Star Com), umeanza kuisumbua serikali, MwanaHALISI imegundua.

Wabia hawa wawili waliunda kampuni ya Star Media (Tanzania) Ltd., ili iweze kutekeleza makubaliano kati yao.

Hata hivyo, habari kutoka China zinasema Star Com ni kampuni “changa sana,” isiyokuwa na ofisi yake ya kujenga na hadhi ya kimataifa ya kuweza kuingia ubia nchi za nje.

Kwa upande wake, Star Media ilikuwa ifanye mabadiliko ya mfumo wa utangazaji wa analogi uliokuwepo na kuingiza mfumo mpya wa digitali unaotumika katika mifumo mingi ya utangazaji wa kisasa.

Lakini hivi sasa, taarifa za kuaminika ndani ya serikali na TBC kwenyewe, zinasema serikali inakataa kuidhamini kampuni ya Star Media ili iweze kukopa fedha benki kwa ajili ya kutekelezea kazi iliyopewa.

Ili kampuni hiyo itekeleze majukumu yake ya kimkataba, inadai sharti ikope fedha kwa kudhaminiwa na serikali kama inavyoruhusiwa chini ya mkataba wake na serikali wa 30 Novemba 2009.

Sharti la kudhaminiwa ili kampuni ikope limo katika kifungu cha kwanza cha mkataba kinachosema, “Motisha kwa uwekezaji – sehemu ya 1.1.4.”

Kifungu hicho kinasema, “Dhamana ya serikali itatolewa kwa ajili ya mtekelezaji wa mkataba – Star Media – kupata kukopa Benki ya China Export & Import au Benki ya Maendeleo ya China (CDB).”

Mkataba ambao MwanaHALISI imeona, unaonyesha kuwa katika “Mpango wa Uwekezaji na Uwezeshaji TBC wa 2009,” Star Media itawekeza mtaji wa dola 238 milioni, kati yake, dola 68 milioni zitatokana na mkopo.

Kimgawanyo, dola 34 milioni zitatokana na thamani ya hisa 10,000 za wabia hao; wakati Star Media yenyewe itapata dola 136 kutoka vyanzo vyake vya mapato.

Kulingana na vyanzo vya habari vya MwanaHALISI, serikali imegundua kuwa Star Media haina uwezo kifedha.

Kwa msingi huo, serikali inasita kudhamini kampuni hiyo kukopa fedha benki kwa hadhari kuwa huenda ikashindwa kuzirejesha.

Lakini kwa kuwa dhamana ni moja ya makubaliano katika mkataba, kitendo cha serikali kukataa udhamini kinachukuliwa kuwa ni ukiukaji mkataba.

Mazingira haya yanaiweka Star Media katika nafasi ya kudai kile unachoita haki yake, hata kwa kufungua malalamiko Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya kibiashara (ICC) iliyoko The Hague, Uholanzi, ambako mkataba wao unasema maamuzi yake yatakuwa ya mwisho.

“Hapa ndipo penye tatizo. Inaonekana serikali imeanza kushtukia kampuni hii. Lakini hakuna njia nyingine ya kufanya zaidi ya serikali kudhamini mkopo huo kama ilivyojifunga katika mkataba,” anasema kiongozi mmoja wa serikali.

Amesema, “Ni kwa kujua hilo, ndiyo maana Wachina wameamua kushinikiza kupewa fedha ili serikali igome na wao wakimbilie ICC,” amesema kigogo huyo asiyetaka jina lake litajwe gazetini.

Kuibuka kwa mvutano huu wa ndani kwa ndani na kimyakimya, kumekuja mwezi mmoja baada ya serikali “kushindwa” katika shauri lililofunguliwa mahakama ya kimataifa ya usuluhishi na kampuni ya Dowans Tanzania Limited.

Kwa mujibu wa uamuzi wa shauri hilo, serikali inatakiwa kulipa Dowans, ambayo ilirithi mkataba wa Richmond Development Company (RDC), kiasi cha Sh. 185 bilioni.

Makubaliano ya TBC/Star Media yamezaa kitu kipya kiitwacho Star Time kinachoshughulikia uuzaji wa ving’amuzi kwa wateja wanaounganishiwa matangazo ya TBC ya mfumo wa digitali.

Mradi huo umeingia utata mkubwa kwa kuwa kampuni ya China imegoma kusaini mkataba wa pango katika majengo ya TBC na matumizi ya minara na viwanja vya shirika hilo

Taaraifa zinasema hadi sasa Star Time inadaiwa Sh. 300 milioni huku Mamlaka ya Kodi ya mapato (TRA) ikiwakaba koo kwa kuwadai Sh. 2.2 bilioni zikiwa kodi ya mapato kwa biashara zake nyingine.

Kampuni ya Star Time inajenga majengo yake, ndani ya viwanja vya TBC, bila kuwa na vibali vya ujenzi kutoka mamlaka husika nchini au kujisajili kwa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (ERB).

Taarifa za ndani zimedaia kuwa wafanyakazi wengi wa kichina kwenye miradi ya Star Time hawana hati za kufanya kazi nchini. Kati ya wafanyakazi 32 Wachina, ni watano tu wenye hati hizo zinazotolewa na Kamisheni ya Kazi.

Hofu inayowakumba Wachina ni kwamba wafanyakazi wasiokuwa na vibali wanaweza kunyimwa vibali hivyo kwani kazi zao zinaweza kufanywa na Watanzania.

Mkataba wa TBC na Star Media ulioidhinishwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa Mkurugenzi wake mtendaji, Emmanuel Ole Naiko kusaini upande wa serikali, unataka wafanyakazi wa TBC wafundishwe namna ya kuendesha mitambo na kurusha matangazo kwa njia ya digitali.

Juni mwaka jana, serikali iliridhia TBC, chini ya utawala mpya wa mwandishi wa siku nyingi Mtanzania, Tido Mhando, ifanye kazi na kampuni ya Star Com ya China.

Kwa mujibu wa mkataba, pande hizo mbili zilipaswa kuwa na mradi wa pamoja baada ya Star Com kuuziwa hisa 6,500 huku TBC ikibaki na hisa zake 3,500. Hii ikiwa na maana kuwa TBC inamiliki hisa 35 dhidi ya 65 za Star Com. Kila hisa kati ya hizo 10,000 ina thamani ya dola 100.

Nayo Star Media ilisajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni na Biashara (BRELA) 26 Juni 2009 na kupewa hati Na. 71639. Imedhaminiwa kwa dola 1 milioni.
Novemba mwaka jana, MwanaHALISI liliripoti kuwa mchakato wa kumpata mbia wa TBC, haukushirikisha taasisi muhimu za kiserikali.

Hizi ni pamoja na Msajili wa Hazina, mwenye jukumu la kutunza – kama mwakilishi wa serikali – kumbukumbu za mali na huduma za serikali, mashirika, wakala na makampuni; na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA).

Wakati ule, gazeti hili lilielezwa na ofisi ya Msajili wa Hazina, “Hatuna taarifa za kuuzwa hisa za TBC kwa kampuni ya China.”

Nao PPRA, kupitia ofisa wake mwandamizi, walisema, “Tuliombwa tu ushauri tukatoa. Tuliwaeleza mapendekezo yetu. Nini walikifanya na kipi hawakukifanya, hatuwezi kujua.”

Naye Tido Mhando alipoulizwa alisema, “Mamlaka zote zinazotakiwa kufahamu mchakato huo zimejulishwa. Yeyote anayetaka kujua suala lolote kuhusu ubia wa TBC na kampuni ya Kichina, aende kwenye mamlaka hizo.”

Aliyekuwa waziri wa habari, George Mkuchika, ambaye hakupatikana juzi kutoa maoni yake, aliwahi kudai kuwa “Taratibu zote zilizingatiwa,” akikanusha habari iliyoandikwa na gazeti hili.

Mkuchika ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), alisema baada ya kutembelea Beijing, China iliko Star Com, wataalamu wa TBC na katibu mkuu wa wizara (Tanzania) kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini China, walijiridhisha na uwezo wa mbia na kwamba alipitia mkataba kabla ya kusainiwa.

Hata hivyo, MwanaHALISI iligundua mkataba huo haukuwahi kuwasilishwa Baraza la Mawaziri ili kupitiwa na kuidhinishwa rasmi. Hilo lilikuwa ni jukumu la waziri Mkuchika akisaidiana na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.

Kadhalika, mkataba haukupata kuangaliwa katika mtizamo wa kisheria kwa kuwa haukupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mshauri mkuu wa kisheria wa serikali.

Sasa yameibuka malalamiko kwamba mradi wa hivi karibuni wa kuuza ving’amuzi, unaoendeshwa na kampuni ya Star Media, haujaidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi ya TBC.

Imedaiwa pia kuwa wajumbe wa Bodi ya Star Media waliteuliwa kinyemela na menejementi ya TBC badala ya Bodi ya TBC.

Pia hakuna hata mjumbe mmoja wa Bodi ya TBC na Star Media mwenye ujuzi wa kuendesha au kutengeneza mitambo hiyo.

Ndani ya kampuni ya Star Media hakuna mtu yeyote wa TBC ambaye anadhibiti mapato na matumizi ya kampuni hiyo.

0
Your rating: None Average: 2.5 (2 votes)