Tendwa alifunikwa kwa rushwa ya bia 2005


Maureen Urio's picture

Na Maureen Urio - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa ameporomosha bomu zito linalojeruhi hadhi yake na kukichafua kabisa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tendwa anasema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, alikula rushwa na amethibitishia ulimwengu kuwa wagombea uongozi kupitia CCM wamekubuhu kwa rushwa.

Kuthibitisha kuwa uchaguzi wa mwaka 2005 ulikithiri kwa rushwa, Tendwa anasema alikuwa miongoni mwa waliohongwa na baadhi ya wagombea kupitia chama hicho. Kwa hiyo, Tendwa alikula rushwa ya wagombea wa CCM.

“Mimi mwenyewe katika uchaguzi wa mwaka 2005 nilikula rushwa; tulikuwa huru katika hilo. Nilikuwa naambiwa ‘chukua katoni ya Heinken hizo nenda nyumbani;’ kwa kweli hali ilikuwa mbaya,” alinukuliwa Tendwa na gazeti la kila siku la Nipashe la 30 Septemba 2010.

Sheria za nchi zinakataza kutoa na kupokea rushwa, lakini ili kukwepa sheria hiyo, serikali ya Awamu ya Tatu iliwasilisha bungeni muswada uliopitishwa kuwa sheria iliyobariki matumizi ya zawadi (takrima) kutoka kwa wagombea wakati wa uchaguzi.

Wanaharakati wa asasi za utawala bora na demokrasia walipinga mahakamani wakitaka sheria hiyo ifutwe.

Sheria hiyo iliyotetea ‘zawadi’ kama kitendo halali cha kuonyesha ukarimu wa ‘Kiafrika’, ilifutwa na Mahakamu Kuu, Aprili 2006.

Tendwa katika mazungumzo yake na waandishi wa habari waliokuwa kwenye mafunzo ya kuboresha taaluma ya habari yaliyosimamiwa na Media Focus in Africa wiki iliyopita, alisema alikula rushwa ya bia aina ya Heinken, siyo takrima.

Kwa hiyo, Tendwa alitenda kosa la jinai. Je, heshima na uadilifu wake si wa kutiliwa shaka hasa katika kipindi hiki anapoongoza ofisi inayosimamia Sheria ya Matumizi ya Gharama za Uchaguzi?

Je, mtu asiye na uadilifu anaweza kuaminiwa kusimamia uadilifu wa watu wengine? Nani ataamini kwamba hali tena rushwa!

Msajili wa Vyama vya Siasa alijitolea mfano yeye katika kuthibitisha kwamba rushwa ilikithiri. Miaka mitano baadaye anakiri alipokea rushwa huku akiwa msajili wa vyama tangu mwaka 2001 alipoteuliwa kuchukua nafasi ya msajili wa kwanza wa vyama vya siasa, George Liundi.

Tendwa amefanya kazi ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kwa muda wa miaka 23, hivyo ni mwanasheria. Kama msajili alipokea rushwa mwaka 2005. Je, heshima yake haiwezi kutiliwa shaka? Anaweza kuthubutu leo kuwakamata watoa rushwa?

Aidha, Tendwa anathibitisha wazi kuwa uchaguzi wa mwaka 2005 haukuwa wa haki kwa sababu ulitawaliwa na rushwa ambayo yeye mwenyewe alishiriki, lakini kwa wakati ule hakutoa taarifa yoyote; aliona sawa tu. Inawezekana Taasisi ya Kuzuia Rushwa wakati huo - Takuru (sasa TAKUKURU) iliona haya na kukaa kimya.

Kauli ya Tendwa kwamba alikula rushwa inamwonyesha kuwa siyo mtu anayestahili kusimamia ofisi hiyo nyeti. Anaweza kuwaonea haya wagombea waliompa rushwa na wakashinda mwaka 2005.

Hili linajidhihirisha hivi: Katika mazingira ya kutatanisha, wiki mbili zilizopita, Tendwa aliingilia kazi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kulegeza muda wa kufunga mikutano ya kampeni kutoka saa 12.00 jioni hadi saa 1.00 usiku. Alilenga kunufaisha wagombea wa CCM.

Tendwa anaonekana kupindisha hata sheria mpya ya matumizi ya gharama za uchaguzi kwa kutupilia mbali madai yaliyowasilishwa na wapinzani kwamba CCM imeangiza vifaa vya kampeni nje ya utaratibu.

CCM wanaweza kumwamini Tendwa kwa sababu anawalinda, lakini Watanzania hawawezi kumwamini. Kama alishawahi kupokea rushwa na kunyamaza, basi kuna mengi anayoficha kwa lengo la kuwabeba CCM.

Katika kura za maoni kupata wagombea wa ubunge na udiwani kupitia CCM, TAKUKURU iliwataja wagombea wengi kuwa wamenaswa. Baada ya baadhi yao kuwa wakali, waume zao kutishia kuiumbua TAKUKURU, ni mshindi wa Iringa Mjini, Frederick Mwakalebela na Joseph Mungai wa Mufindi waliofikishwa kortini.

TAKUKURU imechuja majina ya watuhumiwa, kwa hiyo Tendwa hawezi kuwa na ushahidi wa kuthibitisha mawaziri au wagombea waliotoa rushwa wakati wa kampeni na hivyo kuwaengua.

Hii yaweza kuwa ghiliba katika juhudi zake za kuwapaka wananchi mafuta kwa mgongo wa chupa kuwa yuko makini na kazi yake, wakati amedhihirisha kazi yake ni kuwafunika watuhumiwa wa rushwa.

Hivi Tendwa anaweza kweli kuthubutu kuwatoa madarakani viongozi walioingia katika majimbo kwa rushwa baada ya uchaguzi kama anavyosema? Mbona hakutoa hata taarifa juu ya waliopita kwa njia hiyo 2005?

Anaweza kweli kuukabili mfumo uliomteua kuwa msajili? Mgombea urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete amewasafisha wagombea wote kuwa safi, wachapakazi na wanaostahili kuchaguliwa tena. Tendwa atapata wapi ujasiri kuwaumbua wateule wa bosi wake?

Hawezi maana ameonyesha wazi kuwa si mwaminifu, alipokea rushwa akijua wazi kuwa anavunja sheria na anastahili kuadhibiwa. Hawezi kuwa mfano wa kuigwa na hafai kusimamia masuala yoyote ya uchaguzi.

Tena anaendelea kutetea vitendo vya rushwa kwa kuwatetea wanaopokea rushwa kuwa hawana hatia kwa kusema kuwa wale wanaopokea hawana uelewa wa kutosha na hawajui athari zake. Je, hajui ni sheria anayopaswa kutumia ambayo inasema kutojua sheria siyo kinga?

Kama Tendwa hakuweza kukataa rushwa ya pombe na hadi sasa “anajivunia Heinken;” kama bado anaingilia Tume ya Uchaguzi ili kuibeba CCM; hawezi kuona magari ya serikali yakibeba nyama ya nyati, vitenge kwa ajili ya rushwa; na hawezi kuona magari ya serikali ambayo yanambeba Salma Kikwete.

Tendwa alistahili kujiuzulu kazi zamani; hasa pale nafsi yake ilipomsuta kuwa alipokea rushwa. Alistahili kujiondoa katika ofisi hii baada ya kugundua kuwa ni mchafu.

Tendwa hasafishiki kwa kuongea na waandishi wa habari kwa njia ya porojo. Kujisafisha ni kuondoka katika ofisi hiyo, tena kwa kujutia na kuomba kazi nyingine. Vinginevyo anataka kusema kuwa “hivi ndivyo sote tulivyo serikalini.” Sidhani hivyo.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: