Tendwa ana hamu ya kutenda jinai…


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version

JOHN Tendwa, msajili wa vyama vya siasa nchini, ana hamu ya kufuta vyama vya siasa kwa madai kuwa havina uwakilishi katika ngazi yoyote ya uongozi.

Amesema ofisi yake inafanya mchakato wa kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinasajiliwa upya kila baada ya miaka mitatu.

Msajili alitoa kauli hiyo wiki iliyopita wakati akifanya tathmini ya miaka 20 ya kuanzishwa tena kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Je, hivyo ndivyo sheria ya vyama vya siasa ya 1992 inavyosema?

Kwa mujibu wa sheria hiyo, hakuna kifungu kinachosema kuwa msajili atakuwa na mamlaka ya kusajili vyama na baadaye kuvifuta kama havina uwakilishi.

Sheria pia haimpi mamlaka ya kuvisajili vyama na kuvifuta kila baada ya miaka mitatu.

Mamlaka ambayo Tendwa anayo, kwa mujibu wa kifungu cha 19(1) cha sheria ya vyama vya siasa, ni kufuta usajili wa chama chochote cha siasa ambacho kitatenda kinyume cha sheria.

Sheria inaelekeza, pamoja na mambo mengine, kutotenda ubaguzi, udini wala ukabila; na kuendesha vyama kwa misingi ya kidemokrasia ikiwa ni pamoja na kuwa na vikao na uchaguzi kila baada ya muda maalum.

Chama pia hakitakiwi kuwa na sera zinazotetea kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania au matumizi ya nguvu katika kupata wanachama na kufanikisha malengo yake ya kisiasa.

Je, vyama ambavyo havina wawakilishi vimeleta hasara gani kwa taifa?

Zimefanyika chaguzi nyingi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini; lakini haijawahi kusikika kuwa vyama hivyo vinailetea hasara yoyote serikali.

Tendwa na ofisi yake, hawajawahi kutoa malalamiko ya vyama visivyo na wawakilishi kuiletea hasara serikali au kutoa mfano wa hasara hizo.

Vyama hivi vinajiendesha vyenyewe; ama kwa michango ya wanachama wake au ufadhili wa wenye mapenzi navyo.

Hata hivyo, vyama hivi ni asasi za kijamii zilizo makini katika kutoa elimu ya uraia na elimu kwa wapigakura.

Vimewezesha wananchi wengi kupata ufahamu juu ya masuala ya siasa na maendeleo katika maeneo yao na taifa kwa jumla.

Kadri elimu na maarifa, ambayo wananchi wanapewa au kushirikishwa inavyoongezeka, ndivyo wananchi wanavyoelewa zaidi na kudai haki yao ambayo Tendwa anaweza kuwa anaona ni “mashambulizi” kwa waliomteua.

Tendwa anadai kuwa vyama hivi vinaibuka wakati wa uchaguzi. Hata kama hilo ni sawa, hali hiyo haiwezi kuwa na madhara kwa wananchi wala serikali.

Aidha, serikali haina vipimo vya viwango vya “kazi za kisiasa” za chama cha siasa. Si Tendwa binafsi wala ofisi yake yenye majedwali ya kupimia kazi za siasa za vyama.

Hata hivyo, vyama vya siasa haviripoti wala kulazimika kuripoti kwa Tendwa au ofisi yake juu ya kazi zake za kisiasa isipokuwa juu ya mikutano na chaguzi zinazoleta mabadiliko ya viongozi.

Tendwa asivunje sheria.

0
No votes yet