Tendwa jivue koti la unafiki


editor's picture

Na editor - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MWISHONI mwa wiki iliyopita Msajili wa Vyama vya Siasa nchini John Tendwa alizionya taasisi za dini nchini zisiwe chanzo cha uchochezi kwa kupigia kampeni chama chochote cha siasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Msajili huyo amesema taasisi za kidini zinagusa roho za watu wote bila kujali vyama, na kazi zake kubwa ni kuhubiri amani, utulivu na kuwajengea watu wake maadili ya kiroho.

Lakini dini, mbali ya kuwalisha waumini wao chakula cha kiroho pia zimekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza na kuhudumia waumini wao kielimu, afya na kiuchumi.

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu, dini zimekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa wapigakura. Ndiyo maana kila dini ilijitahidi kutoa waraka kwa waumini wao kuelekeza sifa za kuzingatia katika kuchagua viongozi bora kwa miaka mitano ijayo.

Kama kuna dini iliyofikia hatua ya kuelekeza waumini wao wachague viongozi kwa misingi ya dini, huo utakuwa ukiukwaji wa taratibu na tutaungana na Tendwa kukemea dalili na viashiria vyote vinavyoweza kusababisha nchi yetu kujitumbukiza katika uvunjifu wa amani kwa sababu ya tofauti za kiitikadi.

Hata hivyo, tunamtaka msajili aonyeshe dhamira ya kweli katika kusimamia vyama na kulea demokrasia ya vyama vingi.

Tunasema hivyo kwa kuwa tunajua Tendwa amefikia hatua ya kutoa tamko hilo kwa vile asasi hizo za kidini na za kiraia zinatoa elimu ya uraia kwa wapigakura jambo linalokera chama tawala. Kisheria msajili hapaswi kuwa na chama, lakini anaegemea upande mmoja.

Mwaka 2000 Askofu Zachariah Kakobe wa Kanisa la Full Gospel alishutumiwa alipojitokeza kumpigia kampeni aliyekuwa mgombea urais kupitia chama cha Tanzania Labour Party, Augustine Lyatonga Mrema. Ulionekana udini.

Askofu Kakobe alipotangaza kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa mfuasi wake, Tendwa hakulaani kwamba kitendo hicho kingeathiri waumini wake; alichekelea.

Mwaka 2005, baada ya Jakaya Kikwete kuteuliwa na CCM kuwa mgombea urais, maaskofu walijitokeza na kusema ni chaguo la Mungu. Tendwa hakulaani kauli hiyo; alichekelea pia.

Ukweli kauli hiyo ilikuwa mbaya zaidi kuliko hata uamuzi wa Askofu Kakobe kumpigia kampeni Mrema mwaka 2000. Tamko la maaskofu lilimaanisha kwamba wagombea kutoka vyama vingine hawakuwa chaguo la Mungu.

Kama hawakuwa chaguo la Mungu walikuwa chaguo la shetani? Lakini leo askofu Kakobe anapoonyesha hisia zake dhidi ya mgombea kipenzi cha Tendwa anabadilika na kutoa tamko kulaani.

Tutakuwa wa kwanza kuungana na Tendwa ikiwa maaskofu au masheikh wanawaelekeza wafuasi wao kuchagua viongozi wa dini zao.

Msajili anapaswa kuelewa dini haziwezi kubaki zikihubiri mambo ya kiroho wakati waumini wao hawana afya nzuri, elimu nzuri na uchumi mzuri. Siasa ina athari kubwa katika masiaha yao.

Tukatae udini, ukabila na ubaguzi mwingine wa aina yoyote, lakini si elimu ya uraia kwa wapigakura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: