Tendwa kaanguka vibaya 


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Msajili wa Vyama vya  Siasa, John Tendwa

MIKUTANO na maandamano yalioitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika mikoa mbalimbali nchini sasa yameonyeasha dhahiri kumkera Rais Jakaya Kikwete, na amewajibu viongozi wa chama hicho kuwa tamko la kumtaka atatue matatizo na shida za wananchi katika kipindi cha siku saba, ni jambo ambalo halitawezekana.

Akihutubia taifa juzi katika hotuba ya mwisho wa mwezi wa Februari ambayo alizungumzia mambo matano, milipuko ya mabomu Gongo la Mboto; hali ya chakula nchini; bei ya sukari; hali ya umeme na hali ya usalama; Rais alionyesha dhahiri kutokukubaliana na maandamano ya CHADEMA.

Rais alionyesha kujibu changamoto iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilibroad Slaa, wiki iliyopita katika maandamano yao mkoani Mwanza kuhusu ugumu wa maisha unaokabili wananchi. Rais Kikwete alisema:

 “Hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa. Mzee Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii.  Na wale wa umri wangu au kunizidi wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang’atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri. 

“Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, Mzee Mkapa nae kakaa miaka 10 hakuyamaliza.  Mie nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano hayataisha yote.  Lililo muhimu kuliko yote ni kuwa katika kila awamu nchi yetu imekuwa inapiga hatua ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo.  Hali iliyokuwa wakati ule sivyo ilivyokuwa mwaka 1985, wala 1995 au 2005 na ilivyo sasa.  Katika miaka mitano hii kuna maendeleo yanayoonekana wazi.”

Kikwete alisema kuwa pamoja na changamoto nyingi, amefanya juhudi kubwa na mafanikio yanaonekana katika nyanja zote za maisha ya wananchi.     

Hakuishia hapo tu, alisema ni muhimu watu kutambua ukweli kwamba uchumi kama wa Tanzania ambao haujajenga uwezo wake wa ndani wa kujitosheleza kwa mahitaji yake, huathirika sana na yale yanayotokea katika uchumi wa dunia.

Rais Kikwete alisema uchumi wa dunia unapoyumba na wa Tanzania pia huyumba, bei za mafuta katika soko la dunia zikipanda na Tanzania pia gharama za uchukuzi na uzalishaji huongezeka na kusababisha bei za bidhaa kupanda.

Ni kwa maana hiyo alitaka CHADEMA kisiibebeshe serikali yake lawama hizo, kwani pamoja na changamoto zilizopo, serikali imekuwa kitafuta nafuu kwa kiwango inachoweza.

Ingawa Rais Kikwete hakubaliani na kauli za CHADEMA, lakini walau amejibu shutuma zilizoelekezwa kwake. Amefanya pengine kile ambacho mahafidhina wengi ndani ya serikali yake ama wasingependa kabisa Rais azungumzie hayo kwa kuwa kwao angeonekana kuwa anatii alichoambiwa na CHADEMA, au wengine labda bila kujijua wakimtaka ake kimya huku mambo yazidi kumwendea kombo. Kutoa kauli si jambo dogo.

Wakati Kikwete akitoa kauli hiyo, hakika wapo watu aina ya Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ambao wamejikuta katika aibu kubwa. Tendwa amenukuliwa na gazeti la serikali la Daily News, alisema kwamba kauli ya kumpa rais siku saba kujibu shutuma za hali mbaya ya uchumi, ni sawa na uhaini.

Hii ni kauli iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, mwanasheria ambaye amekomaa kufikia ngazi sawa na jaji wa Mahakama Kuu. Hii ndiyo inanisukuma kuandika makala haya huku nikijiuliza, hivi hawa ndio washauri wa rais waliomzunguka kushoto na kulia, wakijaribu kumpotosha ili asijibu mambo muhimu yanayoikabili serikali yake kwa kisingizio cha kutisha vyama vya siasa?

Sikupata kuwaza wala kudhani kwamba Tendwa angeweza kufikia hatua ya kuwa na fikra tenge kiasi hicho. Hakuna ubishi kwamba Tendwa ni mwerevu, walau wa sheria za nchi hii, zaidi sana sheria ya vyama vya siasa ambayo ni wajibu wake mkuu wa kuisimamia.

Ninaamini Tendwa anafahamu vilivyo vyama vya siasa kisheria vina haki ya kufanya mikutano ya hadhara, maandamano na wakati wote kueleza sera zao. Kikubwa kwa vyama vya upinzani ni kufichua udhaifu wa serikali na kuwakumbusha wananchi juu ya wajibu wa serikali iliyoko madarakani katika kutimiza majukumu yake.

Haya ni mambo ambayo Tendwa kwa uelewa wake, si magumu. Ni mepesi. Anayajua na sitaki kuamini kwamba mara hii amesahau kwa kuwa ndicho kitu alikuwa akikumbusha vyama vya siasa wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Leo nini kimempata Tendwa hadi kujikuta akieleza sera za chama, haki ya chama kujinadi kwa wananchi kwa mujibu wa sheria ni uhaini? Tendwa yuko na shinda ndani yake.

Lakini kinachonishangaza zaidi ni Tendwa kushindwa kusoma alama za nyakati. Tendwa si mgeni nchini, naamini anakumbuka vilivyo aibu waliyovuna wenzake wa aina yake serikalini.

Hawa ni pamoja na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema na hivi karibuni kabisa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja. Viongozi hawa wote kila mmoja kwa nafasi yake akiamini anamjibia rais Kikwete, walijikuta wanavuna aibu.

Kombani na Werema wakijibu kauli za wananchi za kutaka kuwapo kwa katiba mpya nchini, kwa tabia ile ile ya kihafidhina na kujisahau walisema Tanzania haihitaji katiba mpya kwa sasa kwa sababu iliyopo haina shida.

Siku chache baadaye Rais Kikwete akihutubia taifa katika salamu zake za mwaka mpya, alisema ameamua kuanza mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya. Hali hii kwa hakika iliwalowesha Kombani na Werema.

Lakini Werema alijiunga tena na Ngeleja katika aibu nyingine ambayo awali walikuwa wamezungumza kwa mbwembwe zote kwamba serikali ilikuwa imeamua kulipa fidia ya Sh. 94 bilioni kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans dhidi TANESCO kama ambavyo Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC) ilikuwa imeamua. Lakini Kikwete hakukubaliana nao. Aibu! Serikali imeunda kamati kutafuta jinsi ya ama kukwepa mzigo wa fidia hiyo au walau kuupunguza.

Kwa staili ile ile ya Kombani, Werema na Ngeleja sasa mzee mzima Tendwa naye anatumbukia kwenye mtego wa kumjibia Kikwete. Kwa Tendwa kumtaka rais ajibu madai katika kipindi cha siku saba ni uhaini, na haifai kutajwa chini ya mbingu, lakini aliyepewa changamoto husika, yaani Rais Kikwete, amejibu katika kipindi hicho.

Sasa Tendwa inabidi ajitafakari na kuiuliza anasimamia nini? Je, anamsaidia rais au ni utamaduni ule ule wa kihifidhina? Lakini haya yote yana maana gani hasa? Hivi akina Kombani, Werema, Ngeleja na sasa Tendwa wanaweza kusema kuwa wako sawa kama wasaidizi wa rais katika nafasi zao?  Hivi ni kwa nini bado wapo kwenye nyadhifa zao, wanaamini katika nini basi?

0
Your rating: None Average: 3.4 (5 votes)
Soma zaidi kuhusu: