TFF wanajua sababu za Yanga kususia


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version

KLABU ya Yanga iliyoingia kwenye michuano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati kama timu ya pili iliyotokana na Tanzania Bara kuwa wenyeji wa michuano hiyo, inaambiwa imehujumu michuano.

Katibu Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicolaus Musonye, amesimama kidete kueleza kwamba ni Yanga walioifanya michuano iharibike kinyume na matarajio.

Musonye anayefahamu vizuri siasa za mpira wa Tanzania, kwa kuwa amekuwa kiongozi wa CECAFA kwa miaka mingi, hajasema atafanya nini ikibainika kuwa ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waliochochea Yanga isusie mechi?

Viongozi wa Yanga wanasema yalikuwepo makubaliano ya maandishi kuwa Yanga na Simba zitapewa Sh. 50 milioni kila moja kwa kuwa ndizo zinazovuta watazamaji na hivyo kuingiza mapato makubwa kwenye michuano hiyo.

Haya ni makubaliano yanayotajwa kuwa yalifanyika mbele ya Musonye mwenyewe ambaye Jumapili alisikika akithibitisha kuwa palikuwa na matatizo lakini yalitatuliwa.

Kitu kimoja kimevuruga mambo. Viongozi wa Simba waliwageuka wenzao Yanga pengine kwa kuamini Yanga wasipokwenda uwanjani, wao watakuwa wameibuka kidedea.

Laiti Simba wangegoma kama Yanga, lazima mechi ingefanyika kwa kuwa TFF ingehangaika nao kwa majadiliano ili kuepuka kufedheheka na hatimaye kubebeshwa lawama na CECAFA.

Ni utaratibu wa michuano ya CECAFA kwamba chama kinachokuwa mwenyeji, ndicho huhusika na usimamizi wa mapato ya milangoni. Ndio maana michuano ilipofanyika nchini Rwanda, Shirikisho la Rwanda liliruhusu watazamaji kuingia uwanjani bure zilipocheza timu zao.

Mpaka michuano inamalizika, si CECAFA wala TFF walioeleza kwa ufasaha kilichosababisha kupangua ratiba iliyokuwa imeonyesha awali kuwa Simba na Yanga, iwapo zingepita kwenye robo fainali, zingekuja kukutana nusu fainali.

Sasa kama wao TFF na CECAFA walikuwa wa kwanza kukiuka kanuni za michuano wanayoisimamia, walitarajia Yanga baada ya kudanganywa kitoto, wafanye nini?

Pasingekuwa na makubaliano tangu awali –tunaambiwa yalifanywa siku nane kabla ya michuano – Yanga isingekuwa na namna yoyote ile ya kukwepa lawama kwa kutoingiza timu kwa ajili ya mechi ya kuamua mshindi wa tatu.

Kilichoisibu mechi hiyo ni kule viongozi wa TFF kutokuwa waadilifu kwa ahadi waliyoitoa kabla ya michuano na hata asubuhi ya siku ya mechi yenyewe.

Sawa, Yanga imeadhibiwa kwa kufungiwa kucheza michuano ya CECAFA kwa miaka mitatu na kulipa faini ya dola 35,000 ambazo kwa hesabu ya harakaharaka, ni sawa na Sh. 40 milioni.

Linakuja swali hapa: adhabu hiyo ndiyo imewafundisha viongozi wa TFF walioahidi kuzilipa Simba na Yanga fedha ili kuzisaidia kukidhi gharama za timu zao?

Hivi Watanzania wanatakiwa kuamini kwamba viongozi wa Yanga hawana akili timamu kiasi kwamba hawajui athari za kukosesha maelfu ya watazamaji burudani ndani ya uwanja?

Kwamba Yanga leo hawajui kuwa nyuma yao kuna kundi kubwa la washabiki waliotaraji kuona timu yao inaingiza kikosi kabambe uwanjani na kuvuna dola 10,000 za mshindi wa tatu!

Hofu yangu ni pale viongozi wa Yanga watakapokuja na vielelezo vya makubaliano waliyoyafanya kwenye kikao na TFF pamoja na Simba. TFF watasema nini?

Hadi sasa, Watanzania hawajaelezwa sababu za viongozi wa Simba, hasa Omary Gumbo na Mohamed Mjengwa, waliokuwepo kwenye kikao na Yanga, TFF na CECAFA, kutokuwepo uwanjani kushuhudia mechi.

Mtu anaweza kufahamu haraka kwanini viongozi wa Yanga akiwemo Mwenyekiti Imani Madega, Katibu Mkuu wake, Lucas Kisasa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Emanuel Mpangala, hawakufika uwanjani, maana walishaamua kutopeleka timu.

Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wa Yanga, Francis Lucas, Gumbo na Mjengwa waliiwakilisha Simba kwenye kikao cha pamoja na Yanga, TFF na CECAFA huku Yanga ikiwakilishwa na Kisasa na Mpangala.

Wakati tunajiandaa kwenda mitamboni, viongozi wa Yanga Mwenyekiti wa Yanga ambaye ni mwanasheria kitaaluma, mpaka tulipokuwa tunajiandaa kuingiza mtamboni gazeti, alikuwa anakusanya nguvu ili kutoa tamko rasmi baada ya kutamkiwa adhabu na CECAFA.

Hilo ni jambo la kusubiri matokeo. Wakati Yanga inalaumiwa kwa yaliyotokea Jumapili, wapo wengine wa kubeba lawama hususan wale wanaoendelea kuamini kwamba bila ya kuzitumia nguvu za wachezaji wa Simba na Yanga, hawawezi kutimiza malengo yao ya kupata utajiri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: