Thubutu! Wabomoe matumaini yetu?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 02 December 2009

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

MWELEKEO wa mabadiliko mema Zanzibar umeshajijenga. Kuufuta ni vigumu. Rais Amani Abeid Karume hawezi. Maalim Seif Shariff Hamad hawezi.

Nataka kuamini hawawezi. Watakuwa wajinga. Tena wapumbavu. Nani aliwasukuma kukutana Ikulu kama siyo wananchi walio nyuma yao?

Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF, alisema mwaka 2001, ni upumbavu kurudia kwenye maovu.

Wazanzibari weshaamua. Wanataka kujenga nchi yao iwe kweli ya maziwa na asali. Lakini wao ni wengi. Haiwezekani watu milioni wakaongoza. Wametoa dhamana.

Upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) yupo Karume, upande wa Chama cha Wananchi (CUF) ni Maalim Seif. Wawakilishi wa Wazanzibari hawa walikutana 5 Novemba 2009 na kukubaliana kubadilika na washirikiane kujenga nchi.

Nani anataka kuturudisha nyuma? Hakuna cha Muhammed Seif Khatib wala Ali Juma Shamhuna. Hakuna hata cha Mama Asha Bakari Makame. Wote ni sehemu ya wananchi wanaoitakia mema Zanzibar, na hatimaye Tanzania.

Siamini kama Khatib, Mbunge wa Uzini, Shamhuna, Mwakilishi wa Donge na Mama Asha, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake CCM, wanataka Zanzibar iwake moto. Siamini.

Iwake ili wakaishi wapi? Sawa wana pesa watasafiri na kukimbilia Dar es Salaam au watakako. Watahama na familia zao. Hawatakuwa Wazanzibari halisa hao. Bado itawaandama tu.

Zanzibar inajulikana ilivyo kipenzi cha wazawa wake. Ni nchi kipenzi kikubwa kwa waijuao. Inapendwa na hata Wamarekani waliopata kuitembelea. Wayuropa na wengineo wanaipenda. Kama si mataifa yao basi kwa mtu mmoja mmoja. Wanaipenda.

Kila wakifikiria fukwe zetu mwanana wanalia. Wakiangalia kima punju wa Jozani, viungo mtawalia vya Kizimbani na Dole, dolfini wa Ghuba ya Menai, wanabaki kuendelea kuapa, “Sitaacha kutenga chochote ili kila mwaka niende Zanzibar.”

Basi hata haya mafiga matatu – Khatib, Shamhuna na Mama Asha – hawawezi kuikosa Zanzibar. Kama wanafanya mzaha, wawaulize Wazanzibari kwa mamia walioko ughaibuni; wengine wameondoka Zanzibar tangu waliponyanyasika na kushikwa na woga baada ya maafa yaliyofuatia mapinduzi ya 12 Januari 1964.

Ah, wacha bwana, Zanzibar ni nzuri. Waliosema ni njema atakaye aje, kama walikuwa wakiamini hivyo ndani ya nyoyo zao, hawakukosea. Siyo nchi ya kujaribia uhuni na ushenzi. Utakwama tu. Usipojisuta, utasutwa.

Ninaamini mafiga haya wanacheza tu makida. Si vibaya kucheza ngoma. Lakini ngoma wanayoicheza wanaijua. Sina wasiwasi wanajua pia vya kuicheza.

Ukitazama walichokisema, unabaini wanasumbuliwa na woga. Ni wa bure lakini. Ni jitihada za kupaisha majina. Wajulikane wapo. Watu wengine ni muhimu wawepo. Inasaidia. Si kila msemaji anakosea njia. Wengine wanatuzindua.

Nani asiyewafahamu hawa? Wanajulikana na tunawajua. Wana matatizo. Wanajaribu kuyasahau wanashindwa. Si rahisi mtu kusahau utamu. Wamekuwa nao, wanataka zaidi. Nani hataki utamu? Sote tunautaka. Tatizo ni kwa kiasi gani mtu anadhani wengine hawautaki.

Si hivyo tu. Kama ni utamu basi kila Mzanzibari ana haki ya kuufaidi. Mafiga haya wamekuwa na vyeo vikubwa na wanasahau hivyo dhamana tu. Mamlaka ya nchi, ya wananchi wenyewe. Ndivyo Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 isemavyo.

Wananchi ndio wenye nguvu ya kuridhia na kukataa chochote. Ninaamini wanachohitaji mafiga matatu ni kusaidiwa kidogo tu mawazo ili watulie kiakili. Hili linahitaji muda.

Ukiyachambua maelezo yao utakuta yana uzito fulani. Wa ubaya na uzuri. Khatib na Shamhuna wanasema CCM haihitaji kushirikiana na CUF kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Ni kweli.

Upo umuhimu mkubwa Zanzibar kuwapo upinzani kisiasa. Baada ya chama kinachoshinda uchaguzi, kihalali, kupewa nafasi ya haki na kuunda serikali, lazima kile kilichoshindwa, kibaki chama cha upinzani. Huu ndio mfumo wa demokrasia ya kwelikweli.

Mahitaji ya Zanzibar siyo serikali ya umoja wa kitaifa kwa muda mrefu. Hapana. Natofauti sana na wengine. Hiyo ni njia tu ya kufikia demokrasia; ile ya chama kinachoshindwa katika uchaguzi ulio huru, wa haki na uwazi, kikwelikweli, kukubali matokeo na mgombea wake kukiri na kumpongeza aliyeshinda.

Muhimu hapa ni serikali inayoundwa kuwajibika ipasavyo kwa umma, kutambua na kuheshimu utawala bora: vigezo ni kujali watu; kuheshimu utawala wa sheria; kutumia vema raslimali za nchi na mali ya umma; kusikiliza wakosoaji wake; kuheshimu upinzani ikiwemo kutambua mchango wake ndani na nje ya Baraza la Wawakilishi.

Baraza iwe ndio mahali pa kupitishia maamuzi makubwa yanayohusu maslahi ya Wazanzibari. Kila kinachofikiriwa na serikali ili kuimarisha uchumi, huduma za jamii na kujenga mlahaka mzuri wa nchi mbele ya macho ya ulimwengu, kiamuliwe hapo.

Umuhimu wa kutumia chombo hiki kwa kila maamuzi, ndio hoja ya Mama Asha. Anaposema serikali ya mseto au ya umoja wa kitaifa haiwezi kuundwa Zanzibar kwa maneno maana Katiba hairuhusu – ingawa pia haijapinga – anahimiza kutumika Baraza la Wawakilishi.

Anaposema kutekelezwa kwa jambo hilo kutafanyika tu yakiwepo mabadiliko makubwa ya katiba hajakosea. Huo ndio utawala bora. Marekebisho au mabadiliko yoyote ya katiba lazima yawasilishwe, yajadiliwe na kupitishwa barazani.

Jambo hili si la kuamuliwa na Baraza la Mapinduzi au Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM; hapana. Huko ni kudharau wananchi; wale wenye mamlaka ya kuongoza nchi.

Tuelewane vizuri. Mtu anaposema, “suala hili lazima lipelekwe kwa wananchi,” maana yake si lazima iwe kutumia kura ya maoni. Hiyo ni njia moja. Zipo nyingine; na hii ya kutumia Baraza la Wawakilishi ndiyo bora zaidi.

Mama Asha amesema, “Hata hivyo hakuna jambo lisilowezekana isipokuwa taratibu na sheria za nchi zizingatiwe hasa kwa vile SMZ inaendeshwa kwa kuzingatia Katiba na Sheria.” Vizuri sana. Wapi amekosea?

Ningeogopa iwapo angerudia kauli aliyoitoa kwenye kikao cha NEC, Butiama mwaka jana na ikavutia wakubwa wakatae muafaka waliofikia na CUF.

Ipo kwenye kumbukumbu kuwa Mama Asha alipata kusema barazani, “Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikupatikana kwa vikaratasi.”

Angerudia haya ningejua anaendelea kudanganyika tu. Mama huyu anayejulikana kuishi kwa kuonewa huruma, opportunist, aliponda muafaka uliopigwa kumbo na CCM. Ni huyu alimtukana Maalim Seif matusi ya nguoni kikaoni Butiama.

Ipo kanda katika mfumo wa hansard inayothibitisha alichokisema pamoja na ma opportunists wenzake kutoka Zanzibar. Wote tunawajua hata wanaojidai wema mitaani.

Watu wa aina hii wanakuwa na nongwa sana wanapobaini mabadiliko yanayokusudiwa kufanywa, yanaweza kupokonya utamu wanaofaidi.

Ni hawa waliobeza makubaliano yaliyofikiwa kwa gharama kubwa ya akili za waliojadiliana, muda waliotumia na fedha za kugharimia vikao; huku Wazanzibari wakisubiri kwa shauku muafaka usainiwe ili wajenge nchi yao.

Kauli za wahafidhina wakiwemo vijana wachanga katika siasa, zilipotisha viongozi wa juu wa CCM na Taifa, zikasababisha kufuta matumaini ya wananchi. Muafaka ukakwama. Tukarudi tulipokuwa.

Yapo maneno mabaya waliyoyatoa Khatib na Shamhuna. Wamezidi kuthibitisha ukorofi wao kisiasa juu ya Wazanzibari. Tutawajadili.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: