Timu ya Rais ya EPA: Kuna kitu au porojo tupu?


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version

TIMU ya Rais ya kuchunguza ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imemaliza kazi yake.

Utata uliojikita ndani ya EPA, ndiyo unaowafanya wananchi kuwa na hamu ya kutaka kujua kilichogunduliwa na kupendekezwa na Timu ya Rais Jakaya Kikwete.

Wananchi wanataka kujua kama Timu ya Rais, imefanya kazi iliyotumwa, au imeendeleza tabia ya kulindana ambayo imezoeleka kwa miaka nenda rudi.

Je, Timu imeweza kufichua yale ambayo serikali ilitaka kuficha wakati ule? Wamepata wapi ubavu huo leo? Jibu hilo nalo linasubiriwa na wengi.

Je, timu ya Kikwete inakuja na majina kamili ya wahusika wa EPA? Hayo hasa ndiyo wananchi wanataka kujua na ni jukumu la rais kuyataja majina hayo hadharani.

Timu inatakiwa kusema bila kujitafuna, ni wapi ambako wahusika wa EPA wamejichimbia – ndani na nje ya nchi.

Je, waliwezaje kufanikisha mipango yao wakati baadhi ya wanaotajwa ni watu wa kawaida kabisa? Waligawana vipi nyara zao na wale waliowatuma? Nani wengine walishiriki katika ukwapuaji huu?

Je, wakwapuaji wana hadhi gani katika jamii? Wanashika nyadhifa zipi? Je, hawana uhusiano wa moja kwa moja au hata wa mbali na serikali au chama tawala? Kama wanao, ni kwa kiasi gani? Ushawishi wao ukoje?

Je, waliotumika kuotesha makampuni kama uyoga na hatimaye kufanikisha ukwapuaji, wamezifanyia nini fedha walizokwapua?

Kama kuna fedha zilizorejeshwa ni sehemu gani ya zilizochukuliwa; na zilizobaki zitakusanywa kwa mtindo gani?

Wenye makampuni halisi ni akina nani na wako wapi? Wanamiliki vitega uchumi gani na wapi? Je, mpaka sasa wanapowasilisha ripoti yao, serikali imekamata vitegauchumi vingapi na vya thamani gani?

Kama matarajio yote haya ya wananchi hayamo katika taarifa au yamo kwa kiasi kidogo tu, kwa nini rais akubali kupokea porojo badala ya ripoti halisi inayokidhi matarajio ya wananchi?

Bila shaka Rais Kikwete anajua kuwa wananchi wanataka kuona fedha za umma zinarudishwa na wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria bila kujali uwezo wao kifedha au mamlaka waliyonayo.

Je, fedha nyingine zilizokwapuliwa zimekwenda wapi? Waliolipwa wako tayari kwenda mbele ya vyombo vya sheria na kutaja kila kilichofanyika? Kama ndiyo, kwa kiwango gani serikali imewahakikishia usalama wao?

Tayari imefahamika kuwa makampuni yaliyotajwa kuwakilishwa na wadai waliokwapua mabilioni ya shilingi, yalikuwa makampuni hewa; hivyo baadhi ya fedha zilizokwapuliwa zilibaki katika mikono ya BoT.

Jopo la uchunguzi lilikuwa chini ya uenyekiti wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.

Wajumbe wengine wawili, ni Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea.

Ukwapuaji ndani ya EPA uligunduliwa baada ya nchi wafadhiri na wananchi kuchagiza serikali kufanya uchunguzi ndani ya BoT.

Hata hivyo, serikali ilikubali kufanyika ukaguzi katika Akaunti ya EPA pekee. Awali kazi ya ukaguzi ilifanywa na kampuni ya maodita ya Deloitte & Touche kutoka Afrika Kusini.

Hata hivyo, kampuni hiyo haikumaliza kazi iliyopewa, baada ya serikali, kwa sababu inazozijua, iliamua kusitisha kazi ya Deloitte & Touche.

Kabla ya kufunga virago, tayari maodita walishagundua kuwapo kwa makampuni hewa. Baadhi ya yaliyodai kuwakilisha makampuni ya nje, yalikuwa ya kubuni tu.

Vilevile baadhi ya makampuni ya ndani hayakuwa makampuni halali. Mengi yaligundulika kuwa yalianzishwa kwa kutumia nyaraka za kugushi.

Kampuni walizozitaja kwamba wanaziwakilisha, nyingi zilikuwa zimekufa kitambo; nyingine hazikuwapo kabisa.

Mfano hai ni kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyokuwa imechotewa dola za Kimarekani 30,732,658.82 (sawa na zaidi shilingi bilioni 40 za Tanzania) wiki tano baada ya kusajiliwa.

Maodita waligundua pia kuwa kampuni kama ya Kagoda haikuwa na anwani kamili; ilionekana kama ilisajiliwa kwa kazi maalum ya kukwapua fedha kutoka BoT.

Hata wakurugenzi wake halisi hawakujulikana wazi. Mahali palipotajwa kuwa makazi yake hapakufahamika kwa watoa leseni na vibali vingine vya biashara.

Lakini katika hali ambayo haijulikani kilichopo nyuma yake, Kagoda ilisajiliwa kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA); Ikapewa leseni na hati ya kufanya biashara na serikali, pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Temeke.

Ni utata huo na mwingine, uliosukuma wakaguzi kuwa na mashaka zaidi na Kagoda. Hilo liliamsha wafadhili na wadau wengine wa maendeleo, kushinikiza kufanyika upya kwa ukaguzi BoT.

Utata mkubwa ulioikumba serikali ni pale waziri wa fedha wakati huo, Zakia Meghji alipodai kuwa fedha walizopewa Kagoda zilikuwa kwa madhumuni ya usalama wa taifa.

Baada ya kubanwa, Menghji alakana kauli ya mwanzo na kudai kuwa alikuwa amedanganywa na aliyekuwa gavana wa BoT, Daudi Ballali.

Jambo moja ambalo wananchi wanasubiri majibu yake ni jinsi gani wizi mkubwa wa kiwango cha kuacha akaunti ya EPA bila fedha, ulifanyika bila vyombo vya ulinzi na usalama wa taifa kujua.

Je, kwa nini viongozi wa vyombo hivyo walishindwa kuwajibika kwa kushindwa kuzuia unyang?au huo wa fedha na rasilimali nyingine za taifa?

Hakuna awezaye kutetea vyombo hivyo au hata kuvisemea lolote pale itakapodaiwa kuwa baadhi ya viongozi wake walishiriki katika ukwapuaji wa fedha na raslimali za umma.

Je, madai kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilihusika katika uchotaji huu? Madai haya yana ukweli kiasi gani? Ni kweli kilichotewa fedha? Nani alikichotea? Wangapi walikataa kupeleka mgao?

Ikiwa timu ya rais itashindwa kuleta majibu ya kutosha, basi tatizo litakuwa limeahirishwa na muda si mrefu litaibuka upya.

Kiashiria cha kushindwa kwa timu ya rais kuleta majibu kinajidhihirisha katika hatua ya Kikwete kuamua kuunda Timu badala ya kutumia taarifa ya maodita wa Ernts & Young waliopewa kazi ya ukaguzi baada ya Deloitte & Touche kuondolewa.

Timu ya rais inatarajiwa pia kutaja kiini cha ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi; msukumo hali wa kuasisi wizi wa aina hii kupitia benki.

Kwa mfano, nani alikuwa anamtuma yupi, kwa nani na kuchukua nini. Wananchi wanataka kuona vitaarifa na maagizo kwenye vikaratasi (memo) kutoka serikalini kwenda Benki au chama cha siasa.

Kuna taarifa zisizothibitishwa kwamba walioasisi mpango huu, kwanza walitaka msaada wa Sh. 25 bilioni kwa 'kazi maalum za kijamii,' lakini walibadilisha mpango huo na kubuni wa ukwapuaji kutoka akaunti ya EPA ambako walidhani mambo hayatafumuka.

Wananchi wanasubiri timu ya rais kuthibitisha taarifa hizo ambazo zimeenea sana nchini na wanaotajwa kuhusika nazo hawajajitokeza kuzikana.

Kama timu ya rais ilifanya kazi yake kwa makini, bila shaka ilipata fursa ya kumhoji Ballali kabla hajaaga dunia.

Je, alihusika? Alihusikaje? Ulikuwa mradi wake au alishinikizwa? Kama alishinikizwa, nani aliyefanya kazi ya kumshinikiza?

Ni majibu kwa maswali hayo ambayo yanaweza kusaidia wananchi kujua kwa nini gavana ambaye amefanya kazi hadi mashirika ya fedha ya kimataifa, ateremke hadi kuwa 'gavana wa SAKOSI?'

Aidha, wananchi watataka kujua tume imepata nini juu ya watu muhimu wanaodaiwa kurahisisha ukwapuaji.

Wale ambao wametajwa kuwa karibu na maamuzi yaliyosaidia uchotaji wa fedha ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Andrew Chenge, aliyekuwa waziri wa fedha, Basil Mramba na Katibu Mkuu Hazina, Gray Mgonja.

Jambo kubwa ambalo wananchi wanataka kuona ni hatua ya serikali dhidi ya wahusika; wawe ndani ya serikali au nje katika biashara zao.

Wananchi wanatarajia pia kuona CCM ikionyesha kwa vitendo kwamba haikuwa nyuma ya mpango huu wa ukwapuaji.

CCM inatarajiwa kueleza hatua itakazochukua kwa wanachama na viongozi wake waliobainika kushiriki katika ukwapuaji huo.

Kufanya hivyo kutasaidia kurudisha hadhi na heshima ya chama hiki, ambacho katika siku za hivi karibuni hadhi yake imeanza kutokomea.

Kile kilichoitwa na wanachama na viongozi wake kuwa 'miiko ya uongozi,' ambayo ni msingi mkuu wa kuwa na viongozi waadilifu na waaminifu, tayari iligeuzwa kuwa kiini macho.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: