TINDO MHANDO: Aliowatetea ndiyo ‘waliomchinja’


Issac Kimweri's picture

Na Issac Kimweri - Imechapwa 22 December 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi imebobea katika kufanya maamuzi tata. Miongoni mwake ni hulka ya kutenda kinyume cha yale isemayo.

Ukisikia ikihimiza uwajibikaji, uchapakazi kwa bidii unaweza kuingia kwenye kosa la kiufundi kuamini kwamba ndivyo inavyotaka kuendesha mambo yake.

Kwa muda mrefu maamuzi mengi ya serikali hii ya Awamu ya Nne ambayo CCM hupenda kutamba kwamba ni serikali yake, yamejikita katika kitu kimoja, ghilba.

Kila anayeonekana kuchapa kazi sawa sawa ndani ya serikali hutazamwa kwa jicho la husda, aghalabu ataundiwa mkakati wa kumwangamiza.

Ngoja nieleze kidogo. Hakuna ubishi kwamba yaliyomkuta aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta hadi kutoswa kwenye kinyang’anyiro cha uspika kwa kisingizio cha kutaka spika  mwanamke, ni kielelezo cha aina ya mfumo huo wa kusema, “Tunataka uwajibikaji,” kumbe ukweli si hivyo.

Sitta aliadhibiwa kwa sababu alionekana kulijenga Bunge lenye nguvu, lililokuwa linaiwajibisha serikali, lililokuwa linaifanya serikali ikose usingizi.

Alijenga Bunge lililojaa wawakilishi wa wananchi na ambalo liliifanya serikali ikose usingizi kwa kusimamia uwajibikaji wa serikali kwa vitendo.

Kwa kuwa CCM na serikali yake hawataki kuwajibika au tuseme kuwajibishwa, ilipotokea nafasi ya kujivua wajibu huo, kukimbia “kisago” kama cha Richmond, Shirika la Reli la Taifa (TRL), ufisadi katika mkataba wa TICTS, ilikuwa ni sherehe ya mwaka kufanikisha kulirejesha Bunge katika zile zama za kuvunja kila nguvu iliyokuwa ikidai uwajibikaji kutoka serikalini

Hili ndilo lililomponza Sitta. Hakujuwa kwamba alichokuwa akikihubiri na kukisimamia, hakikuwa miyoni mwa baadhi ya viongozi wake.

Hata hivyo, jambo kubwa ambalo Sitta anajivunia, ni kuondoka katika nafasi hiyo akiwa na heshima yake; bado anayo fursa nyingine ya kujiandikia historiaa mpya.

Lakini pia hata utendaji wa waziri kama John Magufuli, ambaye katika utawala wa rais Benjamin Mkapa, akiwa naibu waziri wa ujenzi na hatimaye waziri kamili, kwa aina ya utendaji wake, ilikuwa ni kupoteza muda na rasilimali kuthubutu kumuondoa.

Akiwa katika nafasi hiyo, Magufuli amejitofautisha kabisa na wote walioweka kuongoza wizara ya ujenzi kuanzia Basil Mramba; Andrew Chenge na baadaye Shukuru Kawambwa.

Kwa ujumla wote hao hawana lolote la maana walilofikia katika kipindi chote ndani ya wizara hiyo.

Ingekuwa si ghilba za CCM kwa kuamua kupoteza muda wa mchapakazi kama Magufuli kwa miaka mitano, hakika leo tusengekuwa tunazungumza aina ya masongamano wa magari tutaoona katika jiji la Dar es Salaam.

Hili ni balaa mbalo kwa mtu kama Magufuli angekuwa ameipunguza kwa asilimia 60 sasa, lakini ghilba ziwaache wapi waliozoea kupigiwa makofi bila kuwajibika?

Ni kweli sasa Magufuli amerejeshwa ujenzi lakini gharama ya kumtupa huko na huko ilikuwa ni kubwa sana katika sekta ya barabara.

Kipindi cha miaka mitano ya kufanya majaribio ya mawaziri katika wizara hiyo, hakika kitakuwa kimeigharimu mno serikali na taifa kwa ujumla.

Wakati tukiwatazama Sitta na Magufuli katika sura ya kuwindana na kukataa uwajibikaji ndani ya serikali ya CCM, wiki iliyopita hulka ile ile ikamwangamiza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), Tido Mhando.

Baadhi yetu bado tunakumbuka jinsi Tido alivyobeba kundi la mtandao lililomuingiza rais Kikwete madarakani. Akiwa mkuu idara ya Kiswahili, Tido ndiye aliyeendesha kile kilichoitwa, “Kura za maoni,” ambazo zilikuwa maalum kwa ajili ya kumbeba Kikwete wakati wa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama mwaka 2005.

Hakuna mwananchi yeyote mwenye akili timamu anayeweza kuhoji weledi, uadilifu na uchapakazi wa Tido.

Huyu ni Mtanzania ambaye si tu aling’aa katika fani ya habari nchini, bali duniani kote.

Akiwa ametumika Redio Tanzania (RTD) kabla ya kujiunga na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) idhaa ya Kiswahili, ambako alipanda hadi kuwa mkuu wa idhaa hiyo.

Binafsi ninaamini ni weledi wake na uthubutu wake kulikochochea watawala ambao hawaishi kubadili maamuzi kila uchao, kufunga safari na kumleta Tido nchini kuikoa TBC ambayo ilikuwa ni “marehemu.” 

Leo hii, unapofananisha shirika hili lilipofikia hasa baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Tido kwa takribani miaka mitano, haraka utabaini kuwa ndani ya serikali kuna watu wanaopenda taifa hili kusimama hapa lilipo kila mwaka.

Alikuwa ni Tido aliyeiokoa TBC kutoka sura ya kituo cha tv kinachofanana na kituo cha shule kwa wanafunzi kujifunzia kushika kipaza sauti, hadi kituo kinachoheshimika na kilichosambaa kila kona ya nchi.

Lakini cha muhimu zaidi, TBC chini ya Tido iliweza kujiendesha kama kitu kilichojaa watu weledi katika fani ya habari.

Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita wengi walishuhudia jinsi TBC ilivyojipanga kila kona ya nchi ikijitahidi kuwataarifu wananchi matukio mbalimbali ya uchaguzi.

Kwa kiwango cha juu kabisa shirika hili la umma lilifanya kitu cha maana ambacho kwa miaka mingi hakijawahi kufanywa na chombo kinachofanana nacho kwa maana ya hadhi yake kama kituo ambacho serikali ina mikono yake ndani yake.

Pamoja na ukweli kwamba TBC ilibeba kwa kiwango kikubwa chama kilichopo ikulu – Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini hata kile kidogo ambacho wapinzani walipata, kilitokana na juhudi zake binafsi.

Taifa hili limeshuhudia vituo kadhaa vya televesheni hasa vile vya binafsi vikijikomba kwa watawala.

Hapana ubishi kwamba Tido alirejeshwa nchini katika ule wimbo wa watawala wetu wa kutaka wataalam wa Kitanzania ambao wamekimbilia nje,  waje kushiriki katika ujenzi wa taifa lao.

Aliitikia wito huo. Akaifanya kazi kwa bidii akiamini kuwa watawala nao wanaamini katika hicho wanachohubiri. Wapi!

Hakuna kinachoitwa kuwajibika kwa bidii, wala hicho kinachoitwa, “ujenzi wa taifa.”

Matokeo yake kwa aina ile ile ya kutaka kila kitu kiwe vile vile jana na leo, mwaka jana  na leo, kwa mazoea yale yale, Tido amerushiwa virago na serikali katika aina ya kumdhalilisha sana.

Amedhalilishwa kama mtu aliyeshindwa kutimiza wajibu, amefanywa kama si wale wale waliomuomba arejee nchini kujenga tv ya taifa! Ni kwa sababu, alijitahidi kuwa binadamu huru; anayefikiri kwa mawazo yake; na asiyesumbuliwa na chochote, isipokuwa weledi.

Ndiyo msingi wa serikali kumuona tishio. Haikumueleza azima ya serikali ya kutosaini mkataba mpya. Kuna taarifa hata baadhi ya stahiki zake ikiwamo mishahara, serikali haijaweza kumlipa.

Jambia lile lile linalokata shingo za wawajibikaji limeanguka Tido.

Udhalilishaji aliofanyiwa Tido unafanana na mwingine mwingi ambao CCM  wamekuwa wakifanyiana wenyewe kwa wenyewe ndani ya chama.

Ni mwendelezo wa kuchinjana – mchakato wa kura za maoni umethibitisha jinsi jambia la kukata shingo lilivyofanya kazi -  watu wasiotakiwa ama sura zao, ama harufu zao, ama ngozi zao, au asili zao.

Wengi wao walichinjwa; bado jambia lile  lingali mikononi mwa “wachinjaji” wanawinda mmoja baada ya mwingine.

Tido alisema alishitushwa kwa kukatizwa kwa mkataba wake, kwani walau alikuwa na miezi mingine sita kabla ya kuachia kibarua TBC, lakini kwa kuwa wenye jambia wana hasira ya kupungua kwa kura, wanasaka mchawi.

Wanaamini kuwa TBC haikuwabeba vya kutosha; wanaona kuwa Tido alichangia katika upunguaji wa kura hizo.

Kwa mwendo huu ni vigumu kujenga uwajibikaji wa kweli ndani ya serikali, na matokeo yake ni kujiimarisha katika unafiki ambao kamwe hautatujenga kama taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: