TLS, Wabunge mfukoni mwa Barrick


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 24 August 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

HABARI zilizoandikwa sana wiki mbili zilizopita zilihusu matukio mawili. Kwanza ni Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira chini ya Mwenyekiti wake, James Lembeli, Mbunge wa Kahama (CCM),  kufanya ziara katika mgodi wa dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo, Tarime.

Pili ni tukio la mkutano wa chama cha wanasheria wa Tanganyika (Tanganyika Law Society - TLS) uliofanyika mjini Dodoma na kufunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mtanzania Asha-Rose Migiro.

Matukio haya mawili yalifanana kwa sababu moja kuu; yote yalifadhiliwa na kampuni ambayo inalalamikiwa kwa kudhulumu na kunyanyasa wananchi popote pale inapofanya shughuli zake.

Kampuni hiyo iliyofadhili ziara ya wabunge na mkutano wa wanasheria ni African Barrick Gold (ABG) yenye makao makuu yake Toronto, Canada.

Katika tukio la kwanza wabunge walitembelea mgodi wa North Mara uliopo takriban kilometa 30 kutoka mjini Tarime ambao unamilikiwa na kuendeshwa na Barrick.

Na katika tuko la pili wanasheria wanachama wa TLS walifanya mkutano wao mkuu pale Chuo Kikuu cha Dodoma kwenye ukumbi wa Shule ya Sayansi Jamii ambao ulipambwa na mabango ya Barrick kila upande kama miongoni mwa wafadhili wake.

Matukio haya mawili yanakera kwa namna tofauti. Kwanza tukio la wabunge lilikera na kuudhi wananchi kwa vile lilionyesha dhahiri shahiri kuwa wabunge wale walijua kuwa wanakosea lakini wakaona bora kukosea kuliko kukosa posho na mapochopocho ya Barrick.

Ndege zenye Na 5H-KKC, 5H-TMC na 5H-NCS zilizoonekana zimeegeshwa uwanja wa ndege wa Dodoma majira ya saa 3.00 asubuhi huku maofisa wa Barrick, akiwamo mtendaji mkuu Deo Mwanyika wakirandaranda, saa mbili baadaye zilitua uwanja wa ndege binafsi wa Barrick, Nyamongo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, ambaye yupo mstari wa mbele kupinga vitendo vya Barrick jimboni kwake alipohojiwa juu ya ufadhili huo alijibu, “Mbona tumefuatana na wabunge wa CHADEMA?”
Ina maana sasa wabunge wa CCM hawajiamini kabisa na kipimo chao kwa jambo lolote ni ushiriki wa wabunge wa CHADEMA?

Je, kushiriki kwa Esther Matiko, Suzy Lymo na Mchungaji Peter Msigwa wa CHADEMA kunafanya jambo baya kuwa zuri? Ina maana siku hizi wabunge wa upinzani hutumika kuhalalisha rushwa za safari, mapochopocho na posho kutoka makampuni yanayolalamikiwa?

Kama kweli wabunge wetu walikuwa na nia njema kwa nini hawakuandamana na waandishi wa habari kutoka vyombo huru kama Mwananchi, Tanzania Daima, Mtanzania, Nipashe, MwanaHALISI au angalau hata HabariLeo?

Kitaaluma Lembeli ni mwandishi wa habari, hivyo si mgeni na mambo ya habari. Atawachukuaje wanahabari wa MAELEZO wasiokuwa na gazeti, TV wala redio bali husubiri fadhila za wenye vyombo hivyo?

Mwaka 2009 Barrick walilalamikiwa kuchafua maji ya Mto Tigithe na kusababisha madhara kwa binadamu na mifugo. Kamati ya Bunge chini ya Job Ndugai iliwapa miezi mitano kurekebisha.

Baada ya miaka miwili wamerekebisha uchafuzi huo kadiri walivyoona inafaa, halafu inadaiwa wakaandika ripoti ya namna walivyofanya “kazi nzuri” ya kurekebisha uchafuzi wao.

Halafu watuhumiwa Barrick wakakodi ndege kwa ajili ya wabunge wenye uchu wa safari za ndege, wakawalipa posho na kuwakabidhi ripoti iliyoandikwa kitaalamu na Barrick ili wailete Dar es Salaam kuwa ndiyo ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na mazingira. Aibu iliyoje hii!

Kama kweli wameandikiwa ripoti, hakuna mtu mwenye akili timamu atakayeamini ripoti yoyote itakayotolewa na kamati ya Lembeli. Hakuna mtu atakayeamini kuwa ripoti itakayotolewa na kamati ya Lembeli imeandikwa na kamati hiyo.

Hiyo itabaki kuwa ripoti ya Barrick. Haifai hata kidogo. Mto Tigithe ni mchafu, walioathirika kwa sumu ya cyanide na paf ya Barrick bado wanaumwa. Ripoti hiyo inasaidiaje kutibu waathirika wale? Mchezo gani kamati ya Lembeli imefanya?

Ieleweke, mpaka sasa si Barrick wala serikali ambayo imechimba kisima hata kimoja!

Pili ni kuhusu ama uongozi wa TLS kuwafuata Barrick na kuomba ufadhili wa shilingi milioni nne za kugharimia mkutano wa nusu mwaka au Barrick kuwafuata TLS na kuomba wafadhili mkutano huo kwa shilingi milioni nne.

Sielewi ni nani kati ya TLS na Barrick aliyemfuata mwenzake kuomba ufadhili. Lakini jambo moja ni wazi kabisa kuwa TLS haikupaswa kuomba ufadhili kwa Barrick.

Sababu ni wazi kabisa. Utakubalije kushirikiana na mtu anayelalamikiwa kwa uzinzi kama wewe si mzinzi? Utatofautianaje na mlevi kama wewe huonji chibuku, gongo au ulanzi? Haiwezekani upendelee vikao vya wanga kama wewe si mwanga! Wahenga walisema ukitembea na mwizi nawe utaiba!

Kwa wale waliosoma enzi zile za zamani nilizosoma mimi, watakumbuka kitabu cha ‘Someni Kwa Furaha’ kilichokuwa na wimbo usemao:

Paulo usije kucheza na sisi una mikono michafu, Paulo usije kucheza na sisi una vidole vichafu, makucha machafu, miguu michafu, meno machafu, mdomo mchafu.

Paulo mchafu kwa wakazi wa Nyamongo ni Barrick. TLS na kamati ya Bunge watakubalije kujumuika na Barrick mbele ya macho ya wananchi wenye malalamiko lukuki wakihitaji msaada wa kisheria wa TLS?

TLS inayopaswa kutetea haki nchini imekosea kuomba ufadhili kutoka kampuni inayolalamikiwa na wananchi kwa kunyang’anya ardhi Nyamongo bila malipo au kwa malipo kiduchu. Kwa TLS huu ni usaliti.

Nasema haya kwa sababu TLS si chama maskini. TLS wana uwezo wa kupata fedha hizo walizofadhiliwa na Barrick kwa michango yao au kwa kufadhiliwa na makampuni mengine yenye heshima mbele ya macho ya jamii.

Barrick wana kesi ngapi dhidi ya wananchi Mahakama Kuu Mwanza, mahakama ya wilaya ya Tarime au hata Mahakama Kuu Dar es Salaam?

Iweje leo ifadhili mkutano wa TLS? Je, wananchi watakuwa na imani na wanasheria wanachama wa TLS kwenye kesi dhidi ya Barrick? Ninachosema ni kwamba Barrick inalalamikiwa kudhulumu na kunyanyasa wananchi Nyamongo, Buzwagi, Kahama, Tulawaka na kwingineko, haikupaswa kufadhili wanasheria.

Nasema tena kuwa Barrick inatuhumiwa kusababisha mauaji ya wananchi ikitumia polisi na leo hii  imefadhili wabunge kwa safari, mapochopocho na posho za kujikimu.

Kwa kifupi heshima ya TLS na Bunge imeshuka na vyombo hivi vya kutetea haki vinaonekana viko mfukoni mwa Barrick na sasa vyombo hivi vitakuwa vikitoa ripoti ya kuisafisha Barrick kwa tuhuma yoyote na shutuma yoyote itakayoikabili. Bunge na TLS hawatahesabika kama watu huru kwa shauri lolote la Barrick.

0
No votes yet