Trafiki Kombe, tunataka vitendo


Yusuph Katimba's picture

Na Yusuph Katimba - Imechapwa 11 March 2009

Printer-friendly version

SERIKALI imetoa miezi sita kwa wamiliki wa mabasi ya abiria kuhakikisha wanafunga vidhibiti mwendo aina ya "Tachograph" pamoja na mikanda katika viti vyote.

Mbali na hilo, serikali imeagiza kuwa ndani ya miezi mitatu wamiliki wa mabasi wawe tayari wameajiri madereva wenye elimu na ujuzi wa kutosha.

Maagizo hayo yalitolewa wiki mbili zilizopita mjini Dar es Salaam na Mkuu wa Kikosi cha Polisi wa Usalama Barabarani nchini, James Kombe.

Hizi zote zinaonekana kuwa hatua nzuri. Lakini kauli kama hizi ziliishawahi kutolewa na watawala na kuishia midomoni mwao, kwani zimepuuzwa; na viongozi wamekuwa wepesi wa kuagiza pasipo ufuatiliaji wowote.

Mfano mzuri ni huohuo wa vidhibiti mwendo. Katika miaka ya nyumba vyombo vya usafiri wa umma, hasa kwa mabasi yaendayo mikoani. Wamiliki walilazimishwa kufunga vidhibiti baada ya ajali kukithiri.

Mwendo mkali na uzembe wa madereva vilichukuliwa kuwa chanzo kikuu cha ajali; lakini ghafla, utaratibu huo ulitoweka kana kwamba haukuwa amri au uamuzi wa serikali.

Hali hii iliibua maswali mengi hadi baadhi ya wananchi wakadai kuwa huo ulikuwa mradi wa mkubwa mmoja serikalini. Usimamizi wa vidhibiti mwendo uliisha pale ununuzi wa vidhibiti ulipokamilika!

Kwa hiyo Kombe si wa kwanza kutoa kauli kama nzuri zinazoonekana kulinda usalama wa barabara, magari na binadamu.

Mara hii serikali inataka pia kila dereva anayeendesha gari la abiria asiwe chini ya umri wa miaka 30 na asizidi miaka 60. Kombe anasema hatua hizo zitasaidia kupunguza na kuepesha ajali barabarani.

Takwimu zinaonyesha kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikiongezeka; vivyo hivyo vifu kutokana na ajali hizo. Kwa mfano, mwaka 2007 kulikuwa na ajali 17,753 zilizoua watu 2,594.

Mwaka 2008 kulikuwa na ajali 20,615 zilizopoteza maisha ya watu 2,905. Hii ina maana kuwa katika miaka miwili iliyopita watu 5,499 wamepoteza maisha barabarani.

Vifo hivi ni mzigo kwa taifa ambalo linapoteza wanafunzi ambao wangekuwa wataalam; vinaua wataalam na kuacha taifa masikini; vinafanya wengi wawe tegemezi, hasa wale walioachwa yatima na wajane; vinagharimu taifa kwa njia ya tiba kwa waliosalia.

Pamoja na yote hayo – kauli za viongozi, ajali na vifo – bado kuna ulegevu katika udhibiti wa ajali. Kuna mfano wa dereva anayeendesha gari huku akiongea na simu. Ilitangazwa kuwa mtu kama huyo angefikishwa mahakamani. Bado hilo halijatokea.

Madereva bado wanaendelea kuongea na simu wakati wakiendesha; na mara nyingi wakiwa wanapita mbele ya askari wa trafiki.

Kuna mabasi yaendayo mikoani ambayo hayana milango ya dharura (Emergence Doors) inayotakiwa kuwa nyuma ya mabasi. Bado hatua hazijachukuliwa wasiotii amri hiyo.

Nani ambaye hakusikia amri kuwa mabasi yaliyo na injini za malori hayataruhusiwa kuendelea kufanya kazi? Uko wapi utekelezaji. Mabasi ya aina hiyo bado yako barabarani.

Kauli ya Kombe basi isiwe ni mradi tu uliobuniwa kwa kuwanufaisha watu wachache kupitia tatizo sugu. Serikali inapaswa kuchunguza na kufuatilia katika maagizo yake hasa yale yanayolenga maisha ya Mtanzania moja kwa moja.

Kombe bado ana kibarua kigumu. Vidhibiti hivi vinatoka wapi? Ni kule vilipotoka vile ambavyo vilishindikana kufuatilia? Kitu gani hasa kilisababisha udhibiti ushindikane? Nani hasa walisaidia kufanya mradi wa awali ushindwe na polisi wamejifunza nini?

Tusubiri na tuone.

0
No votes yet