TTCL irudishwe kwa wenyewe


editor's picture

Na editor - Imechapwa 05 August 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TUMEKUWA tukichapisha taarifa nzito kuhusu hali ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa muda sasa. TTCL ni kampuni iliyoingizwa kwenye mkenge na serikali kwa kuwakabidi wageni kuiendesha tokea mwaka 2001.

Taarifa hizo zinazotokana na vyanzo vya uhakika na vielelezo visivyo shaka. Zinatokana na kutambua fika wajibu wetu kama Watanzania kusimamia jukumu la ulinzi wa raslimali za umma.

Katika kufanya hivyo, hatujakusudia kwa namna yoyote ile kushusha hadhi ya kampuni au wawekezaji, kama kweli hadhi hiyo ipo.

Tunachokifanya na tutachoendelea kukifanya ni kufichua yale tunayoamini kwamba mambo muhimu yanayopaswa kurekebishwa kwa nia ya kujenga taifa endelevu kwa kutumia raslimali zake.

Kwa upande mwingine, tunajua kwamba wapo wanaoguswa na ufichuaji wetu huo, na kwamba wanaumia maana ni binadamu wenye nyongo.

Lakini hilo halitufikishi katika kuona huruma kwa sababu tunao wajibu wa kutoa mchango wetu ya kuhakikisha raslimali za umma hazichezewi.

Kampuni ya TTCL ni kampuni ya Watanzania inayopaswa kunufaisha Watanzania. Kamwe si kampuni iliyokusudiwa kunenepesha wageni au wajanja wachache. Ni kampuni iliyoundwa na kujengwa kwa kodi zetu.

Kwa sababu hiyo basi, tunadhani serikali ina wajibu wa kueleza ukweli sasa na kuchukua hatua madhubuti za kuirudisha TTCL kwenye utendaji wa wazalendo ambao wamethibitisha mara kadhaa kuwa wanaweza kuiendesha kwa ufanisi.

Baada ya kuuzwa kwa hisa 35 za serikali kwa wawekezaji MSI/Detecon ilitumainiwa kuwa ingefanya vizuri kwa kuipanua mtandao wake wa mawasiliano.

Yaliyotokea kila mmoja anajua. Wawekezaji wameshindwa kulipa hata kiwango cha ununuaji wa hisa hizo ambacho kilikuwa dola 120 milioni.

Hadi sasa wakati inaelezwa kuwa hisa 35 ziliuzwa, ukweli ni kwamba zilizouzwa ni hisa 17.5 kwa dola 64 milioni.

Ndio kusema kwamba kuondoka kwa MSI/Detecon na kuingia kwa Saskatel mwaka 2007 ilikuwa ni utekelezaji wa malengo yaliyoandaliwa kwa ustadi mkubwa na mawakala wa wawekezaji kwa kushirikiana na baadhi ya watawala ili kuimaliza TTCL.

Tunaamini Watanzania waliowengi hawakubali uangamizaji huu wa TTCL. Kama kampuni yao imewekwa katika mahali inachungulia kaburi, wanapambana kuiona inakuja juu maana wanajua umuhimu wake.

Tunahimiza serikali isimamishe mara moja mkataba wa Saskatel kwa vile hauna maslahi yoyote kwa taifa, isipokuwa tu kunenepesha wageni na wale waliowasaidia kupewa mkataba mwaka 2007.

0
No votes yet