Tuache maneno, tuchape kazi - Chami


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 22 February 2012

Printer-friendly version

KILIO cha Watanzania kuhusu kupanda kwa gharama za maisha, mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani, kimepata mbembelezaji.

Mbembelezaji mwenyewe si mwingine ila ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami. Anasema hakuna sababu ya kulia sana. Sababu ya kusema hivyo ni kwamba juhudi za wizara yake na serikali kwa ujumla zinaonyesha mwanga wa mafanikio, japokuwa bado ni kwa mbali.

Katika mahojiano maalumu na MwanaHALISI wiki iliyopita, Waziri Chami anasema serikali imefanya “mambo makubwa” na bado inaendelea kuongeza juhudi katika uwekezaji, uzalishaji mashambani na viwandani na kuongeza mauzo ya nje.

Mathalan, anasema tangu Rais Jakaya Kikwete aingie madarakani, mwaka 2005, viwanda 189 vikubwa vimeanza uzalishaji nchini kati ya 522 vilivyopata leseni.

Viwanda vidogo vinavyozalisha nchini na kutambuliwa ni 10,231 na vyote hivyo, anasema vinazalisha bidhaa zinazouzwa ndani na nje ya nchi na kuingiza fedha za kigeni na kuongeza ajira.

Akinukuu ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri Chami anasema kwa mwaka jana, mauzo ya bidhaa nje yalifikia dola 1.8 bilioni (Sh. 2.88 trilioni) ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kila mwaka katika uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Chami, mauzo hayo yanatokana na kuongezeka kwa mauzo ya nje ya bidhaa za viwandani, kukua kwa utalii ‘wenye tija’ (watalii wachache wanaotumia sana) na mauzo ya madini.

Kwa upande wa kilimo, anasema ingawa kuna ongezeko kwenye kahawa, tumbaku na katani, hali haijawa nzuri kama ilivyokuwa zamani, kabla bei ya mazao hayo haijaporomoka katika soko la dunia.

Matumaini ya Chami yapo kwenye zao la tumbaku ambalo anasema soko lake limeongezeka baada ya kiwanda cha sigara cha Dar es Salaam kuongeza uzalishaji mara mbili, huku wakulima wakipewa mikataba maalumu inayowawezesha kunufaika na mazao yao.

“Tumepata soko zuri la tumbaku ya Tanzania kati ya tani 30,000 na 60,000 kwa mwaka baada ya kusaini makubaliano na kampuni moja ya China,” anasema.

Hata hivyo, wakati mauzo hayo yanaongezeka na fedha za kigeni zaidi kuingia nchini, thamani ya shilingi ya Tanzania inazidi kushuka ikilinganishwa na dola, hali ambayo Waziri Chami anasema “tatizo ni soko huria linaloruhusu kununua zaidi nje kuliko tunavyouza”.

“Katika soko huria, hakuna anayempangia mtu anunue nini nje, aache nini. Ukitaka kwenda kununua shati kama hili (alilovaa) nchini Malaysia, unakwenda. Ukitaka kununua gari Japan unakwenda, na huko kote unapeleka fedha nyingi kuliko sisi tunavyonunua kwao,” alieleza.

Alifafanua kuwa kwa sasa Tanzania inauza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni  kwa mwaka lakini inanunua bidhaa za dola 9 bilioni, na hiyo nakisi ndiyo sababu kubwa ya shilingi kuzidi kushuka ukilinganisha na dola.

Waziri Chami ambaye pia alizungumzia afya yake akisema sasa yuko fiti baada ya kutibiwa kwa wiki 10 nchini India, anasema suluhisho la hali mbaya uchumi wa nchi ni kila mtu kuchapa kazi.

Anashauri kupunguza matumizi yasiyo ya lazim, akuwekeza kwenye viwanda na kualika wawekezaji kwa wingi.

“Tuache maneno, tuchape kazi. Unajua brother, Watanzania tunaongea sana. Utasikia mtu amekaa kijiweni anajadili ohoo mawaziri hawafanyi kazi yoyote… ohoo serikali haijafanya lolote…huyu anayesema hayo yeye amefanya nini?” anahoji.

“Mwingine utasikia ameangalia bunge, ohoo mawaziri hawajasema lolote… je, wewe unayetazama tv kwa saa tano kwa siku, umefanya kazi gani? Sisi Watanzania kila mtu anataka kuwa mwelekezaji, hata kama hana ujuzi katika eneo hilo,” anasema.

Kuhusu raia wa China wanaofanya biashara za uchuuzi Kariakoo na maeneo mbalimbali nchini, anasema si rahisi kuwafukuza nchini kama ilivyowahi kudaiwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu.

Anasema hatua hiyo inaweza kusababisha mgogoro wa kidiplomasia, kwani hata nchi yao inaweza kuchukua uamuzi ambao una athari zaidi kwa Watanzania.

“Mfano, China ilichelewesha kutoa visa kwa wiki moja tu, wafanyabiashara wa Tanzania wanaokwenda huko waliandamana wakaja hapa ofisini, hivi hali itakuwaje iwapo itazuia waingie kabisa,” alisema.

Soko la Pamoja

Waziri Chami anasema kabla ya kufungua milango, Kenya ilikuwa inauza bidhaa kwa wingi nchini, kuliko Tanzania ilivyokuwa inafanya kwao, lakini sasa mambo yamebadilika.

Anatoa mfano kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita, Tanzania imeuza bidhaa nyingi Kenya mara mbili (kwa miaka miwili), wakati nchi hiyo imefanya hivyo mara moja tu.

“Haya ni mafanikio makubwa sana, na hapo hatujazungumzia mazao ya kilimo, nadhani unajua kuwa katika eneo hilo, Tanzania ndiyo inauza Kenya kwa miaka yote,” anasema Waziri Chami.

Ukiacha Kenya ambayo Chami anasema ilijiandaa kiviwanda muda mrefu, Tanzania inauza bidhaa katika nchi zilizosalia za Afrika Mashariki za Rwanza, Burundi na Uganda kuliko nchi hizo zinavyofanya hapa nchini.

Wizara inalenga kupanua wigo wa soko la bidhaa za viwandani hadi nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudan Kusini.

“Tunazidi kufanyia kazi vigezo vya ubora wa bidhaa kupitia EPZ (maeneo huru ya biashara) ili kupenya katika masoko ya Ulaya na Marekani kupitia mikataba ya EBA na Agoa.

“Mikataba hii inaturuhusu kuuza kila kitu isipokuwa silaha, lakini bidhaa zetu hazijafikia ubora unaotakiwa,” anasema.

Kuhusu uingizaji wa bidhaa zisizo na ubora kutoka nje, Waziri Chami anasema linachangiwa na mambo mawili:

Mosi, tabia ya Watanzania kutafuta faida kubwa. Wanaingia mikataba na wauzaji wa nje ili watengenezewe bidhaa zisizo na viwango, ambazo huziuza hapa nchini kwa bei sawa na zenye ubora.

Pili, ukubwa na upana wa mipaka ya nchi. Inakuwa si rahisi kwa mamlaka zetu na vyombo vya dola kudhibiti kila eneo.

Hata hivyo, anasema pale wanapofanikiwa kuzikamata,  huharibiwa na wahusika kuchukuliwa hatua. Anasema wameanza kuzungumza na mabalozi wa nchi zinazohusika na bidhaa hizo, ili zisaidie kuwazuia watu wao kuuza bidhaa zisizo na ubora.

“Hili la pili nalo tunaamini linawezekana, maana hawa wanaotuuzia hizi bidhaa hawawezi kuzipeleka Ulaya wala Marekani,” anasema.

Kuhusu mifuko myembamba ya plastiki iliyopigwa marufuku na serikali lakini bado inazalishwa na kusambazwa nchini, alisema sheria iko pale pale, ingawa wajanja wanaweza kujipenyeza, hivyo akasema endapo watapata taarifa za wahusika wataendelea kuchukua hatua.

Mikakati hiyo pia ina vikwanzo,  Chami anasema tatizo kubwa ni ukosefu wa umeme wa uhakika, ambalo linaweza kuwa limeondoka kabisa ifikapo mwaka 2018 kama mikataba iliyopo sasa itakamilika.

Baadhi ya mikataba ya umeme iliyopo ni kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Intra Energy ya Australia katikia kujenga mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka, Ruvuma wenye tani 281 milioni za  makaa ya mawezi. Mgodi huu una uwezo wa kuzalisha megawati 100-150 za umeme, ambao utaunganishwa hadi Makambako, Iringa umbali wa kilometa 100.

Pia mgodi wa Mchuchuma na Liganga unaotarajiwa kuzalisha megawati 600 ambao unakadiriwa kuwa na tani 483 milioni za makaa. Umeme huo utasafirishwa hadi Mufindi, ambako utaunganishwa hadi Singida.

Pia kuna mgodi wa Kiwira ambako serikali inazungumza na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kuzalisha megawati 50 hadi 100.

Matumaini makubwa pia yapo kwenye gesi inayoendelea kugunduliwa kwa wingi, inayotarajiwa kupunguza gharama za umeme kwa kiwango kikubwa, ukilinganisha na ule wa mafuta.

Changamoto nyingine zinazotajwa na Chami kukwamisha “ndege ya serikali kupaa” ni miundombinu isiyoaminika hasa reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege.

0
No votes yet