Tuamini RAI wana ubia na vyombo vya usalama?


Anthony Kayanda's picture

Na Anthony Kayanda - Imechapwa 09 March 2011

Printer-friendly version

KILA nikifikiria kilichosukuma mhariri wa gazeti la Rai kuchapisha habari zinazotoa tuhuma nzito dhidi ya MwanaHALISI, napata shida kuamini kama kulikuwa na busara yoyote katika uamuzi wao.

Katika toleo lake Na. 907 la Februari 10–16 gazeti hilo lilichapisha habari iliyosomeka, “Mkakati mzito wa kuiangusha Serikali ya Kikwete wapangwa.” Chini yake kukawa na vichwa vidogo vya kunogesha kikiwemo kilichosema, “Mfanyabiashara mmoja na baadhi ya vigogo wa CCM wahusika… gazeti la MwanaHALISI latumika.”

Nilitarajia Watanzania wangejulishwa baada ya taarifa hizo kwamba tayari serikali inashikilia watu kadhaa kwa tuhuma za kutaka kuiangusha serikali, na kusababisha matatizo makubwa ya kiusalama. Na serikalini tunayo wizara ya habari chini ya waziri Emmanuel Nchimbi.

Ukimya unaoendelea kutawala katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuhusu tuhuma hizi unaashiria mambo mawili makubwa.

Kwanza wanaweza kuwa wanazifuatilia kimyakimya kuona ukweli wake ili wapate mahali pa kuanzia katika kushughulikia hao vibaraka kwa mujibu wa sheria za nchi, na hatimaye wananchi waendelee kuishi katika utulivu na kudumisha ile dhana kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani.

Lakini hata kama ni kuzifuatilia kwa njia hiyo, iweje basi watuhumiwa wasikamatwe na kuhojiwa kama ilivyowahi kutokea mwanzoni mwa miaka ya themanini wakati kundi la vijana wachache waliokuwa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) walipokula njama za kuiangusha serikali ya awamu ya kwanza?

Inawezekanaje gazeti hili, viongozi wakuu wa CCM na mfanyabiashara mmoja wale njama za kuangusha serikali bila ya kuwa na silaha, lakini bila ya kuungwa mkono na watu wenye utaalamu wa kijeshi? Mapinduzi ya serikali kwa njia haramu si lelemama.

Nashangaa kuona gazeti linatoa habari nzito kama hiyo ikionyesha bayana kuwa rais aliyechaguliwa na wananchi, na serikali yake awindwe na kikundi cha watu ili ang’olewe madarakani na wasimamizi wa gazeti husika wakaendelea na kazi bila kuhojiwa?

Mashaka haya yananishawishika kuamini huenda walitumwa kwa makusudi kupandikiza mbegu mbaya kwa malengo wanayoyajua wasimamizi hao na waliowatuma. Inawezekana  wakubwa zao ni watu wenye nafasi kubwa katika medani ya uongozi wa juu wa nchi ndio maana wanaogopwa kuhojiwa.

Kwanza, ni jambo la hatari na wananchi wataendelea kuvitilia shaka vyombo vya ulinzi na usalama kwa kunyamazia taarifa zinazohusu masuala ya usalama wa taifa lao. Ninaziona dalili za siku moja kuchapishwa taarifa za upotoshaji kama vile ni siku ya wajinga hata kama zitagusa maslahi ya taifa kama hii iliyochapishwa wiki chache zilizopita.

Pili, inawezekana vyombo vya ulinzi na usalama vimepuuza tuhuma hizo za Rai baada ya kubaini ni za uzushi zilizopikwa makusudi kwa ajili ya kuridhisha watu fulani wanaodhani wanaimiliki nchi kama kampuni binafsi na wanaweza kuitafuna watakavyo.

Kama hili la pili lina ukweli, basi tujue wazi kuwa tasnia ya habari imepata pigo kubwa na kunahitajika kazi ya ziada kuiokoa kwa kuwa bado wananchi wengi wana imani nayo kama mhimili muhimu katika jamii kwa sababu ya mchango wake katika kuirekebisha serikali iliyopo madarakani.

Laa, kama vyombo vya ulinzi na usalama vimepuuza tuhuma kwa kuwa ni za upotoshaji, basi ni dhahiri baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari wanatunga mambo kwa maslahi binafsi. Na hii ni hatari kwa ustawi wa vyombo vyenyewe, taaluma ya uandishi wa habari na usalama wa nchi.

Isije ikawa baadhi ya vyombo vinalazimika kupika taarifa nzito wakitumia majina ya vyombo vingine vyenye nguvu ya soko, ili nao wapate biashara. Hiyo yenyewe nayo ni hatari. Lazima chombo kijiuze kwa taarifa za kweli.

Chombo gani kinajipitisha katika ofisi mbalimbali za umma na binafsi kutafuta matangazo ili kiishi, na chombo gani kitajiendesha chenyewe kutokana na kuuza habari zake hata kama hakitapata matangazo ya biashara.

Ifike mahali wale wanaojiita “waandishi waandamizi” wakatambua kauwa Watanzania wameamka na hawakubali tena kudanganywa.

Wasomaji wa zama hizi wanajua ni chombo gani kinatoa taarifa zinazowanufaisha na wakiunge mkono na kipi kinawapigia upatu na kuwanyenyekea mafisadi na mawakala wao serikalini wakisokomeze kwa kupuuza taarifa zake.

Lakini, hebu nielekeze jicho la mwisho kwa kutafakari taarifa zilizochapishwa na Rai hilohilo, zilizosema, “CCM sasa yafika njia panda.” Taarifa hizo zilisema chama hicho kikongwe kimepoteza matumaini kwa vijana wengi.”

Najiuliza maana ya taarifa hizi iwapo zinalenga kuchangamsha vijana waichukie serikali yao?

Wasimamizi wa gazeti hilo wanataka vijana wanaodai wamepoteza matumaini wafanye nini kama siyo kuingia barabarani kama wenzao wa Tunisia na Misri ambako maandamano ya mfululizo yamefanikiwa kuangusha tawala zao, pamoja na Libya ambako Kanali Muamar Gaddafi anapambana kutokomeza vikundi vya waasi kudhibiti utawala wake.

Kumbe hata wale vijana wa CCM waliotoa tamko la kuishinikiza serikali kutoilipa kampuni ya Dowans fidia wanayodai TANESCO kwa mkataba wao kuvunjwa, na kuivunja Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kwa kushindwa kuwajibika, nao ni sehemu ya hao wenye mkakati wa kupindua serikali?

Waandishi wa habari waache mtindo wa kujipendekeza kwa watu fulani ambao wanadhani bila ya kuwatumikia watashindwa kuhudumia familia zao. Taaluma ya habari itakuwa na maana kwa jamii ikiwa inatoa yale yenye maslahi kwa jamii si vinginevyo. 

Anthony Kayanda ni mwandishi wa habari kijana anayeishi mkoani Kigoma ambaye amekuwa msomaji mkubwa wa MwanaHALISI.

Anapatikana kwa imeili: akayanda@yahoo.com
0
No votes yet