Tubadili mfumo; wanaoshindwa washirikishwe, wasikilizwe


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 20 May 2008

Printer-friendly version

KAMA kuna jambo ambalo baadhi ya Watanzania wenzetu hawajafuzu, ni mwenendo wa siasa za ushindani zinazohusisha chama tawala na vyama vya upinzani.

Na kwa kuwa mfumo wetu unaruhusu "mshindi achukue yote," moja kwa moja tumekuwa tunaendekeza siasa za aliyeshindwa kukosa yote.

Maana yake ni kwamba hata pale ambapo mshindi atamzidi mshindani wake kwa kura chache sana; atatangazwa mshindi, na atachukua "kila kitu."

Kwa staili hii, Dk. Salmin Amour alitangazwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar mwaka 1995 dhidi ya mshindani wake Seif Shariff Hamad; huku Dk. Salmin akitamba kwamba hata ushindi wa goli moja ni ushindi kama wa magoli sita!

Wafuasi wake kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliwabeza wafuas wa Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa miaka mitano.

Na Dk. Salmin mwenyewe alimnyanyasa Hamad kisiasa kwa miaka mitano yote, kiasi cha kuzorotesha na hatimaye kuua uhusiano wa kijamii wa watu wa Unguja na Pemba; jambo ambalo lilikuza na kupanua uhasama wa kisiasa uliodumu kisiwani humo hadi leo.

Ubabe na manyanyaso ya CCM dhidi ya CUF ndicho kichocheo cha ugomvi mkubwa kisiasa visiwani humo, ambao Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alitangaza kwamba ulikuwa unamnyima usingizi.

Ugomvi huo ndiyo ambao Rais Jakaya Kikwete aliuita "Mpasuko wa kisiasa Zanzibar" ambao alisema anadhamiria kuukomesha.

Rais yangu ni kwamba mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar hauwezi kukoma kama CCM itaendeleza siasa za kibaguzi, ambazo zinawanyima mashabiki wa CUF fursa ya kushiriki katika siasa za visiwa vyao.

Kwamba tofauti kati ya aliyetangazwa mshindi na aliyetangazwa kushindwa ni asilimia zisizozidi tano (5), ni ishara kwamba wagombea urais wana nguvu sawa kisiasa.

Hii si tofauti ya kumfanya aliyeshinda achukue yote, atambe, abeze na kunyanyasa waliobaki.

Tofauti kubwa kati ya vyama hivi visiwani ni kwamba chama kimoja kina nguvu za dola; kingine kina nguvu ya umma.

Na kama anayetangazwa mshindi anakuwa ametoka kwenye chama dola, huku akiwa amemtangulia mshindani wake kwa asilimia ndogo, ni mazingira tosha ya kusukuma hoja ya wapinzani kwamba walio madarakani wamekuwa wanajipachika ushindi kwa kutumia vyombo vya dola na kodi ya wananchi.

Ni mazingira haya haya yaliyosababisha hekima ya Mwalimu Julius Nyerere aliyewashauri Wazanzibari kuunda "serikali ya umoja wa kitaifa" ambayo CCM imekuwa ikiigomea kwa zaidi ya miaka 12 sasa.

Ni kutokana na uzito wa ujumbe uliomo kwenye hekima hii kwamba Kamati ya Mwafaka iliyoundwa na Rais Kikwete kushughulikia mpasuko wa kisiasa Zanzibar, ilifikia mahali pa kukubaliana kwamba hatima ya Zanzibar ni katika vyama vikubwa kuongoza kwa ushirikiano.

Hii ndiyo hekima iliyowashinda Dk. Salmin, Amani Karume na Kikwete, kiasi cha kusababisha minong'ono sasa kwamba rais aliposema anatafuta njia ya kumaliza mpasuko huo hakujua au hakuamini alichokuwa anasema.

Kushindwa kwao kutambua hekima hii ya Nyerere ndicho chanzo cha vurugu za sasa Zanzibar, kutokana na CCM kukataa mapenedekezo ya kamati ya rais kuhusu serikali ya mseto visiwani.

Kukosekana kwa hekima hii ndiko kunawafanya asilimia 51 kuwabeza asilimia 49 na kuwatenga katika mikakati ya maendeleo ya kisiasa.

Na mwendelezo huu wa ugomvi kama ulivyo Zanzibar umekuwa "ustaarabu" wa kisiasa wa CCM hata katika majimbo ya uchaguzi nchi nzima.

Kwa kuwa Halmashauri nyingi zinaongozwa na CCM, na kwa kuwa chama hicho kina wabunge na madiwani wengi zaidi, imejengeka dhana potofu kwamba "walioshinda waachwe wafanye watakavyo, watekeleze sera za chama chao."

Lakini inapofika zamu ya chama kingine kushika "dola ya halmashauri" ? kama kilivyo CHADEMA kule Tarime, Karatu, Moshi Mjini na Kigoma; au kama kilivyo CUF kisiwani Pemba.

Hata pale chama hicho kinapotaka kutekeleza sera yake kwa kutumia kanuni ile ile inayotumiwa na CCM, serikali na chama tawala huingilia na kukwamisha shughuli za maendeleo kwa itikadi za kisiasa!

Tarime ni mfano mzuri. Wakati CHADEMA kimekuwa kinasisitiza kwamba sehemu ya kodi ya wananchi iitumike kulipia karo za watoto wanaoshinda mitihani ya elimu ya msingi kuanza sekondari, serikali imeingilia kati na kuwalazimisha wazazi walipe hela za michango ya shule na kulipa karo hizo, hata kama wengi wao hawana vyanzo vya kuaminika vya mapato.

Kule Karatu, Mbunge wao, Dk. Willibrod Slaa, amekuwa akipambana kijasiri dhidi ya mbinu za chama tawala na serikali zinazolenga kukwamisha utekelezaji wa sera za CHADEMA katika halmashauri ambayo CCM ni chama cha upinzani!

Je, inakuwaje mshindi anachukua yote anapokuwa wa CCM, lakini anazuiwa kuchukua yote anapokuwa ametoka chama kingine?

Na kwa nini tuendeleze ugomvi na mgawanyiko wa kiitikadi hata baad aya mshindi wa kura kutangazwa na kuapishwa?

Kwa nini rais au mbunge apendelee watu wa chama chake wakati akijua yeye ni kiongozi wa wote, hata waliomkataa?

Kwa nini tung'ang'ania siasa za kutugawa badala kuzifanya zituunganishe?

Hapa ndipo tunapopaswa kuanzia kujadili upya mwelekeo wa siasa zetu za ushindani. Ikibidi turekebishe utaratibu wa uwakilishi, ili walioshinda wapewe nafasi, lakini na wengi walioshindwa washirikishwe na wasikilizwe.

Migogoro ya kisiasa itakoma pale tutakapotambua na kutumia vema dhamana ambayo wananchi huwapa viongozi na wawakilishi wao. Anayeshinda awe wa wote si wa kundi la wachache ndani ya jamii ya wengi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: