TUICO yameguka


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 11 March 2009

Printer-friendly version
NBC yatangaza kujiondoa rasmi
Yaungwa mkono na wengine

UWEZEKANO wa kumeguka kwa Shirikisho la Wafanyakazi wa Taasisi za Fedha na Viwanda Tanzania (TUICO), sasa ni wazi.

Tayari tawi la TUICO la Benki ya Biashara (NBC Limited) limesimamisha michango ya wafanyakazi wake kwa TUICO-Taifa, ipatayo Sh. 12 milioni kila mwezi kuanzia Februari hii.

Habari za kuaminika zilizopatikana juzi Jumatatu, zimeeleza kuwa shirikisho jipya la wafanyakazi lingeweza kusajiliwa wakati wowote wiki hii.

Msemaji wa TUICO-NBC alilieleza MwanaHALISI kuwa mashirika na makampuni mengine makubwa tayari yamekubali kujimega kutoka TUICO-Taifa kutokana na kile walichoita “kutoridhishwa na uongozi wa sasa unaodaiwa kusimama zaidi na menejimenti kuliko wafanyakazi.”

Haikufahamika haraka ni matawi ya makampuni na mashirika yapi yako pamoja na NBC, lakini kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa TUICO Benki ya National Microfinance (NMB), Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Kiwanda cha Saruji Tanga (Tanga Cement) “yameonyesha nia.”

Taarifa ya TUICO-NBC iliyopelekwa kwa Katibu Mkuu wa TUICO-Taifa kumuarifu kusitisha michango ya wafanyakazi, ilitolewa tarehe 23 Februari 2009.

Barua iliyosainiwa na Iddi Jan Mbona, Mwenyekiti NBC-TUICO na Katibu Zablon Yebete kwenda kwa Mkuu wa Huduma za Wafanyakazi NBC Makao Makuu, inasitisha upelekaji TUICO-Taifa michango ya wafanyakazi wa benki hiyo.

“Tafadhali elewa kuwa kwenye mkutano wa wafanyakazi/wanachama wa TUICO-NBC uliofanyika 16 Februari 2009, iliamuliwa kwa pamoja kuwa makato ya asilimia mbili (2%) kutoka kwa wafanyakazi wa NBC ambayo hulipwa makao makuu ya TUICO yasiwasilishwe huko hadi utakaposhauriwa upya…” imeeleza barua hiyo.

Barua hiyo inasema hundi iliyokuwa imeandikwa kwa ajili ya wasilisho la makato ya Februari, “isimamishwe au iwasilishwe kwa walioweka saini barua hii kwa ajili ya hifadhi salama.”

Mgogoro wa sasa umeibuliwa na hatua ya TUICO-Taifa kumwondoa Alquin Senga katika Kamati ya Majadiliano ya NBC.

Kamati ya Majadiliano ya NBC huundwa na wajumbe 10. Tisa kati yao ni wafanyakazi wa benki hiyo na mmoja hutoka TUICO-Taifa (Senga).

Wajumbe kutoka NBC Limited ni Iddi Mbona (Mwenyekiti), Yebete (Katibu), Doscar Vuhalula, William Mapella, Jephta Mallaba, Christopher Mbatta, Joseph Mbonyi, Sophia Msuya na Said Mohamed.

Kwa takriban miaka mitano sasa, wafanyakazi wa NBC wamekuwa katika mvutano na menejimenti ya benki hiyo iliyonunuliwa na mabenki ya Afrika Kusini.

Lakini kwa miaka miwili sasa, Senga amekuwa mjumbe kutoka makao makuu ya TUICO anayekaa kwenye Kamati ya Majadiliano ya NBC na ameonyesha umahiri wake katika kujenga hoja na kutetea wafanyakazi.

Kimamlaka, Kamati ya Majadiliano ya NBC hukutana na menejimenti kupanga maslahi ya wafanyakazi.

Kuondolewa kwa Senga kwenye kamati hiyo kunachukuliwa sasa na TUICO-NBC kuwa njama za kudhoofisha msimamo na madai ya wafanyakazi NBC.

Kuanzishwa kwa shirikisho jipya kunatarajiwa kuungwa mkono na matawi ya TUICO nchi nzima ambayo yana madai mbalimbali dhidi ya uongozi wa sasa.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Majadiliano inayoundwa na wafanyakazi wa NBC, Zablon Yebete, alithibitisha juzi Jumatatu, kuwa tayari wamepitisha uamuzi wa kusitisha malipo ya Sh. 12 milioni kila mwezi kutoka makato ya wafanyakazi wa taasisi hiyo ya benki.

Taarifa zimeeleza kuwa uongozi wa TUICO-Taifa umemwondoa Senga katika Kamati ya Majadiliano bila kushirikisha uongozi wa TUICO-NBC, jambo ambalo limeelezwa na NBC kuwa “dharau kwa kamati.”

Katibu Mkuu TUICO-Taifa, Boniface Yohana Nkakatisi, anadaiwa kukana kufanya mabadiliko hayo, na kwamba ni Senga ambaye aliamua “kumpisha mtu mwingine.”

Hata hivyo, Mwenyekiti wa TUICO-Taifa Omari Ayoub, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA), anadaiwa kusema kuwa mabadiliko hayo ni halali na kwamba yalifanywa na uongozi wa juu akiwamo yeye, Nkakatisi, ambaye ni Katibu Mkuu na Senga.

Habari kutoka mikoani zinasema Katibu Mkuu wa TUICO, Nkakatisi anazungukia mikoa yote nchini, hasa matawi ya NBC akishawishi wafanyakazi kukataa kuungana na uongozi wa makao makuu.

Tayari ameripotiwa kuwa Tanga na Jumapili iliyopita aliripotiwa kuwa Arusha kwa shughuli hiyohiyo.

Nkakatisi anashutumiwa kwa kukataa kukutana na ujumbe wa TUICO-NBC pale ulipokwenda kumwona ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Wafanyakazi wa NBC Dar es Salaam ndio wawakilishi halali wa wafanyakazi wa matawi yote ya benki hii nchi nzima.

MwanaHALISI lilimtafuta Katibu Mkuu Nkakatisi lakini alikata simu mara mbili. Awali, alikataa kuzungumza lakini kwa mara ya pili alipokea na baada ya mwandishi kujitambulisha alikata simu. Alipotafutwa tena na tena, simu yake haikuweza kupatikana.

Kumeguka kwa TUICO kunapeleka ishara kuwa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) nalo litameguka.

TUICO ni mwanachama wa TUCTA na mgogoro unaoendelea ndani ya TUCTA, ambao umesababisha Katibu Mkuu wake Nestory Ngulla kusimamishwa na kuchunguzwa kwa tuhuma za ubadhirifu, unamhusu pia mwenyekiti wake, Omari Ayoub.

0
No votes yet