Tuige ya maana yatakayotukomboa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

DUNIA tunayoishi leo ina changamoto nzito na ngumu kupata jibu la haraka juu ya ni kwa nini kitu fulani kinafanywa hivi na si vile. Waweza kujiuliza maswali mengi mazito katika kila kitu kinachotokea katika jamii, lakini usipate jibu la ni nini kinasababisha mambo fulani yatokee.

Kwa mfano, mwanasiasa mmoja hivi karibuni alinieleza kwamba katika upigaji wa kura za maoni ndani ya CCM, mchakato uliolalamikiwa kugubikwa na vitendo vingi vya rushwa, ilikuwa vigumu kusema fedha pekee ingemvusha mgombea.

Mwanasiasa huyo aliniambia katika jimbo la Ubungo, hakukuwa na ubishi kwamba mchuano ulikuwa miongoni mwa watu watatu, hawa ni Shamsa Mwangunga, Waziri wa Maliasili na Utalii; Hawa Ng’umbi, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe na kada wa CCM na mjumbe wa NEC, Nape Nnauye.

Lakini mwanasiasa huyo alinieleza kwamba siasa ina maajabu yake. Alisema aliyekuwa na fedha nyingi zaidi ni Mwangunga; lakini aliyekuwa na uwezo wa kujieleza na kuteka jukwaa zaidi alikuwa Nape, na kwa aliyekuwa na mikakati ya kujipenyeza kwa wapigakura ndani ya CCM alikuwa Ng’umbi.

Kwa upeo wake matokeo ya kura za maoni jimbo la Ubungo hayakuamuliwa kwa fedha au uwezo wa kujieleza na kwa maana hiyo uhodari wa kujinadi na kunadi sera, ila kwa mbinu za kujipenyeza.

Ingawa sikukubaliana moja kwa moja na uchambuzi wa kada huyo, lakini itoshe tu kusema siasa za Tanzania kwa sasa zina mambo mengi ambayo huwezi kujua ni kwa nini yanatokea. Hata profesa wa sayansi ya siasa inakuwa vigumu kwake kusema kwa hakika haya yanatokea kwa sababu hizi na hizi.

Hata hivyo, tunaponzungumza mikakati ya kujipenyeza kwa wapigakura kwa maana ya Tanzania , ni kujipenyeza tu bila kuwa na chochote kwa kuwa tumesikia wengi wakisema kwamba ndani ya mchakato wa uchaguzi kwa sasa “mkono mtupu haulambwi?”

Wakati nikitafakari tafakari ya kada huyo wa CCM, kadri siku zinavyokaribia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu, nimekuwa najiuliza maswali mengi ya msingi juu ya mwenendo wa kampeni za wagombea urais. Swali langu ni juu ya kuzidi kutanda kwa mabango ya mgombea urais wa CCM kila kona. Kila uchao yanaibuliwa mapya katika kona tofauti.

Hakuna ubishi kwamba mabango ya wagombea yanatengenezwa kwa gharama kubwa, swali lingekuwa mbona bango halizungumzi ni kwa nini basi fedha nyingi kiasi hiki zitumike kwenye mabango wakati mgombea angeweza tu kutumia majukwaa ya kisiasa kijinadi?

Hali hii ndiyo ilinikumbusha kile wataalam wa siasa wanachokiita kwa lugha ya kimombo “Image over substance.” Kwa tafasiri isiyo rasmi “muonekano unafunika hoja”.

Mbinu hizi zimekuwako kwa miaka mingi katika safu za siasa hasa kwa mataifa yaliyoendelea. Kwa mfano miaka ya mwanzo ya themanini aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, ‘mwana mama wa chuma’ Margaret Thatcher, aliwahi kutumia mbinu hii.

Katika moja ya mikutano ya chama chake cha Conservative kuelekea uchaguzi mkuu, jukwaa la kukaa viongozi wakuu lilikuwa limebandikwa picha kubwa ya mwanamama huyo akiwa anaangalia vifaru vya taifa hilo wakati nchi hiyo ilipopigana na Argentina katika vita ya visiwa vya Falklands na ambayo nchi yake ilishinda.

Picha hiyo kubwa kwenye mkutano wa Conservative ilikuwa inawakilisha ujumbe mmoja tu, kwamba mnaye kiongozi hodari, shupavu ambaye hata kwenye vita hakuna cha kuhofu.

Hali hiyo ilimuongezea umaarufu Thatcher ambaye alidumu madarakani kwa takribani muongo mmoja tangu 1979 hadi 1990 kama Waziri Mkuu wa Uingereza.

Kwa nini mbinu za mabango ni muhimu kwa wanasiasa? Aghalabu huondoa watu kwenye mambo ya msingi kama vile kujadili uchumi, maisha ya watu kwa ujumla, mustakabali wa taifa katika mambo mengi ya maana na kuibua tu hoja za muonekano. Hili hufanywa si kwa bahati mbaya katika kampeni za siasa, ila ni mkakati wa ndani kabisa wa kugeuza upepo wa kisiasa usielekee kwenye mambo ya msingi ila muonekano tu.

Ndiyo maana tunapotazama mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu wa sasa, hasa kwenye ngazi ya urais, tafakari ya wingi wa mabango na staili mpya inayoonekana kwa sasa tofauti na mwaka 2005, ni aina nyingine ya kuwasilisha ujumbe kama ule wa Thatcher mwaka 1983 baada ya kushinda vita vya Falklands.

Pamoja na kutambua kwamba mataifa yaliyopiga hatua kubwa kimaendeleo yanaweza kufanya siasa za ziada (surplus) kwa sababu wamevuka hatua ya kuzungumzia mahitaji muhimu ya binadamu; chakula, mavazi na malazi, kwetu ni jambo linalostahi kuepukwa kwa sababu hatuna nguvu za kumudu ziada hiyo.

Ni hatari kwa taifa linalijikongoja kutoa elimu kwa watu wake, vituo, zahanati na hospitali za serikali zikiwa hazina huduma muhimu; tukishindwa kutimiza mambo muhimu ya msingi katika kusaidia watu wetu, matumizi ya dhana hiyo ya ‘image over substance’ ni hatari kwa ustawi wa jamii.

Lakini hali yote inatupa tafsiri moja juu ya siasa zetu, nakumbuka wakati sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa inajadiliwa na Bunge la 1995-2000, aliyekuwa mbunge wa Mtera na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu, John Malecela, alitetea hoja ya vyama vya siasa kupewa fedha nyingi (ruzuku) kwa kile alichosema ni gharama ya demokrasia.

Zinatakiwa fedha za kukoga watu kwenye kampeni, magari makubwa ya kifahari, mabango kila kona na kila aina ya mbwembwe bila kujali kwamba wapo watu wanaolala njaa, wakishindwa kumudu hata mlo mmoja kwa siku.

Kama haki ingekuwa inatawala katika kuamua jinsi ya kutumia rasilimali zetu chache tulizonazo, hakina siasa za kujisumbua sana na muonekanao kuliko mambo ya kimsingi zisingepata nafasi na kwa maana hiyo tungeelekeza fedha nyingi pale kwenye mahitaji halisi.

Ni katika kutafakari hali hii, mtu anapaswa kujiuliza taifa hili litakabili vipi mambo yake ya vipaumbele kama wagombea wanajinadi wao na si masuala ya msingi kwa ustawi wa taifa hili.

0
No votes yet